Picha: DC SHINYANGA AFANYA MKUTANO KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI BUGAYAMBELELE..AKOMAA NA WATENDAJI,WENYEVITI

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga amewataka maafisa watendaji wa vijiji na kata kusoma taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi pamoja na wenyeviti wa vitongoji,mitaa,vijiji na kata kufanya mikutano kwa ajili ya kutatua kero zinazowakabili wananchi.

Matiro ametoa agizo hilo leo Jumatatu Februari 26,2018 wakati wa mkutano wa kusikiliza kero za wananchi akiwa ameambatana na maafisa mbalimbali wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga katika kijiji cha Bugayambelele kata ya Kizumbi katika manispaa ya Shinyanga.

Alitoa agizo hilo baada ya wananchi kudai kuwa viongozi waliopo katika kata hiyo hawafanyi mikutano kusikiliza kero za wananchi na badala yake wamekuwa wakisubiri uchaguzi ukikaribia ndiyo wanajitokeza.

Mmoja wa wananchi hao,Paul Kashinje (87) alisema viongozi wa eneo hilo hawawajibiki kwa wananchi matokeo yake wamekuwa wakikabiliwa na changamoto lukuki na kutoa tahadhari kuwa kipindi hiki wanataka vitendo zaidi kuliko maneno kwa viongozi hao na wasipobadilika watawashughulikia.

Kufuatia hoja hiyo na zingine,Matiro aliwaagiza viongozi wa vitongoji,vijiji,mitaa na kata kuhakikisha wafanya mikutano na wananchi ili kujadili namna ya kutatua kero zao huku akiagiza maafisa watendaji kusoma taarifa za mapato na matumizi ili kuondoa migongano isiyokuwa ya lazima.

Katika hatua nyingine Matiro alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kujenga nyumba bora badala ya kuishi kwenye nyumba za udongo ambazo ni rahisi kubomoka inaponyesha hata mvua kidogo tu.

Matiro pia aliwataka wananchi kutunza mazingira kwa kupanda miti na kuitunza na kulima zao la mtama badala ya kulima mahindi ambayo ustawi wake siyo mzuri mkoani Shinyanga.

Wakizungumza mbele ya mkuu wa wilaya,wananchi walizitaja baadhi ya kero zao kuwa ni kukosekana kwa eneo la mazishi “makaburi”,ukosefu wa shule,barabara,zahanati,maji,umeme na migogoro ya viwanja.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro (kulia) akimsikiliza kwa makini mwananchi mkazi wa kijiji cha Bugayambelele akielezea jinsi anavyoteseka kupata huduma ya maji -Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mzee Paul Kashinje akieleza kero yake kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro ...Alisema "Viongozi wetu hawafanyi chochote,ujio wako hapa naamini utasaidia...Tumechoka na maneno yao,tunahitaji vitendo,bila vitendo tunawashughulikia".
William Mlori akielezea kero ya viwanja na ardhi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akitoa majibu ya kero za wananchi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwasititiza viongozi kushirikisha wananchi katika masuala ya maendeleo.
Wananchi wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro 
Diwani wa kata ya Kizumbi Reuben Kitinya akieleza namna wanavyotatua kero za wananchi.
Mwananchi akielezea kero yake.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiandika dondoo muhimu wakati wa mkutano huo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro na maafisa mbalimbali wakiwa katika mkutano huo.
Maafisa kutoka halmashauri ya manispaa ya Shinyanga wakiwa eneo la mkutano.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Katunda,kijiji cha Bugayambelele,Safari Elias akizungumza katika mkutano huo.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم