SERIKALI YA ZANZIBAR YAAPA KUULINDA MUUNGANO

 Na mwandishi wetu, Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kuulinda Muungano kwa kuwa ndio tunu kubwa ambayo imeachwa na waasisi wa Muungano huo na kwamba Serikali haitotumia nguvu kwa baadhi ya wananchi wenye maoni taofauti bali itawaelimisha.



Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla wakati alipokuwa akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulioongozwa na Waziri wa Wizara hiyo Balozi Liberata Mulamula (Mb) na kuongeza kuwa Zanzibar inatambua umuhimu wa Muungano uliopo pamoja na manufaa yake huku akitolea mfano kwa baadhi ya Wazanzibar wanaoishi Bara ambao ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameongeza kuwa kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika masuala ya kuimarisha uchumi na kuwaletea Wazanzibar maendeleo kutokana na umoja, amani na mshikamano uliopo tangu uwepo wa muafaka wa Serikali ya Kitaifa na kuwataka wafanyabiashara na wawekezaji kujitokeza kuwekeza visiwani humo katika sekta mbalimbali ikiwemo eneo la Uchumi wa Buluu.

BONYEZA HAPA KUJUA VITUO VITAKAVYOTOA CHANJO YA CORONA TANZANIA


Akizungumza wakati wa kujitambulisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano uliopo katika utendaji kazi na kwamba kwa sasa Wizara inaendelea na maandalizi ili kuwawezesha Viongozi wakuu wa pande zote mbili kushiriki kikamilifu katika mikutano ya Kimataifa.

Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ukiongozwa na Balozi Liberata Mulamula ambaye ameambatana na Naibu Waziri Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine pamoja na Naibu Katibu Mkuu Balozi Fatma Mohammed Rajab na baadhi ya Wakurugenzi wa Wizara hiyo uko visiwani Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha kwa viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments