MAKALA :UKOSEFU WA JENGO,VIFAA VYA KISASA CHANZO CHA UZALISHAJI WA VIFARANGA WA SAMAKI WASIO NA UBORA


Na Dinna Maningo, RORYA

UZALISHAJI wa samaki wanaofugwa kwenye mabwawa kwa njia za kizamani umekuwa na changamoto, hali inayosababisha vifaranga kuzaliwa kwa idadi ndogo na wasio na ubora kutokana na ufugaji usiokuwa na mfumo wenye vyombo maalumu vya Teknolojia ya kisasa vya kufuga na kutotoresha vifaranga. 

Malunde 1 blog imefunga safari hadi Taasisi ya Utafiti wa uvuvi (TAFIRI) kituo cha Sota kilichopo kijiji cha Sota kata ya Tai wilaya ya Rorya mkoani Mara,ambayo ipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuzungumza na watafiti wa uvuvi, wafugaji wa samaki aina ya Sato wanaofugwa kwa kutumia mabwawa na vizimba ndani ya ziwa Victoria.

Tausi Khitentya ni Afisa mfawidhi kituo cha utafiti wa uvuvi Sota wilayani humo anaeleza kuwa ufugaji wa kisasa wa kutumia mabwawa na vizimba ni mzuri  endapo changamoto zake zikitatuliwa na na utaleta tija na kipato kikubwa kwa wafugaji lakini pia kuzitatua changamoto za watafiti wa uvuvi ikiwemo kupatiwa vifaa vya kiteknolojia vya kufanyia utafiti.

Khitentya anasema kuwa 1988 kituo hicho cha utafiti wa uvuvi kilianzishwa wilayani humo na kwamba lengo ni kuhamasisha ufugaji wa samaki,kufanya tafiti na ushauri,kupata taarifa za kitafiti na kuziwasilisha ili kutoa muongozo katika tafiti za uvuvi nchini.

Khitentya anasema kuwa kituo kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za ukosefu wa vitendea kazi vya kufanyia kazi za utafiti,jengo na Vifaa vya kisasa vya kutotoresha vifaranga wa samaki,upungufu wa watumishi 13 ,nyumba za watumishi na upungufu wa boti.

"Baada ya kuhamia Sota tulifanya kazi kwenye mazingira magumu tulikuwa na upungufu wa ofisi,maabara kwa ajili ya shughuli za utafiti,umeme, changamoto hizi zilipelekea 2001 kuhamia mitaani kule Kabwana-Shirati hadi 2020 tukapanga ofisi zenye umeme ili kufanya shughuli za Serikali.

" Tuliomba fedha Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kutujengea majengo ya ofisi,maabara na nyumba za watumishi, wametujengea jengo la utawala na jengo la maabara ya utafiti ujenzi ulioanza 2016 unaojengwa na Suma JKTumekamilika 2020 tunasubiri tukabidhiwe japo tangu mwaka jana tunayatumia majengo hayo maana tuliona tusiendelee kuingia gharama za fedha kulipa kodi kwenye ofisi za kupanga",alisema Khitentya.

Anasema kuwa kuna maabara ya utafiti lakini haina vitendea kazi " COSTECH wametujengea jengo la utawala na maabara lakini halina vifaa vya maabara vya kisasa kwa ajili ya utafiti,vifaa vya kukusanya takwimu za kitafiti tunapokwenda fildi,vifaa  vya kukusanya sampuli za maji,na vyakufanyia uchambuzi wa sampuli za maabara.

"Tuna boti moja ya kubeba watu 10 haiwezi kwenda maji marefu,hatua vifaa vingine vya kielektlonic,vifaranga vinavyozaliwa vina ubora kidogo kutokana na mabwawa yasiyo na viwango vya kisasa" anasema.

Hali ya uzalishaji wa samaki.

Khitentya anasema kuwa wanatumia njia ya kawaida ya kuzalisha vifaranga ambayo ni ya kuweka neti ndani ya bwawa lenye maji nakuweka samaki wazazi wanaachwa,wanataga na kutotoa kisha vifaranga vinachukuliwa .

  "Kituo chetu ni cha utafiti hatuna jengo,teknolojia ya kisasa inahitaji jengo maalumu la kutotoresha ambalo ndani yake litakuwa na mfumo wa kisasa wenye vyombo maalumu vya kisasa vya kutotoresha,Hapa zetu tumeweka wazazi 16 wastani kwa mwezi ni vifaranga 24,000,samaki anakua kwa wiki sita hadi nane ndipo anatotoa vifaranga.

"Teknolojia ya sasa samaki akitaga yai ananyang'anywa anaendelea kutaga alafu mayai yanatotoreshwa kwa njia za kisasa wanapelekwa kwenye jengo ambalo lina vifaa maalumu vya utotoreshaji",anasema.

Anasema kuwa wanafuga samaki kwa kutumia njia ya kawaida ya mabwawa, yalikuwa 9 lakini yanayotumika ni matatu kwasababu yakupotea kwa maji na miundombinu ya maji,hakuna pampu ya kusukuma maji.

Anaeleza kuwa kituo hicho cha utafiti hutoa mafunzo ya ufugaji wa kisasa kwa kutumia mabwawa na vizimba ambayo ni endelevu ambapo hukusanya wadau, vikundi vya ufugaji na kupatiwa elimu.

"Tuna wadau mbalimbali akiwemo Dkt. Masuba,kikundi cha MICHEEO,TAFG Tarime,mwaka jana tumetoa mafunzo kwa wageni mmoja mmoja wapatao 39 ambao tunawapa mafunzo na kuondoka na tunawatembelea kwenye mashamba yao.

"Tuliseminisha kikundi cha ufugaji samaki cha MICHEEO chenye wanachama 30 wanawake wakiwa 22 na wanaume 8 pamoja na wana kikundi wanne wa TAFG kutoka maeneo ya Rorya, Tarime na Serengeti.

Mwandishi aliongozana na Cesilia Mataba ambae ni afisa mtafiti na mkuu wa kitengo cha  cha utafiti (TAFIRI) Sota kutembelea ufugaji wa samaki wa mabwawa.

Malunde 1 blog ikatembelea ufugaji wasamaki kwa kutumia vizimba vilivyopo ndani ya ziwa Victoria kwa kikundi cha MCHEEO NA TAFG mwendo wa mita 240,kutoka nchi kavu kwa kutumia usafiri wa mtumbwi wa kupiga kasia mwendo wa dk5,ambapo ukitumia mtumbwi wa injini ni dk1 kufika eneo kunapofugwa samaki kwa njia ya vizimba.

Mataba anasema ufugaji wakwenye  vizimba uzalishaji wake ni mkubwa"ufugaji wa samaki umesaidia sana kupunguza ile kasi kubwa ya wavuvi kuvua samaki ziwani tukisema tutegemee kuwavua bila ufugaji samaki watazodo kupungua ziwani.

"Ufugaji umesaidia watu kupata ajira,samaki wa vizimba ni wakubwa kwasababu wanakuwa kwenye Mazingira yao ya asili ya maji tofauti na wa mabwawa ambayo maji yake yanakuwa hayana ubaridi baada ya kupigwa jua,changamoto ni wadudu wala samaki na ugonjwa wa fangasi huu unapunguza uzalishaji.

Daud Malunga mkazi wa Sota ambaye ni msaidizi wa ufugaji wa samaki (TAFG) kwa kutumia vizimba ambae pia ni mtaalamu wa mtumbwi wa kupiga gasia,anayehudumia samaki chakula anasema;

"Huwa natumia mtumbwi wa kupiga kasia nawapelekea chakula samaki waliopo ziwani kwenye vizimba,samaki wakubwa ni gramu 90-100 hao wana kula chakula mara tatu kwa siku.

" Wale wadogo wanakula mara nne hadi tano kwa siku,ulishaji wake unategemea hali ya hewa,wakati wa mvua hawali sana kwa sababu ya ubaridi wa maji,nimefanya kazi ya ubaharia miaka 10 kwenye boti ya kasia ni mzoefu", anasema Malunga.

Mtaalamu wa ufugaji wa samaki kutoka kikundi cha TAFG Tarime Janeth Nyamnata anasema "kikundi chetu kipo Tarime ila tunafuga samaki kwenye vizimba ziwani Rorya kwakuwa Tarime hakuna ziwa,mradi umeanzishwa mwaka jana ambapo mwezi januari mwaka huu tuliweka vifaranga kwenye vizimba, tunatarajia kuvuna hivi karibuni.

"Tuna vizimba 22 vilivyo na saizi ya 5 kwa 5 urefu kina cha maji mita 6, awali chakula tulikuwa tunanunua cha Thailand ila kwa sasa tuna mashine yetu Tarime inayotengeneza chakula cha samaki" anasema Nyamnata.

Katibu wa kikundi cha Micheeo Bonjo Ojora mkazi wa kijiji cha Sota anasema kuwa wanapovuna samaki kilo moja uuzwa sh.5,500,alizitaja changamoto za ufugaji wa samaki ni pamoja na ukosefu wa  fedha ili kukidhi  mahitaji ya uendeshaji wa shughuli za ufugaji samaki na vifo vitokanavyo na fangasi.
Cesilia  Mataba Mkuu wa kitengo cha utafiti wa uvuvi (TAFIRI) Sota na Daud Malunga msaidizi wa ufugaji wa samaki kikundi cha TAFG wakilisha chakula samaki kwenye vizimba vya kikundi cha TAFG.
Cesilia  Mataba Mkuu wa kitengo cha utafiti wa uvuvi (TAFIRI) Sota akionyesha bwawa la samaki.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments