MGUMBA:TANZANIA INA UTOSHELEVU WA CHAKULA KWA ZAIDI YA ASILIMIA 119

Na Amiri Kilagalila,Njombe

Naibu waziri wa kilimo nchini Omary Mgumba amesema,Tanzania bado ina hali nzuri ya uwepo wa chakula kwa kuwa mpaka leo taifa lina utoshelevu wa chakula kwa zaidi ya asilimia 119.

Mgumba ametoa taarifa hiyo mkoani Njombe wakati wa kongamano la vijana katika kilimo mwaka 2020 lililowakutanisha takribani vijana 200 wa mikoa ya Njombe,Iringa na Ruvuma kwa lengo la kuwahamasisha vijana kujishughulisha na kilimo chenye tija nchini.

"Leo hii mpaka sasa kama taifa naomba niwaambie watanzania na vijana mlioko hapa tuna utoshelevu wa chakula zaidi ya asilimia mia moja na kumi na tisa"alisema Mgumba

Naibu waziri Mgumba amewaeleza vijana na watanzania kuwa kilimo kimeendelea kukuwa na kutoa mchango kwa uchumi wa nchi katika maeneo mbali mbali kwa kuwa takwimu zilizopo za mwaka 2018 zinaonyesha sekta ya kilimo inachangia asilimia 28.2 ya pato la taifa na sekta ndogo ya kilimo mazao inachangia zaidi ya asilimia 16.2 huku watanzania wanaoshiriki katika sekta ya kilimo wakiwa zaidi ya asilimia 58 na kusababisha kilimo kuwa na mchango mkubwa katika ajira.

Mgumba amesema wizara ya kilimo imeendelea kupata mafanikio makubwa kisera na taasisi ikiwemo kuanzisha mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja,na kusababisha ongezeko kutoka tani laki tatu na mbili mpaka kufikia tani laki nne na stini kwa mwaka.

Vile vile ametoa wito kwa vjana kujihusisha katika kilimo kwa kuwa nchi ya Tanzania ina eneo kubwa linalofaa kwa ajili ya kilimo.

"Nchi yetu ina eneo linalofaa kwa kilimo,ambalo linakadiliwa kuwa zaidi ya hekta milioni 44 linafaa kwa kilimo na mifugo hiyo ni fursa vijana mnatakiwa kuitumia,na kati ya hizo hekta milioni 29.4 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji"alisema Waziri Mgumba

Aidha amezitaka halmashauri zote nchini kusimamia kikamilifu mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake vijana na walemavu,pamoja na kutoa mikopo ya kueleweka kwa vijana ili waweze kuwekeza kikamilifu katika kilimo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم