VIONGOZI WA DINI YA KIISLAMU WALAANI MATUKIO YA ULAWITI KWA WATOTO

Viongozi wa dini ya kiislamu wamelaani vikali matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia yakiwemo ya ulawiti kwa watoto wa kiume ambayo yamekuwa yakiripotiwa kutokea katika mikoa mbalimbali nchini.


Wakizungumza Novemba 26, 2022 kwenye sherehe ya kuzaliwa Mtume Mohamed (S.A.W) iliyoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa Mwanza, viongozi hao walisema wale wote wanaojihusisha na vitendo vya ukatili ikiwemo ulawiti kwa watoto wa wenzao wenzao hawatakuwa salama kwani hata maandiko matakatifu yamekemea vikali vitendo hivyo.


Sheikh Mohammed Kusoma kutoka Nakuru nchini Kenya aliyekuwa mgeni rasmi kwenye sherehe hiyo iliyofanyika katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, alisema uislamu umekataza matukio ya ukatili hivyo yeyote anayekiuka atalaaniwa.


"Mwenyezi Mungu amewalaani wale wote wanaowafanyia watoto wa wenzao vitendo vya ukatili ikiwemo lawiti/ ulawiti, uislamu pia umekataza hivyo yeyote anayekiuka haya atambue kabisa amelaaniwa" alionya Sheikh Kusoma akihimiza waumini wa dini hiyo kuwa mstari mbele kupinga aina zote za vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.


Naye Sheikh wa Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke alisema matukio mengi ya ukatili wa kijinsia ni matokeo ya mmomonyoko wa maadili katika jamii na hivyo kutoa rai kwa waumini wa dini hiyo kumtanguliza Mtume katika mipango yao hatua itakayowasaidia kuwa salama.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kuzuia ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake KIVULINI, Yassin Ally alisema jamii inapaswa kuzingatia malezi bora kwa watoto wote, wa kike na wa kiume kwani siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la vitendo vya ulawiti kwa watoto wa kiume ambao hapo awali waliachwa wenyewe tofauti na watoto wa kike ambao waliangaliwa kwa umakini zaidi.


Kwa mujibu wa ripoti ya jeshi la polisi kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba 2022, kulikuwa na matukio ya ukatili wa kijinsia 4,797 yaliyohusisha ubakaji huku matukio ya ulawiti yakiwa ni 1,044.


Hayo yamejiri wakati mataifa mbalimbali duniani yakiungana kuadhimisha Siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ambapo taasisi ya KIVULINI inashirikiana kwa ukaribu na BAKWATA kutoa elimu kwa jamii kujiepusha na mtukio ya ukatili wa kijinsia.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Sheikh Mohammed Kusoma kutoka Nakuru nchini Kenya akizungumza kwenye sherehe ya Maulid ya Mtume Mohammad (S.A.W) iliyofanyika katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Sheikh Mohammed Kusoma kutoka Nakuru nchini Kenya akizungumza kwenye Maulid ya Mtume Mohammad (S.A.W) ngazi ya Mkoa Mwanza iliyoandaliwa na BAKWATA mkoani Mwanza.
Sheikh wa Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke akizungumza kwenye maadhimisho ya kuzaliwa kwa Mtume Mohammad (S.A.W) iliyofanyika ngazi ya Mkoa Mwanza katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Sheikh wa Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke akitoa nasaha zake kwenye Maulid ya Mtume Mohammad iliyofanyika ngazi ya Mkoa Mwanza katika uwanja wa Nyamagana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akitoa salamu zake kwenye maadhimisho hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally (mwenye vinasa sauti) akizungumza kwenye Maulid ya Mtume Mohammad (S.A.W) iliyoandaliwa na BAKWATA Mkoa Mwanza.
Sheikh Mohammed Kusoma kutoka Nakuru nchini Kenya akiongoza dua la kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake wakati wa Maulid ya Mtume Mohammad (S.AW) iliyoandaliwa na BAKWATA Mkoa Mwanza.
Sheikh Mohammed Kusoma kutoka Nakuru nchini Kenya akiongoza dua la kuliombea Taifa na viongozi wake wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Sheikh wa Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke akiongoza maandamano kutoka ofisi za BAKWATA kuendelea uwanja wa Nyamagana kwenye sherehe za Maulid ya Mtume Mohammad (S.AW).
Maandamano kutoka ofisi za BAKWATA kuendelea uwanja wa Nyamagana kwenye sherehe za Maulid ya Mtume Mohammad (S.AW).
Maandamano kutoka ofisi za BAKWATA kuendelea uwanja wa Nyamagana kwenye sherehe za Maulid ya Mtume Mohammad (S.AW).
Jumbe mbalimbali za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Jumbe mbalimbali zikihamasisha jamii kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments