KIVULINI YATOA TUZO ZA UJASIRI NA UBUNIFU KWA VIONGOZI VINARA WA KUHAMASISHA JAMII KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA MWANZA


Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally (kulia) akimkabidhi tuzo Sheikh wa Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally (kulia) akimkabidhi tuzo Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Mwanza, Isack Ndassa.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally (kulia) akimkabidhi tuzo Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya viongozi wa dini mkoani Mwanza.

 ***
Shirika la kutetea haki za wanawake na watoto (KIVULINI) limetoa tuzo za ujasiri na ubunifu wa kuhamasisha jamii kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kwa viongozi mbalimbali mkoani Mwanza.


Tuzo hizo zimekabidhiwa na Mkurugenzi wa shirika hilo, Yassin Ally Alhamsi Septemba 29, 2022 kwenye kikao kazi cha Kamati ya kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA) Mkoa Mwanza.


Miongoni mwa viongozi waliokabidhiwa tuzo hizo ni pamoja na Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Mwanza Isack Ndassa, Sheikh wa Mkoa Mwanza Hassan Kabeke, Kamati ya MTAKUWWA Mkoa Mwanza pamoja na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa Mwanza.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mkurugenzi huyo wa shirika la Kivulini Yassin Ally alisema kumekuwa na uelewa wa kutosha kwa wajamii kutonyamazia vitendo vya ukatili wa kijinsia ambapo wamekuwa wakifichua vitendo hivyo katika madawati ya jinsia, ustawi wa jamii na hata kwenye vyombo vya habari.


“Sasa tunashuhudia matokeo ya MTAKUWWA yametoa elimu na wanajamii na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini hawanyamazii tena vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani kwa wanawake na watoto tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo ilionekana ni jukumu la wadau kama KIVULINI”, alibainisha Yassin.


Naye Sheikh wa Mkoa Mwanza Hassan Kabeke alisema katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika ndoa, BAKWATA imeanza kutoa mafunzo ya misingi ya ndoa kwa wanaume wa kiislamu kabla ya kufunga ndoa ambapo hapo awali mafunzo ya aina hiyo yalikuwa wakitolewa kwa wanawake pekee.


“Hatua hii itasaidia ndoa kudumu tofauti na sasa ambapo ndoa nyingi huvunjika kutokana na wanaume wengi kutokuwa na ujuzi wa namna bora ya kulea ndoa” ,alisema Sheikh Kabeke.

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم