TPC YATAKIWA KUBUNI HUDUMA MPYA ZA WATEJA KWA KUTUMIA MFUMO WA ANUANI ZA MAKAZI NA POSTIKODI

 Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, mawasiliano na Teknolojia ya habari Teddy Njau akiongea wakati wa mafunzo ya uelewa wa mfumo wa anuani za makazi Jijini Dodoma.

*****


Na Dotto Kwilasa Malunde 1 Blog,DODOMA.

SHIRIKA la Posta Tanzania (TPC) limetakiwa  kutumia mfumo wa anuani za makazi na postikodi kubuni huduma mpya kwa wateja ili utekelezaji wa mfumo huo utakapokamilika uweze kutumika ipasavyo kufikisha huduma na bidhaa kwa wateja.

 

Hayo yameelezwa na jana Jijini hapa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Teddy Njau wakati akifungua semina ya mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu mfumo wa anuani za makazi na postikodi kwa Mameneja wa Mikoa ya Shirika hilo wa Tanzania Bara na Zanzibar.

 

Njau amewataka washiriki hao kuweka anuani za makazi kwenye maeneo yao; kwa wateja wao na kubuni huduma mpya zitakazotumiwa na wateja kupitia mfumo wa anwani za makazi utakapokamilika utekelezaji wake kwa kuwa Shirika hilo lina mtandao mpana nchi nzima na ni wadau wa msingi wanaotakiwa kutumia miundombinu hiyo.

 

“Kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha anuani za makazi zinawekwa na kutumika nchi nzima, leo mnapatiwa mafunzo ya kujenga uelewa ili mkasimamie na kushiriki utekelezaji wa mfumo huu kwenye mikoa yenu Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuwa ninyi ni wadau muhimu na ni wajumbe kwenye kamati za kitaalamu,” amesisitiza Njau

 

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kufungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Wizara hiyo, Caroline Kanuti amesema kuwa mfumo wa anuani za makazi utakuwa wa kidijitali ili kutoa fursa kwa Serikali kutekeleza majukumu ya sensa ya watu na makazi ili anuani zijumuishwe kwenye sensa inayoanza mwezi Agosti mwaka huu.


Ameongeza kuwa utekelezaji wa mfumo wa anuani za makazi utafanyika kwa miezi mitano nchi nzima kwenye kata na wadi 4,174; halmashauri 196 na mikoa 31 ili zoezi hili likamilike ipasavyo na taarifa zake ziwekwe kwenye tovuti maalum na zitumike kwenye simu za mkononi ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi

 

Naye Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika hilo, Macrice Mbodo amesema kuwa Shirika lake ni mdau muhimu katika anuani za makazi na postikodi ndani na nje ya nchi kwa kuwa posta zote duniani zina jukumu la kutoa anuani zinazotambulika na muundombinu huu utakapokamilika Shirika litatumia anwani za makazi kusafirisha huduma na bidhaa kwa wananchi mpaka nyumbani kwa kuwa tayari tuna duka mtandao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments