MAADHIMISHO YA WIKI YA MAZIWA YAANZA NA WENYE MAHITAJI MAALUM

 

Mwanafunzi mwenye ulemavu (kushoto) wa Shule ya Msingi Nguvumali akiwa anafurahia maziwa huku akimwangalia mwanafunzi mwenzake mara baada ya kupatiwa maziwa kutoka Bodi ya Maziwa nchini (TDB) ikiwa ni siku ya kwanza ya maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa kitaifa yanayofanyika Mkoani Tanga. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nguvumali Samira Shaban akipatiwa maziwa na mwalimu wake, mara baada ya maafisa kutoka Bodi ya Maziwa nchini (TDB) na Mkoa Tanga, kufika katika shule hiyo kwa lengo la kuhamasisha unywaji maziwa kwa watoto ili kuimarisha afya zao ikiwa ni moja ya shughuli ambazo bodi hiyo itakuwa inafanya katika maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa kitaifa yanayofanyika Mkoani Tanga kwa kuyafikia makundi ya watu wenye mahitaji maalum. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Mmoja wa walimu wa lugha ya alama katika Shule ya Msingi Chuda, akitoa tafsiri kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kutosikia mara baada ya maafisa kutoka Bodi ya Maziwa nchini (TDB) na Mkoa wa Tanga kufika katika shule hiyo, kwa lengo la kuhamasisha unywaji maziwa kwa watoto ili kuimarisha afya zao ikiwa ni moja ya shughuli ambazo bodi hiyo itakuwa inafanya katika maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa kitaifa yanayofanyika Mkoani Tanga kwa kuyafikia makundi ya watu wenye mahitaji maalum. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).
Kaimu Afisa Lishe Mkoa wa Tanga Bi. Sakina Mustapha, akiwafahamisha wanafunzi wa Shule ya Msingi Nguvumali umuhimu wa unywaji maziwa, mara baada ya Bodi ya Maziwa nchini (TDB) kugawa maziwa kwa wanafunzi wakiwemo wenye mahitaji maalum katika shule za msingi Usagara, Chuda na Nguvumali katika siku ya kwanza ya maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa kitaifa yanayofanyika Mkoani Tanga kuanzia Tarehe 31 Mei hadi 04 Juni 2021. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).
Afisa Msindikaji wa Maziwa kutoka Bodi ya Maziwa nchini (TDB) Bw. Dotto Nkuba, akizungumza mara baada ya kuhitimisha zoezi la ugawaji maziwa kwa shule za msingi Usagara, Chuda na Nguvumali katika siku ya kwanza ya maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa kitaifa yanayofanyika Mkoani Tanga na kufafanua kuwa bodi hiyo itaendelea kuyafikia makundi mbalimbali ya watu wenye mahitaji maalum katika kuhamasisha unywaji maziwa ili kuimarisha afya ya mwili. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Picha ya pamoja ya maafisa kutoka Bodi ya Maziwa nchini (TDB), Mkoa wa Tanga na baadhi ya walimu na wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Usagara baada ya wanafunzi hao kupatiwa maziwa na bodi hiyo katika siku ya kwanza ya maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa kitaifa yanayofanyika Mkoani Tanga. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).



Na. Edward Kondela

Bodi ya Maziwa nchini (TDB) imesema katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora imeamua kugawa maziwa kwa watu wenye mahitaji maalum kutokana na virutubisho vilivyopo kwenye maziwa hayo ambavyo vitawasaidia kuimarisha afya zao.

Akizungumza leo (31.05.2021) mara baada ya kuhitimisha siku ya kwanza ya ugawaji maziwa ikiwa ni sehemu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na TDB katika maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa kitaifa yanayofanyika Mkoani Tanga, kuanzia tarehe 31 Mei hadi 04 Juni Mwaka 2021, Afisa Msindikaji wa Maziwa kutoka bodi hiyo Bw. Dotto Nkuba amesema katika siku ya kwanza bodi imetembelea shule tatu za msingi za Mkoa wa Tanga ambazo pia zinawahudumia watoto wenye mahitaji maalum ili kutoa kipaumbele kwa watoto hao kunywa maziwa na kuhamasisha jamii kuwa na utaratibu kwa kunywa maziwa ili kuimarisha afya zao.

“Lengo la kutoa maziwa kwa watu wenye mahitaji maalum tunahimiza kunywa maziwa kutokana na virutubisho vitokanavyo katika maziwa na tumeangalia watoto wa shule kwa siku ya leo na hii haimaanishi watu wengine wasinywe maziwa bali wanywe kwa faida ya afya zao ila hatua hii itakuwa mwendelezo wa kuyafikia makundi mengine.” Amesema Bw. Nkuba

Ameongeza kuwa maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa kitaifa yanayofanyika Mkoani Tanga, yanalenga kuhamasisha wananchi kunywa maziwa kwa sababu ni chakula ambacho kina virutubisho vyote ambavyo ni muhimu kwa mwili wa binadamu hususan maziwa yaliyosindikwa ambayo yamekidhi ubora.

Aidha, amesema Bodi ya Maziwa nchini inahimiza wananchi kunywa maziwa kwa wingi ili kuwa na utamaduni wa kunywa maziwa na kuviwezesha viwanda vya kuchakata maziwa nchini kuuza bidhaa zao kwa wingi.

 

Kwa upande wake Kaimu Afisa Lishe Mkoa wa Tanga Bi. Sakina Mustapha, amesema wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kutoa elimu juu ya umuhimu wa unywaji maziwa kutokana na maziwa kuwa na madini na vitamini pamoja na maji ambavyo vyote hivyo vinajenga mwili, kulinda mwili, kuongeza ufanisi wa kujenga mifupa sambamba na meno, kupata sukari na nguvu mwilini pamoja na nguvu ya ziada ya kufanya kazi.

Bi. Mustapha amewaasa wananachi kwa ujumla kunywa maziwa walau kikombe kimoja kila siku ili kuuwezesha mwili kuongeza virutubisho muhimu vitokanavyo na maziwa.

Wanafunzi waliopatiwa maziwa leo na Bodi ya Maziwa nchini ni kutoka katika Shule za Msingi Chuda, Nguvumali na Usagara zilizopo jijini Tanga na zoezi la ugawaji litaendelea kwa kuyafikia makundi mbalimbali ya watu maalum.

Maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa kitaifa yanafanyika Mkoani Tanga kuanzia Tarehe 31 Mei hadi 04 Juni Mwaka 2021, katika viwanja vya Tangamano yakiwa yamebeba kauli mbiu “Kunywa Maziwa ya Kwetu, Ongeza Uzalishaji na Usindikaji, Kazi Iendelee.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments