TBS YAWANOA MAAFISA KUTOKA MAABARA ZA UBORA NA UCHUNGUZI KUHUSU VIPIMO MWANZA

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Mhe. Amina Makilagi akifungua mafunzo kwa wafanyakazi kutoka maabara za ubora na uchunguzi kuhusu sayansi ya vipimo yaliyoandaliwa na Shirika la Viwango (TBS)mapema leo katika ukumbi wa TMDA Mwanza.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Mhe. Amina Makilagi kufungua mafunzo kwa wafanyakazi kutoka taasisi za maabara za ubora na uchunguzi yaliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika ukumbi wa TMDA Buzuruga Mwanza mapema leo
Washiriki wa mafunzo kutoka maabara za ubora na uchunguzi wakifuatilia mafunzo ya sayansi ya vipimo yaliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambayo yamefanyika leo Nyamagana mkoani Mwanza.


*********

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Mhe. Amina Makilagi amefungua mafunzo kwa wafanyakazi kutoka maabara za ubora na uchunguzi kuhusu sayansi ya vipimo yaliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Mhe. Makilagi amefungua mafunzo hayo Jumanne Septemba 06, 2022 katika ukumbi wa TMDA Buzuruga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhe. Adam Malima.

Mhe. Makilagi ametumia fursa hiyo kuipongeza TBS kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yatakuwa chachu ya kuongeza ufanisi katika maabara zinazofanya vipimo vya ubora na uchunguzi na kutoa majibu sahihi.

"Mwanza ni Mkoa wa kimkakati unaokua kwa kasi, tuna miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi na afya hivyo baada ya mafunzo haya tunategemea kuona mkifanya vipimo vitakavyotoa majibu sahihi na ya kuaminika" amesema Mhe. Makilagi.

Naye Mkurugenzi Mkuu TBS, Dkt. Athuman Ngenya amesema washiriki wa mafunzo hayo watajengewa uwezo kuhusu sayansi ya vipimo (Metrolojia) pamoja na mchakato wa kuangalia ubora wa bidhaa katika vipimo (Ugezi) kwani hizo ni nyenzo muhimu katika uzalishaji akisema "ukikosea vipimo hata bidhaa yako haiwezi kuwa na ubora".

Baadhi ya washiriki akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Mizani TANROADS Mkoa Mwanza, Mhandisi Joseph Kalala pamoja Mwakilishi wa Maabara ya SGS, Suma Mwakyembe wamesema mafunzo hayo ni muhimu na yatasaidia kuleta mabadiliko ya kiutendaji katika taasisi zao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments