WAKALA WA HUDUMA ZA FEDHA AUAWA KWA KUPIGWA RISASI NA WANAODAIWA KUWA MAJAMBAZI


Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi

NA HALIMA KHOYA, SHINYANGA.


Mkazi wa Butengwa Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga Richard Nzumbe ambaye ni wakala wa huduma za fedha amefariki dunia baada ya kuvamiwa na na waodhaniwa kuwa majambazi na kupigwa Risasi akiwa anaingia nyumbani kwake akitokea kwenye duka lake la huduma za fedha.


Tukio hilo la uvamizi kwa kutumia silaha uliosababisha kifo cha Richard Nzumbe,limetokea Desemba 19,2022 majira ya saa 1 usiku katika Kata ya Butengwa Manispaa ya Shinyanga Mkoani humo.




Akieleza juu ya tukio hilo Mwenyekiti wa Mtaa Butengwa,Onesmo Mayeba,amesema majira ya saa 1 usiku alipewa taarifa na mwananchi juu ya tukio hilo ambapo alifika eneo husika na kukuta majambazi hao wamekwisha tenda uvamizi huo huku ikisemekana lengo la kufanya uvamizi huo ni kuwania fedha kutoka kwa marehemu Richald.


“Tukio hili ni la kikatili na tunalilaani kwa sababu majambazi hawa wametoa uhai wa mtu ambapo ni kosa la jinai,hivyo tunaliomba jeshi la polisi kuwabaini wote waliohusika kutenda mauaji hayo na kuwapa adhabu kulingana na Sheria”,amesema Mayenda.


Awali akieleza undani wa tukio hilo Shemeji wa marehemu,Salome Dady, amesema majira ya saa 1 usiku walikuwa ndani yeye na watoto wa dada yake,ndipo waliposikia gari la shemeji yake likiwa limefika getini ambapo mtoto wake alienda kufungua geti hilo ndipo aliposukumwa na majambazi hao na kumfuata marehemu kisha kumfanyia unyama huo.


"Tulikuwa ndani mimi na watoto wa dada mara tukasikia gari likiwa getini ambapo alienda mtoto wa dada kufungua mlango ndipo nikasikia kelele nje ikabidi nitoke nikaone kuna nini nikakuta watu wawili wanampiga risasi shemeji ikabidi nichukue stuli nikampiga mmoja akaanguka halafu nikaenda kuchukua kisu nikamchoma nacho mwingine ndiyo wakachukuana wakaondoka", ameeleza Salome Dady.


Aidha Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa Shinyanga,ACP,Janeth Magomi Amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema Jeshi la polisi linaendelea na msako wa kina kuwabaini waliohusika na tukio hilo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments