MAZUNGUMZO YA KIBIASHARA KATI YA MAREKANI NA CHINA YAVUNJIKA


Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Lu Kang amesema kuwa, mazungumzo ya kibiashara kati ya Washington na Beijing yamevunjika.

Kang ameyasema hayo katika kikao na waandishi wa habari mjini Beijing ambapo ameongeza kwamba siasa za kimabavu na mashinikizo yasiyo ya kimantiki ya Marekani dhidi ya China, ndio sababu ya kuvunjika kwa mazungumzo hayo. 

Amesisitiza kwamba, mazungumzo ya kibiashara ya nchi mbili yatafikia natija pale tu maslahi ya pande hizo yatakapozingatiwa sambamba na kuwepo hali ya kuheshimiana kati ya Washington na Beijing. 

Ameongeza kwamba daima China imekuwa ikisisitizia udharura wa kutatuliwa tofauti zote za nchi mbalimbali kupitia njia ya mazungumzo chanya, lakini katika safari yake nchini Japan Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa nchi yake haipo tayari kufikiwa makubaliano ya kibiashara na Beijing.

Hivi karibuni, Marekani ilizipandishia ushuru wa forodha wa asilimia 10, yaani sawa na kiasi cha Dola bilioni 200 bidhaa za China zinazoingizwa nchini Marekani kama ambavyo pia ilitangaza kuwa inafikiria kupandisha ushuru mwingine wa asilimia 25 sawa na kiasi cha Dola bilioni 325 bidhaa za nchi hiyo ya Asia. 

Kufuatia hatua hiyo, serikali ya China nayo ilizipandishia bidhaa za Marekani ushuru wa dola bilioni 60, sawa na asilimia 10 hadi 25. 

Mgogoro wa kibiashara kati ya China na Marekani ulianza tangu mwezi Machi mwaka jana.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527