SERIKALI YATAKA MEWATA KUHAMASISHA JAMII KUKABILIANA NA MABADILIKO YA MAGONJWA



Waziri Dkt. Dorothy Gwajima akiongea na chama cha madaktari wanawake Tanzania(MEWATA) katika Mkutano wa 19 wa Chama hicho uliofanyika Jijini Dodoma.
Waziri Dkt. Dorothy Gwajima akiongea na chama cha madaktari wanawake Tanzania (MEWATA) katika Mkutano wa 19 wa Chama hicho uliofanyika Jijini Dodoma.

Na Dotto Kwilasa, Malunde1 blog-DODOMA.

WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wanawake na Makundi maalum kwa kushirikiana na Chama Cha Madaktari Wanawake nchini (MEWATA) imejipanga kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya hali ya afya yanayojitokeza na kuziwezesha jamii kuibua mbinu rahisi na sahihi za kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza .


Hayo yameelezwa leo Jiji Dodoma na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima kwenye Mkutano mkuu wa 19 wa MEWATA na kueleza kuwa kupitia wataalamu wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii watahamasisha na kuelimisha jamii yakiwemo makundi maalum ili kuwandaa wananchi kupokea na kukubaliana na mabadiliko ya afya.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo utawezesha kuwapatia wanajamii huduma za kisaikolojia pale wanapokumbana na changamoto mbalimbali za kiafya au taharuki za mlipuko ya magonjwa kama ilivyotokea wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO 19.

Amesema mkutano huo umekuja katika muda muafaka, kwa kuwa mpaka sasa bado Dunia inaendelea kutekeleza jitihada mbalimbali za kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya korona ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu ulimwenguni.

"MEWATA yenye wataalamu wanawake ikishirikiana na wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalamu itaweza kufikisha ujumbe wake kwenye jamii kwa ufanisi zaidi na siyo tu kwa UVIKO 19 bali hata kwa mambo mengine yanayohusu changamoto za afya ili jamii ielewe kwa lugha nyepesi ,"amesema

Pamoja na hayo ameweka wazi kuwa licha ya juhudi zilozopo bado kuna wananchi wengi ambao bado hawajapata elimu ya kutosha ya chanjo ya UVIKO-19 hivyo kuwataka madaktari hao kushirikiana na kuwafikia kwa kuwapa elimu ya afya juu ya magonjwa mbalimbali na kuondokana na mila potofu za jamii zinazopelekea kuathiri afya hasa kwa watoto na wanawake.

"Wito wangu kwenu, tuendeleze jitihada za kulinda afya za akina mama kwani wao ndio chimbuko la familia na nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa kutokana na mchango wao katika uzalishaji, malezi, makuzi na kuimarisha uchumi wa kaya,nawakaribisha pia kufanyakazi nasi kwani maendeleo na ustawi wa jamii unategemea jamii yenye kufanya maamuzi yenye tija juu ya kuboresha afya,"amesisitiza

Mbali na hayo Dkt. Gwajima amesema ili kufikia malengo nguvu ya pamoja inahitajika kwa kuwa jukumu kubwa la sekta ya maendeleo ya jamii ni kuijengea uwezo jamii uelewa wa mambo ili kupokea, kubadilika na kuwajibika kwa kuchukua hatua stahiki kuhusu masuala ya afya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments