MABUSHI ACHAGULIWA KUWA ASKOFU MKUU WA MAKANISA YA IEAGT TANZANIA

Askofu wa Kanisa la IEAGT Mjini Shinyanga David Mabushi, (kulia) ambaye kwa sasa pia ni Askofu Mkuu wa Makanisa ya IEAGT Tanzania, akizungumza mara baada ya kuibuka mshindi kwenye uchaguzi.

Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA

Umoja wa Kanisa la International evangelical Assemblies of God Tanzania (IEAG) kwa mara ya kwanza limefanya uchaguzi wa viongozi wa baraza la umoja huo, na kumchagua Askofu David Mabushi kuwa Askofu Mkuu wa Makanisa ya IEAGT Tanzania.


Uchaguzi huo umefanyika Oktoba 27,2022 katika Kanisa la IEAGT lililopo mkoani Shinyanga ambapo watumishi wa Mungu wa Umoja wa Makanisa ya IEAGT kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, wamepiga kura kuchagua viongozi wa nafasi ya Askofu Mkuu, Makamu Askofu Mkuu, Katibu Mkuu, Muwekahazina wa umoja wa baraza hilo.

Akizungumza mara baada ya zoezi la upigaji kura kwenye uchaguzi huo Mwenyekiti Mtendaji bodi ya wadhamini Kanisa la IEAGT ambaye pia ni msimamizi wa uchaguzi huo Lucas Lugwila, amesema uchaguzi huo umefanywa na wajumbe wapatao 71, wa dhehebu la IEAGT kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.

Mara baada ya zoezi la upigaji kura kumalizika msimamizi wa uchaguzi Lucas Lugwila amemtangaza Askofu David Mabushi kuwa ndiye Askofu Mkuu wa Umoja wa Kanisa la INTERNATIONAL EVANGELICAL ASSEMBLIES OF GOD TANZANIA (IEAGT), kwa kupata kura 68 kati ya kura 71 zilizopigwa.

“Nafasi ya Askofu Mkuu, David Mabushi ameibuka mshindi kwa kupata 68, nafasi ya Makamu Askofu Mkuu mshindi ni Simon Laizer amepata kura 58, nafasi ya Katibu Mkuu mshindi ni Flagson Ndibwa kwa kura 46 na nafasi ya Mwekahazina mshindi ni Timoth Mwantake ambaye amepata kura 58”, amesema Lugwila.

Mara baada ya uchaguzi huo kumalizika Askofu Mkuu David Mabushi akizungumza mbele ya baraza hilo, ameahidi kuendelea kushirikiana na viongozi hao na kuitumikia vyema nafasi hiyo aliyochagulia kwa kusimamia miongozo, Katiba na Misingi iliyowekwa na umoja huo.

Aidha Makamu Mwenyekiti kutoka CPCT taifa, Bartholomeo Sheggah amewapongeza viongozi hao waliochaguliwa, na kuwataka kutumikia vizuri nafasi hizo ili kuendelea kujenga umoja wa kanisa hilo katika msingi mzuri.

Nao baadhi ya Wajumbe wa baraza hilo akiwemo Mchungaji Joseph Jackson amesema wanaimani na viongozi waliowachagua watakwenda kutumika vyema kwenye nafasi zao.

“Jambo la kwanza tunamshukuru mungu ametusimamia tumemaliza salama, ulikua ni uchaguzi mzuri na wa haki, tunawaamini viongozi wetu tuliowachagua na tunaimani watakwenda kufanyakazi kama itakavyompendeza mungu, tutashirikiana nao vizuri”, amesema Mchungaji Jackson.





Mwenyekiti mtendaji bodi ya wadhamini Kanisa la IEAGT mkoani Shinyanga ambaye pia ni msimamizi wa uchaguzi huo Lucas Lugwila akitangaza matokeo ya uchaguzi huo.
Askofu wa Kanisa la IEAGT Mjini Shinyanga David Mabushi, (kulia) ambaye kwa sasa pia ni Askofu Mkuu wa Makanisa ya IEAGT Tanzania, akiwa na Makamu wake Askofu Simon Laizer mara baada ya kupata ushindi kwenye uchaguzi huo.
Viongozi walioshinda kwenye uchaguzi wakiombewa.
Picha ya pamoja ikipigwa mara baada ya uchaguzi kumalizika na washindi kupatikana.
Picha ya pamoja ikipigwa mara baada ya uchaguzi kumalizika na washindi kupatikana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments