WAZIRI JAFO AFURAHISHWA NA KIWANDA CHA IRON STEEL LTD KUTUNZA MAZINGIRA



************

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo, amekipongeza kiwanda cha Iron and Steel ltd kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam kwa kuyajali, kuyahifadhi na kutunza mazingira.

Pongezi hizo zimekuja mara baada ya kiwanda hicho kukamilisha kwa ufasaha maelekezo aliyotoa ya kufanya marekebisho kwenye maeneo mbalimbali ili kutunza na kuhifadhi mazingira katika kiwanda hiko.

“Nimefarijika sana kuja kwenye kiwanda hiki leo na kukuta maagizo yote niliyoyatoa yamefanyiwa kazi na kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa hivyo nimeridhishwa kwa asilimia mia moja na kiwanda hiki kiwe mfano wa kuigwa na wawekezaji wengine Nchini kote, Tunahitaji wawekezaji ambao wakipewa maagizo wanatekeleza kwa wakati”. Amesema Dkt. Jafo.

Naye Meneja wa Kanda ya Mashariki Kaskazini kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bwana Arnold Mapinduzi alipotoa ufafanuzi, ameainisha mambo makuu manne ambayo Baraza lilielekezwa kuyasimama ili kiwanda hiko kiyaboreshe kuwa ni

kusimamia suala zima la ukusanyaji wa taka, kutafuta mbinu ya kuzuia moshi unaosambaa kwa majirani wanaozunguka kiwanda na kujenga paa kwa ajili ya kupunguza vumbi kutapakaa kwa haraka.

Nyingine ni kuhifadhi kwa usahihi bidhaa mbalimbali kama vyuma chakavu pamoja na suala la kujenga ukuta ili kutenganisha na mtaro unaobeba maji machafu ambavyo vyote kwa pamoja vimerekebishwa.

Akiongea katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kindondoni Mhe.Godwin Gondwe amemshukuru Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Mhe. Dkt. Selemani Jafo kwa kushirikiana na ofisi yake katika utendaji, Lakini pia kutumia muda wake kutembelea kiwanda hiko ziara itakayoleta tija kwa Mazingira na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Gondwe pia amewataka wenye viwanda wengine kuiga mfano wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira uliofanikiwa sana katika Kiwanda cha Iron and Steel

Aidha Waziri Jafo ameagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha wanapita katika Viwanda vyote Nchini ambako alitoa maagizo ili kujiridhisha na utekelezaji wake, na Kwa wale ambao hawajatekeleza hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao na pia waendelee kupokea malalamiko ya wananchi na kuyatekeleza.

“zamani kulikua na malalamiko kuwa NEMC haifanyi vizuri ila nataka niwaambie kuwa NEMC ya zamani siyo hii ya sasa kwani wanachapa kazi kwa weledi na bidii”.Ameongeza Jafo.

Naye Afisa Uhusiano wa Iron and Steel Ltd Ndg.Idrissa Ali , amesema maagizo yote manne waliyopewa wamekamilisha na kutekeleza kwa weledi na kuishukuru Serikali kwa kushirikiana nao katika ufanikishaji na utunzaji wa mazingira kwa maendeleo endelevu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments