TANZANIA YACHAGULIWA KWA KUSHINDO KUWA MJUMBE WA BARAZA TENDAJI LA SHIRIKA LA MAWASILIANO DUNIANI - ITU



Na Mwandishi WetuBucharest

 Tanzania imechaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Shirika la Mawasiliano Duniani ITU, uchaguzi uliofanyika kwenye Mkutano Mkuu wa Shirika hilo uliofanyika jijini Bucharest, nchini Romania.



Tanzania ilishika nafasi ya kwanza miongoni mwa wagombea wa SADC baada ya kupata kura 141 kati ya jumla ya kura 180.

 Taifa hilo la Afrika Mashariki litakuwa miongoni mwa mataifa 13 yatakayowakilisha Kanda 'D' kuanzia 2023 hadi 2027, ukiwa ni muhula wa miaka minne kabla ya uchaguzi mwingine kufanyika katika Mkutano Mkuu wa ITU 2027.


Kwa kura zao kwenye mabano, mataifa mengine yafuatayo yalichaguliwa katika kundi ‘D’ pamoja na Tanzania kwenye kundi hilo: Ghana (145), Kenya (146), Misri (142), Tanzania (141), Algeria (138), Morocco
(138), Senegal (137). ), Nigeria (136), Tunisia (133), Mauritius (131), Rwanda (131),
na Uganda (127).


Akizungumzia ushindi huo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Nape Moses Nnauye ameweka bayana jitihada ambazo Serikali
imekuwa ikizifanya kuwezesha ushindi huo kupatikana.


“Dunia kwa kutambua kazi nzuri inayofanywa na Rais wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika kusimamia TEHAMA ndani ya nchi na Kimataifa imeshinda kwa kishindo kuwa Mjumbe wa Baraza hili”, alibainisha Waziri Nape.


Katika Mkutano huo Tanzania imewakilishwa na wataalamu wa sekta ya
Mawasiliano kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
walioambatana na wataalamu wengine wa taasisi za Mawasiliano wakiwemo TCRA,
UCSAF na TTCL.


Mchakato wa kuwania Nafasi hiyo ulianza baada ya kuundwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Mkutano huo ambayo iliratibu kazi mbalimbali zilizowezesha Tanzania kurejea
tena kwenye Baraza hilo muhimu katika sekta ya Mawasiliano.



Kuchaguliwa kwa Tanzania kwenye Baraza hilo kuwa Mjumbe anaewakilisha Kundi
‘D’ linalohusisha nchi za Afrika unaipa nchi Nafasi muhimu na adhimu kutetea
masuala ya Mawasiliano yanayohusu ukuzaji wa teknolojia za Mawasiliano na
namna zinazovyoathiri Maisha ya wananchi kila siku.


Awali kabla ya uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza hilo Tendaji, wajumbe wa nchi 193 wanachama wa Shirika hilo walimchagua Bi. Doreen Bogdan-Martin wa Marekani
kuwa Katibu Mkuu Mtendaji wa ITU, shirika la Umoja wa Mataifa lenye dhamana ya
kusimamia masuala ya Mawasiliano duniani, ukiwemo mgawanyo wa masafa ya
Mawasiliano, masuala ya Mawasiliano ya satelaiti, usambazaji wa huduma za
Mawasiliano na ukuzaji wa teknolojia za Mawasiliano miongoni mwa masuala
mengine.


Pamoja na mchango wa Wizara inayosimamia sekta ya Mawasiliano, Wizara ya Mambo ya Nje pamoja na Balozi mbalimbali za Tanzania pia zilishiriki kikamilifu kuhakikisha Tanzania inatambulishwa vilivyo kwa nchi wanachama wa ITU, hatua iliyowezesha ushindi huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments