SERIKALI KUENDELEA KUMSAIDIA MBWANA SAMATTA

SERIKALI imesema itaendelea kumsaidia kwa hali na mali Nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, anayechezea Klabu ya Genk ya Nchini Ubelgiji Mbwana Samatta ili kuhakikisha kuwa anafungua milango ya uwekezaji na kuiweka juu ramani ya Soka la Tanzania katika anga la kimataifa.

 
Akizungumza jana Jumanne (Mei 28, 2019) Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam na Nahodha huyo waTaifa Stars, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alisema Samatta ameonyesha njia iliyoshindwa kufikiwa na wachezaji wengi wa miaka ya nyuma waliojaribu kucheza Soka la kulipwa katika vilabu mbalimbali vya Nchi za Nje hususani Bara la Ulaya.

Dkt. Abbasi alisema Serikali ilimteua Sammatta kuwa Balozi wake wa Utalii kutokana na sifa kubwa zilizoletwa na mchezaji huyo nje ya mipaka ya Tanzania kwa kuwa Serikali ina Imani naye kubwa katika kufungua milango ya fursa za uwekezaji hususani katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano hapa nchini. 

“Mbwana Samatta ameonyesha njia ambayo ilikuwa ndoto iliyoshindwa kutimizwa na wachezaji wengi wa zamani, hatua hii aliyofikia ni kubwa na imetokana na sifa kubwa ya nidhamu na kipaji cha mchezo huu hili ni funzo kwa wachezaji wetu chipukizi” alisema Dkt. Abbasi.

Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi alisema kwa sasa yapo mambo makubwa na mazuri hususani vivutio vya sekta ya utalii, hivyo kupitia nafasi yake ya Ubalozi Serikali itatoa msaada wowote unaohitajiwa na mchezaji huyo ili kuhakikisha kuwa vivutio vya Tanzania vinabainishwa na hivyo kutangaza mambo mazuri ya Tanzania.

Aidha Dkt. Abbasi alisema Ofisi yake imeandaa mikakati mbalimbali ya mawasiliano ya kitaifa katika kuisema nchi katika maeneo mbalimbali hivyo kumtaka mchezaji huyo kutumia majukwaa hayo kwa ajili ya kuona namna bora ya kutumia fursa hizo ili kuitangaza Tanzania nje ya mipaka yake.

Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi alimtaka mchezaji huyo kuwasiliana naye iwapo kutakuwepo na changamoto yoyote anayoweza kuipata katika kutekeleza majukumu yake ya nafasi ya Ubalozi kwani kwa sasa Serikali ya Awamu ya Tano imefungua milango ya ushirikiano na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga hatua katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Kwa upande wake, Nahodha huyo wa Taifa Stars, Mbwana Samatta alisema akiwa nchini Ubelgiji tayari amefanya juhudi kubwa katika kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini, ambapo mwanzoni mwa mwezi ujao madaktari 5 wa timu hiyo wanatarajia kuja nchini kwa ajili ya kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii nchini.

Samatta alisema raia wengi wa kigeni wana shauku ya kutembelea Tanzania kutokana kusikia na kuona uzuri wa vivutio mbalimbali vya utalii ikiwemo Wanyama, hivyo akiwa Balozi wa Utalii afanya kila liwezekanalo  kukaa karibu na viongozi na wachezaji wa klabu yake ya KRC Genk kuwaeleza uzuri wa Tanzania ili na wao waonesha nia ya kuitembelea Tanzania.

“Wachezaji wengi hususani wale wa kiafrika waliopo nje hususani Bara la Ulaya wanaipenda sana Tanzania, na hi inatokana na sifa tuliyonayo, na hivyo kwa kutumia nafasi yangu ya Ubalozi nitaendelea kushawishi waitembelee Tanzania” alisema Samatta.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Samatta Tours, Hamis Waziri aliishukuru Serikali kutokana na jitihada mbalimbali inazofanya kwa ajili ya kuhamasisha sekta ya utalii nchini na kusema taasisi hiyo itakuwa tayari kutangaza matukio mbalimbali kwa ajili ya kulitangaza jina la Tanzania.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم