TARI: WAKULIMA ZINGATIENI MATUMIZI YA MBEGU BORA ZA KOROSHO

 

Mratibu wa zao la Korosho nchini kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele, Dkt. Geradina Mzena akiwaeleza Maafisa Ugani na Wakulima wa Halmashauri mbalimbali za jiji la Dodoma jana namna bora ya kuzalisha kwa tija zao hilo.

Maafisa Ugani na Wakulima wakifuatilia mafunzo hayo.

Dkt. Mzena (aliyekaa wa kwanza kushoto) akiangalia korosho karanga na bibo lenye ubora lililovunwa kwa mara ya kwanza juzi na mkulima kutoka Bahi Salum Mjungu (aliyevaa miwani). Kushoto aliyesimama ni Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Bahi, Abia Silungwe.
Mtafiti Mwandamizi kutoka Tari Naliendele, Dkt. Wilson Nene akiwafundisha maafisa ugani na washiriki namna ya kutambua aina za magonjwa na wadudu waharibifu wa zao la korosho kupitia moja ya mkorosho ambao umeathiriwa vibaya na ugonjwa wa ‘Die Back’.
Mkulima wa Korosho kutoka Chamwino, Nyembera Moses akizungumza kwenye mafunzo hayo ya Kilimo Bora cha Korosho.

Mmoja wa wakulima akizungumza kwenye mafunzo hayo.

Meneja wa Bodi ya Korosho Kanda ya Kati na Magharibi, Ray Mtangi akifafanua majukumu ya bodi katika kuinua tija ya zao la korosho. 

Kaimu Afisa Kilimo Halmashauri ya Bahi, Hamis Mfuko akishiriki mafunzo hayo.

Afisa Ushirika Halmashauri ya Chamwino jijini Dodoma, Octavian Bidyanguze akizungumza kwenye mafunzo hayo yanayoendelea kutolewa na TARI Naliendele kwenye mikoa 17 nchini inayolima zao la Korosho.


Na Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Chamwino

WAKULIMA wa zao la Korosho wamehimizwa kuendelea kutumia aina 54 za mbegu bora za zao la korosho zinazozalishwa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tari Naliendele, ambazo zimethibitishwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha mavuno yake kwa wingi, sambamba na kuvumilia magonjwa na visumbufu vya wadudu hatarishi wa zao hilo.

Pia imeelezwa kuwa matokeo ya mbegu hizo hata baada ya mavuno hususani kwenye eneo la usindikaji mpaka sasa zimeendelea kutoa matokeo chanya kwenye uzalishaji wa bidhaa zake katika Nyanja ya usindikaji hususani kupitia ‘bibo’ lake kwa kuonyesha ufanisi wa hali ya juu kwa matumizi ya utengenezaji juice, ‘ethanol’ na mvinyo.

Akizungumza na vyombo vya habari, muda mfupi baada ya kutoa mafunzo ya Kilimo Bora cha Korosho kwa Maafisa Ugani na Wakulima kwenye wilaya za Mpwapwa na Chamwino jana, Mratibu wa zao la Korosho nchini  kutoka Tari Naliendele, Dk Geradina Mzena alisema endapo mkulima atatumia walau aina zaidi ya 27 ya mbegu hizo basi atakuwa amejihakikishia usalama na uhakika wa mavuno.

Akifafanua, alisema aina hizo 54 ndani yake zimegawanyika katika makundi 3, yaani kuna mbegu 16 ambazo ni za kawaida (kwa maana ya zisizo chotara), pia kuna mbegu 22 ambazo ni chotara, na nyingine 16 ni aina ya mbegu fupi.

Alisema kituo hicho kinatoa mchanganyiko wa makundi ya mbegu hizo zilizofanyiwa utafiti wa kina lengo likiwa ni kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa mkulima, ikiwemo kulikinga zao hilo dhidi ya mashambulizi ya wadudu na magonjwa, sambamba na kumsaidia mkulima kukabili changamoto za kupoteza miche  na kujikuta akipata hasara endapo atapanda aina moja ya mbegu katika shamba moja.

“Aina zote hizi kwenye makundi haya matatu ni mbegu bora. Ubora wa mbegu hizi kwanza zina uwezo wa kutoa korosho kubwa, lakini pia zinavumilia magonjwa na zinaota na kuzaa vizuri sana kwenye maeneo yote ndani ya mikoa 17 tuliyoifanyia utafiti,” alisema Mzena.

Alisema mbegu hizo zina uwezo mkubwa wa kuvumilia wadudu waharibifu, na zaidi hata inapojitokeza hali ya mabadiliko ya hali ya hewa zinaendelea kuwa imara na kutoa mavuno yaliyo bora ikilinganishwa na zile za kienyeji.

Zaidi Mzena alisema kupitia aina hizo za mbegu zitamwezesha mkulima kuvuna korosho karanga zenye punje kubwa, ambazo idadi yake inaweza kuwa chini ya 200 kwa kilo moja na hivyo kuleta tija kwa ustawi wa uchumi wa mkulima na taifa kwa ujumla.

Akizungumza kuhusiana na bibo bora linalotokana na aina hizo za mbegu, Mratibu huyo, ambaye pia ni Mtafiti na Mratibu wa Ubunifu kutoka Tari Naliendele alisema kituo hicho baada ya kubaini kuwa bibo linaweza kukaa kwa kati ya masaa 12 hadi 24 kabla ya kuharibika waliamua kuja na teknolojia ya kulikausha na kisha kulitumia kutengeneza aina hizo za vinywaji na bidhaa za vimiminika.

“Kuanzia msimu ujao tunategemea wakulima watakuwa na misimu miwili ya kuuza korosho zao, kwanza watapata fursa ya kuuza korosho karanga, na msimu mwingine watauza bibo la korosho karanga lililokaushwa na hivyo kuzidi kuongeza thamani ya zao hilo,” alisema Mzena.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments