DIWANI WA CHADEMA APIGWA MARUFUKU KUHUDHURIA VIKAO AKIMTUHUMU MKURUGENZI KUPIGA VIWANJA..RC SHINYANGA AONYA


Diwani wa Kata ya Ngokolo (CHADEMA) manispaa ya Shinyanga Emmanuel Ntobi.Diwani wa kata ya Ngokolo manispaa ya Shinyanga Emmanuel Ntobi, amesimamishwa kutohudhuria vikao vitatu vya baraza la madiwani, kutokana na utovu wa nidhamu kwa kumtuhumu ndani ya baraza mkurugenzi wa manispaa hiyo Geofrey Mwangulumbi kujimilikisha viwanja Vinane kinyume na taratibu.

Maamuzi hayo yametolewa leo Oktoba 30,2018 kwenye kikao cha baraza la kawaida la madiwani hao, wakati ikitolewa taarifa ya kamati ya maadili juu ya diwani huyo kuwa kwenye baraza lililopita alitoa tuhuma kuwa mkurugenzi anajimilikisha viwanja, na hivyo kushindwa kudhibitisha hoja yake hiyo na kuamuriwa kusimamishwa.

Akisoma taarifa ya kamati hiyo ya maadili, Naibu Meya wa manispaa ya Shinyanga John Kisandu, alisema kutokana na diwani huyo kushindwa kuthibitisha ukweli wa kauli yake hiyo, pamoja na kuitwa kwenye kamati kushindwa kuhudhuria na kutotoa maelezo, hivyo wameazimia kumsimamisha kuhudhuria vikao vitatu na kumnyima stahiki zake zote.

“Kanuni ya 28 kipengele cha tatu za kanuni za kudumu za halmashauri (2013) namba mbili, kinasema endapo mjumbe aliyetoa hoja za kashfa akakataa kufuta kauli yake kwa kuomba msamaha kwa maandishi kama alivyoelekezwa na kamati ndogo, Meya wa mkutano atamsimamisha mjumbe huyo kutohudhuria vikao vitatu,”alisema Kisandu

“Mjumbe aliyesimamishwa kwa mujibu wa kanuni hiyo atapoteza haki zake za posho, nauli na kulelewa na kinga kwa muda wote wa kusimamishwa kwake, kutokana na kusema uongo ndani ya baraza,”aliongeza.

Naye mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, ambaye alihudhuria kwenye baraza hilo,kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe na mheshimiwa Rais John pombe Magufuli kuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga, aliunga mkono maamuzi hayo, na kusema kwamba madiwani ambao wataendelea kuwa na utovu wa nidhamu kwenye vikao na kutoa taarifa za uongo na kuleta migogoro, wanapaswa kushughulikiwa.

Alisema kinachopaswa madiwani ni kuwa wamoja na kujadili masuala ya maendeleo ya manispaa hiyo ambayo yapo nyuma, na siyo kuanza kutafuta marumbano yasiyo na tija yatakayokwamisha kujadili mambo ya msingi kwa ajili ya mustakabali wa manispaa hiyo.

Pia alitoa onyo kwa watumishi wa Serikali ambao wamekuwa hawatunzi siri na kuanza kuzitoa hovyo nje hasa kwa wanasiasa, ambao nao wamekuwa wakizianika kupitia mitandao ya kijamii, kuwa atakayebainika watamshughulikia kisheria nachatafaa tena kuwa mtumishi wa umma.

Kwa upande diwani huyo wa Chadema Emmanuel Ntobi, ambaye hakuwepo kwenye kikao hicho ambacho pia kimehudhuriwa na mkuu wa wilaya hiyo,Jasinta Mboneko, akizungumza na Malunde 1 blog kwa njia ya Simu, alisema hajaridhia maamuzi hayo kwani kauli yake ni ya kweli na hajapokea barua yoyote ya kusimamishwa kuhudhuria vikao vya baraza, ambapo kesho atahudhuria kikao hicho.

Na Marco Maduhu - Malunde1 blog

TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Naibu Meya wa manispaa ya Shinyanga John Kisandu akisoma taarifa ya kamati ya maadili pamoja na vifungu vya kanuni ambayo vimesababisha diwani huyo wa Kata ya Ngokolo Emmanuel Ntobi kusimamishwa kutohudhuria vikao vitatu mfululizo vya baraza la madiwani sambamba na kukosa stahiki zake zote kipindi amesimamishwa.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akizungumza kwenye baraza hilo na kuwataka madiwani wawe na umoja na kuacha masuala ya kuichafua halmashauri kupitia mitandao ya kijamii bali waijenge manispaa hiyo ili kuiletea maendeleo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza kwenye baraza la madiwani, na kuwataka, wamalize miradi ambayo ni viporo,kuhamasisha usafi wa mazingira kwa wananchi, kumaliza uhaba wa madawati mashuleni, na mikopo kwa akina mama,vijana na walemavu.
Madiwani wa mansipaa ya Shinyanga wakiwa kwenye kikao chao cha kawaida wakijadili ajenda mbalimbali kwa ajili ya Mustakabali wa manispaa hiyo.
Baraza la madiwani likiendelea.
Diwani wa Kata ya Ndembezi manispaa ya Shinyanga David Nkulila akichangia mada kwenye kikao cha baraza.
Mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Geofrey Mwangulumbi akijibu maswali kwenye baraza hilo.
Madiwani wakiendelea na kikao cha baraza.
Diwani wa Viti maalumu CCM Shela Mshandete akichangia hoja kwenye baraza la madiwani.
Diwani wa Kata ya Masekelo manispaa ya Shinyanga Samweli Sambayi akichangia hoja kwenye baraza .
Diwani wa Kata ya Mwawaza manispaa ya Shinyanga Juma Nkwabi akichangia hoja kwenye baraza.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack mkono wa kulia akiwa na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko kwenye kikao cha baraza la kawaida la madiwani wa manispaa ya Shinyanga.
Watumishi wa manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye baraza la madiwani.
Watumishi wa manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye baraza la madiwani.
Wachukua kumbukumbu (CC) wa manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye baraza la madiwani wakiandika ndondoo za kwenye baraza hilo.

Na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم