TBA YATUMIA SHILINGI MILIONI 515 KUTOKA MAPATO YAO YA NDANI KUKARABATI NYUMBA NA MAJENGO WANAYOYASIMAMIA


Muonekano ya nyumba zilizofanyiwa ukarabati na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA.)
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miliki wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Said Mndeme akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua nyumba na majengo hayo leo jijini Dar es Salaam na kueleza kuridhishwa na ukarabati huo ambao wanufaika wakubwa ni watumishi wa Umma, watu binafsi, Taasisi za Serikali na Wizara mbalimbali, leo jijini Dar es Salaam.


* Yaishukuru Serikali kwa kutoa Bilioni 23 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati


WAKALA Wa Majengo Tanzania (TBA,) imetumia milioni 515 kutoka mapato yao ya ndani kukarabati nyumba na majengo yanayosimamiwa na Wakala hiyo kupitia mpango wao wa uboreshaji na ukarabati wa 'TBA Branding' ambapo hadi sasa nyumba na majengo yote ya Serikali yanayosimamiwa na TBA katika Mkoa wa Dar es Salaam yamefanyiwa ukarabati wa kuzifanya kuwa za kisasa zaidi na kuboresha mifumo ya maji taka, LUKU huku mfumo wa uvunaji na uhifadhi wa maji ukifanyiwa marekebisho kwa kiasi kikubwa.


Hayo yameeleza na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miliki wa Wakala hiyo Said Mndeme mara baada ya kukagua nyumba na majengo hayo leo jijini Dar es Salaam na kueleza kuridhishwa na ukarabati huo ambao wanufaika wakubwa ni watumishi wa Umma, watu binafsi, Taasisi za Serikali na Wizara mbalimbali.


''Mpango wa uboreshaji na ukarabati wa majengo na nyumba zilizo chini ya Wakala 'TBA Branding' unaendelea nchi nzima, majengo na nyumba zote zitafanyiwa ukarabati wa hali ya juu na hiyo ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa nyumba nyingi zaidi ili kuendana na uhitaji, Dar es Salaam hali za nyumba na majengo ni nzuri, Dodoma na Arusha pia ukarabati unaendelea na majengo yote yatakuwa na taswira inayofanana kwa ubora, rangi na nembo ya Wakala.'' Amesema.


Mndeme amesema, hadi sasa milioni 515 ambazo zimetokana na mapato ya ndani ya Wakala hiyo zimetumika kufanya ukarabati huo uliohusisha kuziweka katika hali ya usasa ambayo matumizi yake yanakidhi watumiaji wa madaraja yote.


''Kwa Dar es Salaam hali ni safi, tumeunga mkono jitihada za mkuu wa Mkoa Amos Makalla kupitia kampeni ya 'Pendezesha Dar es Salaam' kwa vitendo nyumba 149 zimekarabatiwa na kwa awamu ya pili ya mpango huu tutagusa nyumba mpya na kuziboresha zaidi ila kwa sasa ni dhahiri kwamba nyumba na majengo hayana muonekano wa uchakavu uliozoeleka.'' Amesema.


Kuhusiana na madeni ambayo Wakala hiyo inadai kwa Taasisi na Wizara, Mndeme amesema kuwa madeni ya kodi pango kwa Taasisi na Wizara yamefikia Bilioni 9.1 na Serikali imekuwa ikitoa ushirikiano kwa kuhakikisha madeni yanalipwa na kupitia Wizara ya fedha na Mipango inaendelea kufanya uhakiki na hatimaye kufanywa malipo.


Kwa upande wake Meneja wa Usimamizi, Idara ya Miliki Fredy Mangula amesema Wakala hiyo ittaendelea kuongeza idadi ya nyumba kutokana na uhitaji mkubwa wa watumishi wa umma na watu binafsi.


''Mkakati wa Idara ya miliki ni kujenga nyumba nyingi zaidi, nyumba zilizopo ni 6845 huku idadi ya watumishi wa Umma ifikifikia kati ya laki tano hadi sita, Dodoma tumeanza kujenga nyumba za makazi katika maeneo ya Nzuguni, pamoja na Dar es Salaam katika maeneo ya Magomeni na Masaki ambapo kasi ya ujenzi wa nyumba za kisasa inaendelea.'' Amesema.


Mangula amesema hadi sasa jumla ya shilingi Bilioni 23 zimepokelewa kutoka kwa Serikali kwa ajili ya ukarabati nyumba za watumishi wa Umma na viongozi pamoja na ujenzi wa makazi mapya katika maeneo mbalimbali nchini ili kwenda sambamba na uhitaji wa nyumba za makazi.


Ziara ya ukaguzi wa majengo na nyumba hizo umefanyika katika maeneo ya maghorofa ya Garden, Posta, majengo ya Baraza la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Anga, maghorofa ya familia, Ada Estate na maghorofa ya familia Mbezi Beach.


Meneja wa Usimamizi, Idara ya Miliki Fredy Mangula akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara hiyo na kueleza kuwa Wakala hiyo ittaendelea kuongeza idadi ya nyumba kutokana na uhitaji mkubwa wa watumishi wa umma na watu binafsi.
Ziara ikiendelea.

Baadhi ya wakazi wa nyumba zinazosimamiwa na TBA wakizungumza na vyombo ya habari na kuishukuru Wakala hiyo kwa matengenezo hayo na kuwashauri kujenga nyumba nyingi zaidi zenye viwango kutokana na uhitaji mkubwa wa makazi kwa wananchi.



Matukio mbalimbali wakati wa ziara hiyo.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments