PUMBULU: MILA YA KISUKUMA INAYOFANYIKA BAADA YA MWANAMKE KUPOTEZA MAISHA AKIJIFUNGUA


Akina mama wa kijiji cha Nyamswa wilayani Bariadi mkoani Simiyu wakishiriki mila ya Pumbulu kutoka kijiji cha Nyamswa kwenda Kijiji jirani cha Mwasubuya hivi karibuni.

Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.


👉Hawataki kuona mwanaume yeyote wakati wakitekeleza mila hiyo.
👉Wanne wakamatwa baada ya kumshambulia mkandarasi wa barabara.


MILA na Desturi zina mchango mkubwa katika jamii endapo zitaenziwa kwa kuheshimu haki zingine za binadamu, hata hivyo wakati mwingine jamii hutumia haki za kitamaduni kama kisingizio cha kukandamiza wengine au kubinya haki zingine za binadamu katika jamii.


Utamaduni pia huainisha jamii, kiasi kwamba mawazo, matarajio na kanuni zao au viwango vya tabia zao (ambazo wao huamua nini ni muhimu katika maisha yao) yote ni sawa sawa wanapokabili mazingira ya ulimwengu unaowazunguka.

Pumbulu ni moja ya tamaduni za kabila la Wasukuma, ambayo hufanyika au hutimizwa baada ya mwanamke kupoteza maisha akijifungua na kwamba baada ya matanga wanawake hutambika kwa kukimbiza Pumbulu.

Kabla na baada ya Uhuru, Mila hii ilikuwa inafanyika sana katika maeneo mengi ya Usukumani, lakini baada ya miaka ya 1990 ilianza kupungua kutokana na jamii nyingi kupata elimu, dini pamoja na uboreshaji wa huduma za afya.

Mara nyingi wakinamama walikuwa wanapoteza maisha kutokana na ukosefu wa huduma za afya kwani walikuwa wanajifungulia majumbani, hali iliyochangia vifo vyao lakini kwa jamii ya wasukuma ilibainika ni mkosi.

Roda Kuyi mkazi wa Kijiji cha Mhunze wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu anasema kuna baadhi ya wanawake wasiomcha mungu bado wanaendeleza mila hiyo ambayo imepitwa na wakati.

Anasema hutokea mara baada ya mama mjamzito kupoteza maisha akijifungua, ambapo baada ya msiba kufanyika, wanawake hao huchukua majivu ya familia hiyo pamoja na kuvunja vyungu (Malujo), Minyaa, Magaka, na takataka zingine kuzihamishia kijiji cha pili.


Anasema huzihamishia kijiji cha pili (Magharibi) kama ishara ya kuondoa mikosi katika kijiji chao na kwamba wakikutana na mwanaume yeyote njiani lazima apigwe na kuvuliwa nguo.


"Vitu hivyo vinasindikizwa hadi katikati ya kijiji cha pili upande wa magharibi, nao wakina mama wa kijiji cha pili huvipeleka kijiji kinachofuata hadi ziwa Viktoria, lengo ni kuondoa mikosi na zoezi hili hutokea mashariki kuelekea Magharibi (yaani ziwani)’’ anasema Roda.

Anafafanua kuwa wakina mama hao (Pumbulu) hupambana na kila mwanaume wanayekutana naye njiani wakiamini kuwa ndiye aliyesababisha mwanamke mwenzao kupoteza maisha wakati wa uzazi.

Anaongeza kuwa waliamini kuwa mwanamke mwenzao kapoteza maisha kutokana na kushiriki tendo la ndoa na wanaume wengi wakati wa ujauzito wake hivyo mwanaume yeyote hastahili kuonekana wakati wa kutimiza mila hiyo.


Naye Julius Renatus mkazi wa kijiji cha Lagangabilili wilaya ya Itilima alisema mila hiyo imefutwa na ujio wa dini pamoja na elimu ambapo kwa sasa familia nyingi haziamini utamaduni huo.

"Elimu na dini zimeondoa mila hii japokuwa kuna baadhi ya watu wameishikilia, tunaamini itaenda inafutika polepole…tunaiomba serikali ipige marufuku mila ambazo zinahatarisha maisha ya watu kwa sababu sasa hivi kuna mwingiliano wa makabila tofauti tofauti’’ anasema Renatus.

Anasema kuwa wao kama wanaume wa jamii ya Kisukuma wanawajua akina mama hao, hivyo wakiwaona lazima wakimbie kujificha ambapo kwa wageni bado kuna changamoto.

Mayenga Gidakindwa mkazi wa Bariadi anasema siyo mila nzuri kwa sababu inakizana na haki za binadamu sababu mtu ana haki ya kuishi na kutembea popote ndani ya Jamhuri ya Muungano bila bughuza yoyote.

Viongozi wa dini wanena.

Padri John Nkinga ambaye ni Paroko wa Kanisa Katoliki Ngulyati wilaya ya Bariadi anasema wao kama viongozi wa dini wanajikita kuelimisha jamii kupitia nyumba za ibada ili wananchi waachane na mila potofu ambazo zimepitwa na wakati.

"Sisi tukiwa viongozi wa Dini kwa jamii yetu tunajikita kuelemisha jamii madhara ya Mila na Faida ya kuiacha! (We put more Community awarreness on the case!!)… Sasa kwa mfano Pumbulu nimewajibika vilivyo kwanza kuwafundisha Pumbulu, Ni Nini na wamejua na kuachana nayo!’’ anasema Padri Nkinga.

Kuhusu kutimiza wajibu wa kutoa elimu, Padri Nkinga anasema "Hatujawajibiki kwa waumini, Elimu haina mwisho na Imani ni sawa na upepo mtu kujiachia kabisa…anahitaji elimu ya malezi, nashukuru kwa matukio haya yanasaidia kusafisha njia kwa Elimu ya Hakika zaidi!’’

Padri Nkinga anasema ujio wa Dini na Elimu umeipunguza jamii kuachana na mila na desturi sababu walikotoka ni kubaya na watu hawatukutambua thamani ya viongozi wa dini.

"Tumetoka mbali, mtu anakufa anawekewa miba na kuachwa porini…matumizi ya nyumba bora, Hospitali na mavazi, uhakika wa vipimo na tiba, Mila potofu inatuambia tumerogwa tu na kusubiria kifo, mbaya zaidi kuna mahali wanaitumia kuku kam darubini!,’’ anasema Padri Nkinga.

Padri huyo anaishauri Serikali isifuate mkumbo na upendeleo wa mila potofu bali wafuate misingi ya kuisaidia jamii, pia wawe na msimamo mmoja au wasiwe wafuasi wa mila mbaya, na wasimamie Sera na kanuni zinakubalika kimataifa na Kikatiba.

DC azungumzia uwepo wa Pumbulu Bariadi.

Akiwasilisha taarifa ya hali ya ulinzi na usalama mbele ya kamati ya siasa mkoa wa Simiyu, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Bariadi Lupaksyo Kapange amesema hivi karibuni akina mama wanne wamekamatwa na polisi kwa kosa la kumshambulia mkandarasi wakati wakitekeleza mila ya Pumbulu.

"Serikali imechukua hatua ya kukamata wote waliohusika kumshambulia mkandarasi huyo anayetekeleza miradi ya barabara kata ya Nkololo, hatuwezi kufanya mila hizi kuwa sheria ya makabila yote’’ ,amesema Kapange.

Kapange ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Bariadi amesema mila hizo ni kinyume na haki za binadamu na kwamba hazitendi haki sababu ujauzito walipeana watu wawili inakuwaje anapigwa mtu yeyote barabarani.

Kapange anasema mila hiyo ni hatari na inanyima uhuru na haki za binadamu na kwamba serikali itawasaka wale wote wanaopiga watu barabarani wakati wa kutekeleza mila ya Pumbulu kwa jamii ya wasukuma.

Polisi wakamata wanawake wanne kwa kumshambulia mkandarasi.

Jeshi la polisi Mkoani Simiyu linawashikilia wanawake wanne kwa tuhuma za kumshambulia Mkandarasi wa barabara ya Nkololo-Bariadi wakati wakitekeleza mila yao ya kukimbiza Pumbulu.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu Kamishna Msaidizi wa Polisi Blasius Chatanda akiwa ofisini kwake aliwaambia Waandishi wa habari kuwa wanawashikilia wanawake wanne kwa kushambulia mkandarasi huyo na kumsababishia majeraha.

"Ni kwamba mnamo tarehe 09/12/2021 majira ya 11:00 asubuhi, huko maeneo ya kijiji cha Nkololo, Kata na Tarafa ya Nkololo Wilaya ya Bariadi, alishambuliwa Mkandarasi na kundi la Wanawake kwa kumpiga mawe sehemu mbali mbali za mwili wake na kumsababishia majeraha’’ alisema Kamanda Chatanda.

Alisema kundi hilo la Wanawake walikuwa katika kutimiza mila zao za Kisukuma, ambapo Mwanamke akijifungua na ikatokea yeye na mtoto wake wamefariki huwa wanaenda kufanya tambiko hivyo wakiwa njiani wakikutana na mwanaume yoyote wanaanza kumshambulia hii ni kutokana na mila zao za Kisukuma inayotambulika kwa jina la “Pumbulu”.

Alifafanua kuwa hadi sasa watuhumiwa hao wapo nje kwa dhamana na mara baada ya upelelezi kukamilika jalada litaandaliwa kwenda Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na kufikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Kamanda Chatanda anawataka wananchi na wanawake wote kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, huku akionya kuwa mila hizo isiwe chanzo cha kujichukulia sheria mkononi.
Akina mama wa kijiji cha Nyamswa wilayani Bariadi mkoani Simiyu wakishiriki mila ya Pumbulu kutoka kijiji cha Nyamswa kwenda Kijiji jirani cha Mwasubuya hivi karibuni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments