Breaking : TUNDU LISSU AVULIWA UBUNGE TANZANIA


Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameliambia Bunge hilo leo Ijumaa Juni 28, 2019 kuwa amewandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kumjulisha kuwa kiti cha ubunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lisu kipo wazi.

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Mh. Tundu Lissu, amevuliwa rasmi kiti hicho, baada ya kuvunja taratibu mablimbali za Bunge ikiwemo kutohudhuria Mikutano na vikao vya bunge bila kutoa taarifa.

Akiongea leo Juni 28, 2019 bungeni, wakati wa kuhitimisha mkutano wa kumi na tano, kikao cha hamsini na tano kilichoambatana na hoja ya kuahirisha bunge, Spika amesema, amemjulisha Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kujaza nafasi hiyo.

''Napenda kuwafahamisha waheshimiwa wabunge kuwa kiti cha ubunge cha jimbo la Singida Mashariki kilichokuwa kinashikiliwa na Mh. Tundu Lissu kipo wazi na nimemjulisha Mwewnyekiti wa Tume ya Uchaguzi aendelee na taratibu za kukijaza'', amesema.

Ndugai amefafanua kuwa kutokana na Tundu Lissu, kushindwa kutoa taarifa kwa spika kwa muda wote ambao hayupo bungeni, pamoja na kutowasilisha tamko la mali zake anakuwa amevunja sheria ya uchaguzi.

''Kifungu cha 37, kifungu kidogo cha 3 cha sheria ya taifa ya uchaguzi sura ya 343, kinanitaka kumtaarifu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nini cha kufanya''.

Aidha spika ameongeza kuwa ni zaidi ya mwaka mmoja umepita, ambapo Tundu Lissu amekuwa akionekana kwenye vyombo mbalimbali vya habari katika nchi tofauti, huku akiwa hajafika bungeni wala kutoa taarifa yoyote kwa spika au kupitia kwa uongozi wake kitu ambacho ni kinyume na Katiba.
Ndugai amesema hajamfukuza Lissu bali Katiba ndiyo imemuondoa mbunge huyo ambaye kikao chake cha mwisho cha Bunge kilikuwa Septemba 7, 2017 ambapo mchana wa siku hiyo alipigwa risasi zaidi ya 30 akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma.

Mara baada ya kushambuliwa, alipekewa Hospitali ya Rufaa Dodoma kisha usiku huo huo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako alikaa hadi Januari 6 mwaka 2018 alikohamishiwa nchini Ubelgiji aliko mpaka sasa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527