WANANDOA WAPIGWA RISASI NA ASIYEJULIKANA WAKIGOMBANA..MTOTO AFARIKI


POLISI jijini Nairobi nchini Kenya wanamsaka mtuhumiwa mmoja wa mauaji ya mtoto ambaye anadaiwa kuwamiminia risasi wanandoa usiku wakati wakizozana nje ya nyumba yao katika eneo la Buruburu.

Katika kisa hicho, Cecilia Mugure, 42, na mumewe Njoroge Wahome mwenye umri wa miaka 47 walifika nyumbani kwao majira ya saa 3.45 usiku kutoka katika kilabu cha pombe, Bee Centre, huko eneo la Umoja.


Kulingana na ripoti iliyowasilishwa katika Kituo cha Polisi cha Kamukunji, wanandoa hao wakiwa wamelewa walikuwa wakirushiana maneno baada ya mwanamke kugoma kuingia ndani ya nyumba yao.

Baada ya mabishano hayo, jamaa aliyekuwa amejihami kwa bastola aliibuka na kuwafyatulia risasi na kumuua mtoto wao wa kiume, James Muriithi mwenye umri wa miaka 19 huku mama akijeruhiwa vibaya.

Mtoto wao mwingine wa kike mwenye umri wa miaka 13 aliambia Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwamba mabishano ya wazazi wake yalidumu takriban saa mbili kabla ya babaake kuingia nyumbani na kuendelea kunywa.


Msichana huyo alisema alimuuliza babaake kuhusu alikokuwa mama yao, lakini hakujibu kamwe, kisha akaamua kumwamsha kaka yake akimtaka wamfuate mama yao. 

Wawili hao walimkuta mama yao akiwa amelala chini kwenye shuka la Kimasai lakini juhudi zao za kumuamsha ziliambulia patupu.


Polisi wanaendelea na msako mkali kumtia nguvuni Jambazi huyo

Muriithi alimtuma dadake ndani ya nyumba amchukulie simu yake na hapo ndipo mauti yalimkumba. Jamaa aliyekuwa amejihami alitokea ghafla na kunza kuwamiminia risasi.


“Alikimbia hadi ndani ya nyumba na alipokuwa anarudi baada ya kuchukua simu, alisikia milio miwili ya risasi na akamuona wazi jamaa akiwa amejihami kwa bastola. Hapo ndipo aliporudi haraka na kumjulisha baba yake kile alichokishuhudia,” ripoti hiyo ilisema.


Mugure alipigwa risasi kidevuni huku Muriithi naye kichwani. Wahome aliwakimbiza katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki, ambapo mwanawe alitangazwa kuwa tayari amekata roho walipowasili.

Mugure alihamishiwa hadi katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) akiwa katika hali mahututi. Mwili wa Muriithi ulihamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Mama Lucy Hospital. Uchunguzi wa mauaji hayo umeanza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments