MAKAMU WA RAIS TANZANIA ATUMA SALAMU ZA PONGEZI KWA MKUU WA MKOA WA GEITA KUOKOA WACHIMBAJI 15 WALIOFUKIWA UDONGO MGODINI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amemtumia salamu za pole na pongezi Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga kwa kazi nzuri na kubwa waliyoifanya ya kuwaokoa wachimbaji wadogo 15 waliofukiwa na maporomoko ya udongo kwenye Mgodi wa Dhahabu wa RZU uliopo katika Kijiji cha Nyarugusu, wilaya ya Geita katika mkoa wa Geita.


Tukio hilo la kufukiwa wachimbaji hao wadogo 15 wakiwemo Watanzania 14 na raia Mmoja wa China lilitokea usiku wa Tarehe 26 Januari mwaka 2016.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amesema amepokea kwa furaha taarifa za kuokolewa kwa wachimbaji hao wadogo na amesifu na kupongeza jitihada za kuwaokoa wachimbaji hao zilizofanywa na Serikali ya Mkoa wa Geita, Jumuiya ya Wachimbaji Wadogo wa mkoa wa Geita, Wamiliki wa Migodi ya Dhahabu na wananchi kwa ujumla kwa kutoa vifaa mbalimbali vya uokoaji jitihada ambazo zimepelekea kuokolewa kwa wachimbaji hao wakiwa hai.


Makamu wa Rais amesisitiza kuwa “jitihada ,Umoja na Mshikamano ulioonyeshwa na makundi mbalimbali katika kuwaokoa ndugu zetu waliofukiwa na maporomoko ya Udongo wakiwa kazini huko Geita ni mfano mzuri na wakuigwa na wananchi na taasisi nyingine nchini katika kujitolea kwa hali na mali hasa vifaa vya uokoaji kwa ajili ya kusaidia watu wanaopatwa na majanga ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea kama walivyofanya ndugu zetu wa mkoa wa Geita nawapongeza Sana”.


Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amewataka wamiliki wa migodi kote nchini wahakikishe wanafanya kazi zao za uchimbaji wa madini kwa kuzingatia kanuni,taratibu na sheria kama hatua ya kuepuka madhara yanayoweza kutokea wakiwa wanafanya shughuli zao za uchimbaji wa madini.


Kupitia kwako Mkuu wa mkoa wa Geita napenda kutuma salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kutokea kwa tukio hilo na nawaombea kwa Mwenyezi Mungu wachimbaji hao ambao kwa sasa wanapatiwa matibabu Katika Hospitali ya Serikali ya mkoa wa GEITA matibabu mema ili waweze kupona haraka na kurejea kwenye kazi zao za kujitafutia riziki.


Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Kudhibiti Maafa nchini, Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Geita na kupekelea kuchukuliwa hatua za haraka katika kushughulikia ajali hiyo.


Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dar es Salaam 


29-Jan-2017

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم