TANZANIA KUSHIRIKI ONYESHO LA UTALII HISPANIA

 

Kaimu Meneja wa Utalii wa Mikutano na Matukio, Lily Fungamtama (kulia), akizungumza na wadau kutoka mataifa mbalimbali katika Banda la Tanzania. (Picha na mpigapicha wetu).

NA JUMA ISSIHAKA

KATIKA kuendeleza juhudi za kuvuna soko la watalii kimataifa, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), imeratibu ushiriki wa Tanzania katika Onesho la Utalii lijulikanalo kama Feria Internationale de Madrid (FITUR) nchini Hispania.

FITUR ni moja ya maonesho makubwa ya utalii linaloandaliwa na kampuni ya IFEMA ya Hispania, linatarajiwa kufanyika Machi 19 hadi 23 mwaka huu.

Akizungumzia mkakati wa TTB kuhusu soko la utalii la Hispania, Kaimu Meneja wa Utalii wa Mikutano na Matukio, Lily Fungamtama, alisema Tanzania itaendelea kushiriki na kutumia fursa ya onesho hilo kukutana na wafanyabiashara kutoka katika masoko makubwa ya utalii na kudumisha ushirikiano na nchi nyingine zitakazoshiriki.

Alieleza mwitikio wa mawakala na wageni wengi waliotembelea banda la Tanzania umewapa matumaini ya kuongeza idadi ya watalii kutoka Hispania.

"Wengi wao wameonyesha shauku ya kuja Tanzania hasa baada ya kupata maelezo kutoka kwa washiriki Wataalam kutoka Taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii waliohudhuria katika onesho la FITUR 2022," alisema.

Kwa upande wake, Ofisa aliyewakilisha Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA), Jerome Ndanzi, alisema Mawakala wa Utalii waliotembelea Banda la Tanzania wameridhishwa na maelezo ya vivutio vya utalii katika Hifadhi za Taifa na kujionea video zilizokuwa zikionyeshwa.

Aliongeza kwamba video hizo zimekuwa kichecheo kikubwa kwao kushawishika kuweka nia ya hivi karibuni kuzitembelea hifadhi za taifa na maeneo ya kihistoria yanayosimamiwa na TANAPA.

Naye, Mwakilishi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Mhifadhi Mteleka, alisema onesho hilo limekuwa na manufaa kwao baada ya kufanya mkutano na Juan Carlos ambaye ni mtaalamu wa kuandaa miradi inayofadhiliwa na Serikali ya Hispania.

Alibainisha kwamba mtaalamu huyo ameonyesha dhamira ya kushirikiana na TFS kuandaa andiko la kuimarisha utangazaji wa utalii Ikolojia katika nchi ya Hispania.

Mwakilishi wa kutoka Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA) Tumsime Felician, alisema wageni wamekuwa na shauku ya kupata maelezo kuhusu utalii wa uwindaji.

Alitaja miongoni mwa mawakala hao ni raia wa Mexico aliyeonyesha nia ya kuleta wageni wa uwindaji wa kitalii kutoka nchini humo kuitembelea Tanzania.

Aidha, Ofisa Utalii kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Moinga Lesasi, alisema baada ya kupata maelezo ya mazao ya utalii yaliyopo Ngorongoro, wageni wengi wameonyesha shauku ya kuitembelea Tanzania.

Alieleza moja ya jambo wanalotamani zaidi kushuhudia ni namna binadamu anavyoweza kuishi sehemu moja na wanyama wakali wanaopatikana katika Bonde la Ngorongoro, Historia ya Oldvai Gorge na mengine mengi.

Onesho la FITUR mwaka huu ni la kwanza kufanyika tangu kutokea kwa mlipuko wa janga la UVIKO 19 ambao umeathari sekta ya utalii na ukarimu, kwamba mara ya mwisho lilifayika Januari mwaka 2019.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii za mwaka juzi, mwaka 2020, Tanzania ilipokea watalii 18,838 mwaka 2019 na 4,162 mwaka 2020 kutoka Hispania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments