NAIBU WAZIRI KASEKENYA ATOA SIKU 10 MIZANI YA NYAKAHURA, KAGERA KUKAMILIKA

 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, akiongea na wakazi wa kata ya Rulenge Wilayani Ngara, aliposimama kuzungumza nao wakati akikagua barabara ya Omubuga, Rulenge hadi Murugarama (KM 32), iliyotengewa fedha na Serikali kwa ajili ya kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mbunge wa Jimbo la Ngara Ndaisaba Ruhoro (mwenye suti ya bluu), akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya (kushoto), wakati akikagua barabara ya Omubuga, Rulenge hadi Murugarama (KM 32), iliyotengewa fedha na Serikali kwa ajili ya kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami. Kushoto kwa mbunge huyo ni Mkuu wa Wilaya ya Ngara Col. Mathias Kahabi.

Ukarabati wa miundombinu ya mizani ya Nyakahura iliyoko wilaya ya Ngara mkoani Kagera, ukiendelea kwa kasi. Mizani hiyo inatumika kupima magari makubwa ya mizigo zaidi ya 400 kwa siku, yanayofanya safari zake kati ya Tanzania, Burundi na Rwanda.

Ujenzi wa daraja la kudumu la Kitengule lenye urefu wa meta 140 ukiendelea. Kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutaziunganisha wilaya za Karagwe na Misenyi Mkoani Kagera

Meneja wa Wakala wa barabara (TANROADS) mkoa wa Kagera Mhandisi Ntuli Mwaikokesa, akimkumbusha jambo Mhandisi Mkazi Charles Romisha, wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa daraja la Kitengule na barabara unganishi (KM18). Wa kwanza kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani), wakati akikagua ujenzi wa daraja la Kitengule lenye urefu wa meta 140, na barabara unganishi (KM18), kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Col. Sakulo akifuatiwa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.

PICHA NA WUU

.......

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ametoa siku 10 kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Kagera, kuhakikisha anamsimamia mkandarasi anayejenga mizani ya Nyakahura mkoani humo, kumaliza ujenzi na kuanza kutolewa huduma za upimaji wa magari katika mizani hiyo kama zamani.

Akizungumza katika ziara yake ya kukagua miradi ya barabara, mizani na madaraja mkoani humo, Naibu Waziri Kasekenya, amesema kuwa kusimama kwa huduma za upimaji wa magari katika mizani hiyo kunaisabibishia Serikali hasara kubwa, kwani kupitia fursa hiyo magari yanaweza kuzidisha uzito na kupelekea kuharibu barabara.

“Ujenzi wa mizani hii inabidi ukamilike mapema iwezekanavyo, nimeambiwa hapa kwa siku yanaweza kupita magari zaidi ya 500, hivyo magari kutokupima hapa inaweza ikawa sababu ya wasafirishaji kuzidisha uzito na kupelekea kuharibu barabara zetu ambapo Serikali inatumia kiasi kikubwa cha fedha ili kuzijenga”, amesema Kasekenya.

Aidha, amemuagiza Meneja huyo kufanya utaratibu wa kuandaa mchoro wa mizani nyingine ya pili, pembezoni mwa mizani ya kwanza ili kuepusha msongamano amabao unaweza kujitokeza.

“Haiwezekani sehemu inayopitisha magari mengi kama hii ikawa na mizani moja ya kupima magari yanayotoka na yanayoingia nchini, hivyo nakuagiza tena Meneja kuandaa mchoro na kuuwasilisha Wizarani ili tutenge fedha kwa ajili ya mizani ya pili”, amesisitiza Kasekenya.

Kuhusu suala la barabara katika mkoa huo, Kasekenya amesema kuwa Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 12.8 kwa ajili ya ukarabati mdogo wa barabara ya Lusahunga – Rusumo (Km 92), huku ikisubiri taratibu za manunuzi ya kumpata mkandarasi wa kufanya ukarabati mkubwa.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya, amekagua daraja la Kitengule lenye urefu wa mita 140 na barabara za maingilio zenye urefu wa kilometa 18 ambapo ameridhishwa na kasi ya ujenzi ya mradi huo unaojengwa na mkandarasi M/s China Henan.

Amebainisha kuwa daraja hilo ambalo linaunganisha wilaya ya Karagwe na Misenyi, litakuwa ni njia ya mkato kati ya wilaya hizo mbili na hivyo kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa wilaya hizo na mwekezaji wa kiwanda cha sukari kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Ngara, Mheshimiwa Ndaisaba Ruhoro, ameipongeza Serikali kwa kutoa shilingi Bilioni 6 kwa ajili ya maandalizi ya kuanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami za Nyakahura – Kumubuga – Murusugamba (Km 75), Kumubuga – Rulenge – Mururama (Km 32) na Rulenge - Kabanga Nickel (Km 34) ambapo amesema kuwa kukamilika kwa barabara hizo kutarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kutoka wilaya hiyo kuelekea wilaya jirani na hata nchi jirani za Rwanda na Burundi.

Naye, Msimamizi wa Daraja la Kitengule, Charles Rumisha, amesema kuwa mradi ulianza mwezi Oktoba, 2018 na kutarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu ambapo amesisitiza kuwa mpaka sasa wamefika katika hatua nzuri.

Amefafanua kuwa kwenye upande wa barabara ujenzi umefika asilimia 88 na kwa upande wa daraja mkandarasi tayari keshakamilisha ujenzi wa nguzo zote nne, kilichobaki ni kuweka usawa wa juu wa barabara.

Naibu Waziri Kasekenya, yupo katika ziara ya siku Tatu mkoani Kagera ambapo atakagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na na Wizara hiyo ili kujionea maendeleo yake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments