GRAPHITE KUANZA KUCHIMBWA RUANGWA-MAJALIWA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim majaliwa akizungumza na Wananchi wananchi katika vijiji vya Namikulo, Namkatila na Matambarale katika kata ya Chunyu wilayani Ruangwa, Lindi leo Jumanne, Julai 5, 2022.
 
Na Mwandishi wetu -Lindi

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali ipo katika majadiliano na kampuni ya Uranex kwa ajili ya ujenzi wa mgodi wa madini ya bunyu (graphite) utakaoanza hivi karibuni.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Julai 5, 2022) wakati akizungumza na wananchi katika vijiji vya Namikulo, Namkatila na Matambarale katika kata ya Chunyu wilayani Ruangwa, Lindi huku akiwataka wananchi wa wilaya ya Ruangwa kujiandaa kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zitokanazo na ujenzi wa mgodi wa graphite.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kila kwenye rasilimali kabla ya kuanza uwekezaji lazima wahusika wajadiliane na Serikali ili kubaini namna ambavyo itanufaika,"amesema 

Amesema, wakazi wa maeneo hayo watakuwa ndio wanufaika wa kwanza kutokana na shughuli mbalimbali zinakazokuwa zikiendelea kuanzia hatua ya ujenzi hadi uzalishaji.

“Kila shughuli itakayofanyika hapa ni fursa kwetu sisi wana-Namikulo na wana-Ruangwa kiujumla. Tujipange sawa sawa Serikali yenu ipo makini kuhakikisha mnanufaika na mradi huo,"amesema 

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa kampuni ya Uranex, Mhandisi Isaac Mamboleo amesema kampuni yao inatarajia kuanza ujenzi wa mgodi huo katika mwaka huu wa fedha.
Amesema mradi huo ambao utahusisha vijiji saba unatarajia kugharimu shilingi bilioni 625 na utazalisha ajira 950 kati yake ajira 600 wakati wa ujenzi na ajira 350 wakati wa uzalishaji.
Mhandisi Mamboleo amesema kwa sasa wanakamilisha ujenzi wa nyumba 59 zenye gharama ya shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kuwafidia baadhi ya wananchi waliopisha ujenzi wa mradi huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments