MVUVI ALIYEOKOA WATU NDEGE YA PRECISION AIR IKIWA ZIWANI APEWA MCHONGO ZIMAMOTO NA UOKOAJI


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimpongeza na kumfariji kijana Jackson Majaliwa kwa ushujaa wake wa kuwahi katika eneo ilipotokea ajali ya ndege ya Shirika la Precision na kuwaokoa abiria waliokuwa wameshindwa kutoka ndani ya ndege hiyo. Maombolezo ya kuaga miili ya watu wa ajali hiyo yamefanyika katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba Mkoani Kagera 7/11/2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

Kijana aliyefahamika kwa jina la Majaliwa Jackson ambaye anafanya shughuli za Uvuvi katika Ziwa Victoria amependekezwa kuingizwa kwenye Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kupata mafunzo zaidi katika Jeshi hilo baada ya kuonyesha ujasiri mkubwa katika zoezi la uokoaji wa Manusura wa ajali ya Ndege ya Precision Air iliyotokea Novemba 6, 2022 katika Ziwa Victoria mkoani Kagera.


Agizo hilo limetolewa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye yupo ziarani nje ya nchi, kupitia kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alitoa hotuba katika zoezi la kuaga miili ya watu 19 waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo.


“Kwa ujasiri alionyesha Kijana huyu, Mhe Rais ameagiza Kijana huyu akabidhiwe kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ili apate mafunzo ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kupata mafunzo zaidi ya Uokoaji”, amesema Kassim Majaliwa.


Aidha, Waziri Mkuu ameagiza Serikali kuhakikisha Wavuvi waliopo kwenye eneo hilo la Ziwa Victoria wanapatiwa mafunzo ya Uokoaji.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali itagharamia mazishi ya watu wote waliofariki kwenye ajali hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments