WAZIRI MKUU ABAINI UOZO MWINGINE BANDARINI


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amebaini mpango wa kutaka kuyatoa bandarini matrela 44 ya malori makubwa, maarufu kama semitrela, bila ya kuyalipia kodi, huku wahusika wa mpango huo wakitumia jina la Waziri Mkuu.

Alibaini hayo alipofanya ziara ya kushitukiza katika Bandari ya Dar es Salaam, jana.

 Kutokana na tukio hilo, Majaliwa alimuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, kuwakamata mmiliki wa kampuni ya NAS Haulage aliyetajwa kwa jina moja la Bahman na Wakala wa Kampuni ya Wallmark, aliyetajwa pia kwa jina moja la Samwel kwa kuhusishwa na njama hizo.

Pia Waziri Mkuu aliitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutowasikiliza wafanyabiashara wanaotaka kukwepa kodi, kwa madai ya kupewa vibali vya msamaha wa kodi kutoka kwa viongozi wa juu serikalini. "Mtu asije hapa aseme amepewa kibali na Rais John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan au Waziri Mkuu, cha kutaka kutoa mzigo wake bila ya kufuata taratibu.

Akija mtu na taarifa hizo akamatwe mara moja na achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria," aliagiza. Waziri Mkuu alilazimika kufanya ziara hiyo ya ghafla jana baada ya kupata taarifa za mfanyabiashara huyo aliyetaka kuudanganya uongozi wa TPA, kutaka kutoa matrela hayo yaliyoingizwa nchini mwaka 2015 kutoka Uturuki. Bahman alitaka kupata msamaha wa kodi kwa kuidanganya TPA, kuwa amewasiliana na Waziri Mkuu na wasipotekeleza jambo hilo, watapata matatizo.

Majaliwa alisema serikali inasisitiza watu kufuata sheria na taratibu za nchi, ikiwemo kulipa kodi ipasavyo na inataka watendaji wake wafanye kazi bila ya kubughudhiwa, hivyo aliwataka wafanyabiashara kufuata sheria za nchi na kwamba serikali haina ugomvi nao.

Waziri Mkuu alifafanua kuwa mfanyabiashara huyo alitaka kuyatoa matrela hayo bila ya kukamilisha malipo ya ununuzi kutoka kwenye kampuni Serin ya Uturuki. "Magari haya aliyalipia asilimia 30 tu kwa makubaliano ya kumaliza asilimia 70 iliyobaki baada ya kufika Tanzania na atakapokamilisha ndipo angepewa nyaraka, ambayo inaonesha jina la mwenye mzigo, aina ya mzigo na thamani (bill of lading) inasaidia mteja kufanyiwa tathmini ya gharama za kulipia ushuru, lakini huyu bwana hajafanya hivyo," alisema.

Alieleza kuwa kitendo cha kuyasajili magari hayo bila ya kuwa na nyaraka hizo, ni kinyume cha sheria; na pia kinaweza kusababisha kampuni iliyouza magari hayo ya Serin kutolipwa malipo yaliyobaki. Alisema jambo hilo halikubaliki kwa sababu linaweza kudhoofisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Uturuki, kwani tayari kampuni hiyo imeshawasilisha malalamiko hayo katika ofisi za Ubalozi wa Uturuki nchini.

"Uturuki wanawaamini sana wafanyabiashara wa Tanzania, sasa huu ujanjaunja uliotumika katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuyasajili magari haya bila ya kuwa na bill of lading halisi, unajenga sura mbaya kwa wafanyabiashara wengine waaminifu na watiifu wa sheria, nawaagiza TRA kuchukua hatua kwa wahusika, hatuwezi kupoteza mahusiano na nchi kwa sababu ya utapeli wa mfanyabiashara mmoja," alisema.

Pia Waziri Mkuu alitoa mwito kwa mawakala wa forodha, kuhakikisha wanakuwa makini katika kazi zao na serikali haitawavumilia wababaishaji, kwani inasisitiza wafanyabiashara kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo. 

Awali, Mkurugenzi wa Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko alimweleza Waziri Mkuu kuwa pamoja na vitisho vya mfanyabiashara huyo kuwa wasipotekeleza matakwa yake watapata matatizo, lakini waliendelea kusimamia sheria na taratibu.
Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم