WAZIRI SIMBACHAWENE ATAKA WANANCHI KUSHIRIKI UZINDUZI WA MATOKEO YA MWANZO YA SENSA


Waziri wa nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu George Simbachawene.

Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog -DODOMA

WAZIRI wa nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu George Simbachawene amewataka wananchi mkoani hapa na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio la uzinduzi wa matokeo ya mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi ya Mwaka 2022 utakaofanyika katika uwanja wa michezo wa Jamhuri Oktoba 31, 2022.


Simbachawene amesema hayo leo Jijini hapa wakati akizungumza na Waandishi wa habari na kueleza kuwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Uzinduzi huo.


Mbali na uzinduzi huo Waziri Simbachawene ameeleza kuwa Rais Samia pia atazindua Mwongozo Maalum wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ambao lengo lake kuu ni kuhakikisha matokeo ya Sensa yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.


Waziri huyo pia amesema katika uzinduzi huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Marais hao wastaafu watatunukiwa tuzo maalum kwa kufanikisha Sensa katika vipindi vya uongozi.



"Oktoba 31 ni siku maalum kwa taifa letu hivyo basi hatuna budi kuhakikisha kwa tuliopo Dodoma na mikoa ya jirani tunajitokeza kwa wingi uwanja wa Jamhuri na wale tutakaokuwa mbali tufuatilie uzinduzi huo kupitia vyombo vya habari ili tushiriki pamoja na Mheshimiwa Rais kujua tupo wangapi wakati atakapotangaza Matokeo hayo ya Mwanzo,"amesema


Amesema kuwa uzinduzi huo ni tukio muhimu katika historia ya maendeleo ya nchi ndio maana Serikali imeamua kuhakikisha kunakuwa na uwakilishi wa wananchi wa makundi yote ili waweze kushiriki katika tukio hili la kihistoria.


"Sensa ya Watu na Makazi hufanyika mara moja kila baada ya miaka kumi na matokeo yake ndio yanayotumika katika kufanya maamuzi yote muhimu yanayohusu maendeleo ya nchi kwa kipindi cha miaka kumi hadi Sensa nyingine,hivyo
Sherehe hizi za uzinduzi wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 zitahudhuriwa na viongozi wote wakuu wa Serikali pamoja na Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marais wastaafu wa Zanzibar,"amesema


Amewataja Waalikwa wengine kuwa ni viongozi wa Serikali wakiwemo mawaziri na manaibu waziri, Makatibu wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu wa Serikali zetu zote mbili, Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar, viongozi wa vyama vya Siasa na wawakilishi wa makundi mbalimbali katika jamii.


"Matokeo haya ni muhimu sana kwa makundi yote katika jamii, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji na hasa kwa Serikali yetu inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwani Serikali itaweza kupanga mipango yake kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kulingana na idadi, mahitaji na mazingira wanamoishi,"amesema


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments