WAFUGAJI WALIOTISHIA KUWAPIGA MISHALE WATAFITI WA MAFUTA 'TPDC' KISHAPU SASA WAKUBALI...DC MKUDE ATAJA CHANZO CHA MGOGORO



Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude akiendelea kutoa elimu kwa wafugaji juu ya faida ya mradi huo wa utafiti wa Mafuta.
Na Marco Maduhu, KISHAPU

WAFUGAJI Kabila la Wataturu katika kijiji cha Magalata wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, hatimaye wameridhia wataalamu kutoka Shirika la Maendeleo la Mafuta ya Petroli Tanzania (TPDC) kuendelea na shughuli zao za utafiti wa mafuta kwenye maeneo yao.

Awali wafugaji hao waliwazuia watafiti wa mafuta kuendelea na shughuli zao, wakidai kuwa walianza kufanya shughuli kwenye maeneo yao bila ya wao kuwa na taarifa, ndipo wakaingiwa na hofu huenda Mbuga yao ya Marisho inataka kutwaliwa na kuamua kuzuia utafiti huo.

Baada ya kuibuka kwa mgogoro huo na watafiti hao kutishiwa maisha yao kwa kupigwa mishale, ndipo Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkunde, alipofanya ziara  jana kwenda kuzungumza na wafugaji hao, pamoja na kuwapatia elimu juu ya faida kwao endapo eneo hilo likibainika kuwa na mafuta.

Mkude amesema kitu ambacho amekibaini kwenye Mgogoro huo ni ukosefu tu wa mawasiliano pamoja na elimu kwa wafugaji, kwa sababu utafiti huo wa mafuta hauathiri shughuli zozote za matumizi ya ardhi bali itaendelea kutumika kama kawaida.

Amewasihi wafugaji hao waruhusu shughuli hizo za utafiti wa mafuta ziendelee katika maeneo yao, huku na wao wakiendelea na shughuli zao kwenye Mbuga yao, sababu hakuna kizuizi chochote ikiwa utafiti huo unafanyika kwa uchukuaji sampuli tu za kubaini kama mafuta yapo eneo hilo.

Amesema endapo eneo hilo likibainika kuwa lina mafuta, ndipo taratibu zingine za kisheria zitafuatwa za kuwahamisha, ikiwamo ulipwaji wa fidia pamoja na kutafutiwa maeneo mazuri ya malisho kwa ajili ya mifugo yao, na hakuna mtu ambaye anatonewa bali kila mtu atapata haki yake.

“Mradi huu ni fursa kubwa sana ya kiuchumi endapo ikibainika kuwa mafuta yapo eneo hili, kwanza maisha yenu yatabadilika kiuchumi, mtajengewa nyumba nzuri, kutekelezewa miradi ya kijamii ikiwamo ujenzi wa hospitali, shule, miradi ya maji na miundombinu ya barabara,”amesema Mkude.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kishapu Shija Ntelezu, amewaasa wafugaji hao waupokee mradi huo wa utafiti wa mafuta, kwa sababu una maslahi mapana ya kiuchumi kwa Taifa, na kuwataka wapuuze maneno ya baadhi ya watu ambao wanawapotosha kwa maslahi yao binafsi.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa utafiti wa Mafuta Bonde la Eyasi Wembere kutoka (TPDC) Sindi Maduhu, amesema utafiti huo wa mafuta katika bonde hilo ulianza mwaka 2015, na unafanyika katika Mikoa mitano ambayo ni Arusha, Singida, Tabora, Simiyu, pamoja na Shinyanga.

Amesema shughuli ambazo wanazifanya kwa sasa ni uchukuaji tu wa Sampuli, ambazo baadae zitapelekwa kwenye Maabara nchini Marekani, ili kwenda kupata majibu ya kubaini kama maeneo hayo yana mafuta, na kubainisha kuwa shughuli zao za utafiti huo wa mafuta hazizuii matumizi ya ardhi kuendelea kufanyika.

Mwenyekiti wa Wafugaji katika kijiji hicho cha Magalata Kidonge Magulunga, amesema awali walizuia shughuli hizo za utafiti wa mafuta, kwa sababu walishangaa kuona tu wageni wakifanya shughuli zao kwenye maeneo yao bila ya wao kuwa na taarifa, ndipo wakahofia huenda Mbuga yao inataka kuchukuliwa na kuamua kuzuia utafiti huo.

Amesema kwa sasa baada ya kupata elimu na utambulisho rasmi, wamekubali shughuli hizo ziendelee za utafiti wa mafuta, na wapo tayari kushirikiana nao na kuwahakikisha ulinzi wa kutosha na hakuna ambaye atawasumbua tena wala kuwatishia maisha (kuwapiga mishale), bali watakuwa salama hadi pale watakapomaliza shughuli zao za utafiti.

Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude akizungumza na wafugaji katika kijiji cha Magalata wilayani Kishapu, waridhie shughuli za Utafiti wa Mafuta ziendelee kwenye maeneo yao.
 
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude akizungumza na wafugaji katika kijiji cha Magalata wilayani Kishapu, waridhie shughuli za Utafiti wa Mafuta ziendelee kwenye maeneo yao.

Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude akiendelea kutoa elimu kwa wafugaji juu ya faida ya mradi huo wa utafiti wa Mafuta.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kishapu Shija Ntelezu akizungumza kwenye Mkutano huo.

Diwani wa Mwamalasa Bushi Mpina akizungumza kwenye Mkutano huo.

Meneja Mradi wa utafiti wa Mafuta Bonde la Eyasi Wembere kutoka (TPDC) Sindi Maduhu, akielezea shughuli ambazo watakuwa wakizifanya za utafiti.

Mtaalamu wa utafiti wa mafuta ardhini Renatus Kachira, akitoa elimu namna watakavyokuwa wakitafiti Mafuta.

Mwenyekiti wa Wafugaji katika kijiji cha Magalata Kidonge Magulunga, akizungumza kwenye Mkutano huo na kuridhia shughuli za utafiti wa Mafuta ziendelee.

Wafugaji wakiwa kwenye mkutano.

Wafugaji wakiwa kwenye mkutano.

Mkutano ukiendelea.

Mkutano ukiendelea.

Mkutano ukiendelea.

Mkutano ukiendelea.

Mkutano ukiendelea.

Wafugaji wakiwa kwenye mkutano.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments