NAIBU WAZIRI WA AFYA DKT.MOLLE AKABIDHI VIFAATIBA HOSPITALI YA WILAYA YA MAKETE


Na WAF - Makete, NJOMBE.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel leo amekabidhi vifaatiba kwa ajili ya huduma za matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Makete.

Dkt. Mollel amekabidhi vifaatiba vyenye thamani ya Shilingi Milioni 15 ambavyo vimetolewa na Mfuko wa Doris Mollel wakishirikiana na Segal Family Foundation ili kusaidia watoto njiti wanaozaliwa na akina mama katika Hospitali ya Wilaya ya Makete wanatunzwa vyema na kuwa na afya bora.

Dkt. Mollel ameipongeza Taasisi ya Doris Mollel inayoongozwa na Bi.Doris Mollel kwa kuendelea kusaidia jamii ya Watanzania katika masuala ya uzazi na kuwataka Watanzania wengine na Taasisi mbalimbali nchini kuwa Wazalendo na kujitoa kusaidia jamii.

Awali akizungumza Bi. Doris Mollel amesema kuwa Taasisi yake imekuwa ikijishughulisha na kusaidia Huduma za Uzazi na matunzo ya Watoto Njiti na tayari wamekwishazunguka maeneo mbali mbali nchini na kufanya kazi na Wilaya zaidi ya 45.

"Leo tumekuja hapa Makete kuleta mashine hizi 3 za kufua oksijeni kwa ajili ya watoto njiti, mashine hizi zinauwezo wa kuhudumia watoto sita kwa wakati mmoja" amefafanua Bi. Doris Mollel

Katika tukio lingine Dkt. Mollel amekabidhi vifaatiba vya maabara, Jokofu la kutuza maiti 4 kwa wakati mmoja pamoja na mashine ya kufulia nguo ambavyo vimenuniliwa na Serikali kwa ajili ya kusaidia utoaji wa huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Makete.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Makete Mhe. Festo Sanga ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha huduma za afya katika Wilaya ya Makete.

"Mashine hizi zilizotolewa leo tunaamini zitakwenda kutusaidia sisi wanamakete kuboresha huduma za afya na kuwapunguzia kero hawa wananchi" amesema Mhe. Sanga

Mhe. Sanga ameupongeza Mfuko wa Doris Mollel kwa kufika Makete na kutoa msaada katika Hospitali ya Makete ambayo ilikuwa na uhitaji wa vifaatiba kwa ajili ya kusaidia watoto njiti kuweza kupumua vizuri.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم