MFUNGWA AJIUA KWA KUJICHINJA NA WEMBE GEREZANI

 Agustino Moshi (70), mfungwa aliyekuwa anatumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa ubakaji, amejiua kwa kujikata mshipa wa fahamu kwa kutumia wembe akiwa ndani ya Gereza la Karanga mkoani Kilimanjaro.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Jumatatu ya Juni 25 ndani ya gereza hilo na kushuhudiwa na mkuu wa gereza hilo, Kamishina Msaidizi wa Magereza (ACP), Leonard Moshy.

Habari ambazo zimethibitishwa pia na ACP Moshy zinasema mfungwa huyo mwenye namba 648/2015 alijikata na wembe kwenye mshipa wa fahamu shingoni mara tatu.

“Huyo mzee alitokea gereza la Maweni Tanga akaletwa kwa rufaa kwa ajili ya kutibiwa KCMC sasa siku hiyo walizozana na ACP Moshy na ndio akaamua kujiua mbele yake,” kilidokeza chanzo chetu cha habari.

Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, siku hiyo saa 8 mchana, mkuu wa gereza alifika ndani ya gereza kwa lengo la kuwapangia wafungwa kazi ya kwenda shambani, lakini mzee huyo akadai anaumwa.

“Huyo mzee alimwambia bwana jela (ACP Moshy) kuwa ana ED (kibali cha daktari cha kupumzika) lakini bwana jela akakataa na ndipo huyo mzee akasema basi ngoja afe tu,” alidokeza mtoa taarifa.

“Hapohapo akatoa kiwembe akaanza kujikata shingoni kwenye mshipa wa fahamu. Yaani anaushika anajikata damu zinatiririka. Kama mara tatu. Lilikuwa ni tukio la ghafla ambalo kila mtu hakulitarajia”.

Baadaye askari magereza walifanikiwa kumkimbiza katika zahanati ya gereza kwa ajili ya matibabu ya kuokoa maisha yake, lakini hata hivyo kutokana na majeraha hayo alifariki dunia.

Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Gabriel Chisseo alilithibitishia Mwananchi jana juu ya kupokelewa kwa mwili huo na kwamba hadi jana, bado ulikuwa umehifadhiwa hospitalini hapo.

Na Daniel Mjema, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527