Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Majanga Shinyanga! Shule ya Bugoyi "B" Yafungwa Kwa Ubovu wa Choo,Wananchi Wasusia..Diwani Atema Cheche..DC Acharuka, Angalia Picha



Choo cha wanafunzi katika shule ya msingi Bugoyi B kilichojengwa bila nondo kama unavyoona picha kimebomoka na kutitia huku wanafunzi wakiendelea kukitumia,angalia mzigo hapo upande wa kulia-Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog

*****



Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ametoa agizo la kufunguliwa kwa shule ya msingi Bugoyi ‘B’ iliyopo katika manispaa ya Shinyanga iliyoamuriwa kufungwa na ofisa afya wa kata ya Ndembezi ilipo shule hiyo kutokana na vyoo vyake kutitia kwa kujengwa chini ya kiwango.Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog,bwana Kadama Malunde anaripoti habari hii kwa kina.


Shule hiyo ilifungwa siku ya Jumatano Julai 13,2016 kwa muda usiojulikana kutokana na vyoo vilivyokuwa vinatumiwa na wanafunzi vilivyojengwa na manispaa ya Shinyanga mwaka 2004 kubomoka kwa kile kilichoelezwa kuwa ujenzi wake ulifanyika chini ya kiwango bila kuwekwa nondo na nyavu ndogo ndogo (wayameshi) ambapo wananchi walisema fedha zilichakachuliwa.

Katika barua iliyotolewa na afisa afya wa kata ya Ndembezi Costancia Michael kwenye kikao cha wazazi kilichofanyika shuleni hapo jana Julai 13, asubuhi,alisema walifanya ukaguzi kwenye shule hiyo na kubaini kuwa haina vyoo kutokana na matundu nane yaliyokuwepo kubomoka na kusababisha wanafunzi 909 kuchangia vyoo na walimu 25 ambayo ni matundu manne jambo ambalo ni hatari kiafya.

“Ukosefu wa vyoo kwenye shule ni kosa kwa mujibu wa sheria na amri ya kufungwa kwa shule hiyo Bugoyi ‘B’ imetolewa chini ya kifungu cha 163(iii),164(i) na (3) b cha sheria ya afya ya umma Na 1 ya mwaka 2009 kwani inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza kikiwemo kipindupindu",alifafanua afisa afya huyo.

Muda mfupi baada ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro kupata taarifa za kufungwa kwa shule hiyo kwa muda usiojulikana ,alifika shuleni hapo na kueleza kuwa hatua iliyochukuliwa haijamfurahisha huku akiwatupia lawama viongozi wa kata na manispaa kwa uzembe waliouonesha.

“Uongozi wa kata na manispaa mmeonesha uzembe wa hali ya juu,choo kimetitia tangu Juni 13 mwaka huu,wakati wanafunzi wakiwa likizo,mratibu elimu kata anasema walitoa taarifa kwa afisa elimu wa manispaa na wamekuwa wakisubiri majibu ya barua yao mpaka shule imefunguliwa...ujenzi wa vyoo ungeweza kufanyika wakati wanafunzi hawajafungua shule...leo mnafunga shule ili watoto wasisome? hii haiwezekani",alisema mkuu huyo wa wilaya.

Matiro aliagiza shule hiyo ifunguliwe mara moja ili wanafunzi waendelee na masomo kwani hawajawatendea haki na kusisitiza kuwa uongozi wa kata na manispaa ndiyo wameonyesha uzembe wa kuleta siasa kwenye masuala ya maendeleo.

“Wanafunzi hawa hatujawatendea haki..nataka shule ifunguliwe mara moja ,wanafunzi watatumia vyoo vya shule ya jirani na vyoo vya walimu huku wakisubiri vyoo vingine kujengwa na zoezi la kujenga vyoo vipya lianze mara moja ” ,alisema Matiro.

Alisema haiwezekani tangu Juni 13 mwaka huu vyoo vilititia wakati wanafunzi wakiwa likizo lakini mpaka shule inafunguliwa Julai 11,2016 bado viongozi wanasema wanafuatilia suala hilo.

Matiro alisema waliofunga shule hiyo wako sahihi kwani ilikuwa hatari kwa wanafunzi hao na kusisitiza kuwa viongozi wanatakiwa kuacha siasa kwenye mambo ya maendeleo.

Akielezea zaidi kuhusu kutitia kwa vyoo hivyo mbele ya mkuu wa wilaya,Mratibu elimu kata ya Ndembezi Johansen Muntu alisema alipewa taarifa na mwalimu mkuu wa shule hiyo kuhusu kutitia kwa vyoo hivyo Juni 13 mwaka huu na kuamua kutoa taarifa kwa afisa elimu wa manispaa ya Shinyanga.

"Tangu nilipotoa taarifa nimekuwa nikifuatilia lakini kila nikifika kwa afisa elimu alikuwa ananiambia siyo kazi yangu kufuatilia, suala hilo halituhusu,amekuwa kimya mpaka shule inafunguliwa Julai 11 mwaka huu,tumeshangaa leo Julai 13 tunapewa taarifa tena kwa barua iliyoelekezwa kwa mwalimu mkuu na nakala kwa mkurugenzi wa manispaa,afisa afya kwa manispaa,afisa elimu wa manispaa na afisa mtendaji wa kata",alieleza Muntu.

"Ili kulinda afya za wanafunzi na jamii kwa ujumla,unaamuriwa kufunga shule yako kuanzia tarehe ya barua hii hadi hapo utakaporekebisha mapungufu yaliyoelezwa kwa kujenga vyoo vingine vyenye matundu yasiyopungua 40 ya kutosha idadi ya wanafunzi 909 ya wanafunzi wako",alinukuu baadhi ya maneno katika barua hiyo.

Hata hivyo juhudi za mkuu huyo wa wilaya zimezaa matunda baada ya uongozi wa manispaa ya Shinyanga kupeleka greda kwa ajili ya kuchimba mashimo ya vyoo katika shule hiyo kuanzia siku ya Alhamis,Julai 14 ,2016.


Naye mkuu wa shule ya msingi Bugoyi ‘A’ mwalimu Peter Ajali alikubali wanafunzi wa shule ya msingi Bugoyi B yenye wanafunzi zaidi ya 900 kutumia vyoo vya shule yake vyenye matundu ya vyoo 15 huku wanafunzi wakiwa zaidi ya 1300 huku akieleza kuwa hata hayo hayatoshi kwa wanafunzi wa shule hiyo pekee ambapo bado kulikuwa na upungufu wa matundu 35 ya vyoo.


Akizungumza na Malunde1 blog ,mapema leo Julai 14,2016, mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Omari Gindu alisema kuanza kwa ujenzi wa vyoo kumetokana na msukumo alioutoa mkuu wa wilaya aliyekerwa na uzembe wa viongozi na kuongeza kuwa tayari wanafunzi wameanza kuhudhuria masomo yao darasani.

Akizungumza kwenye kikao cha wazazi wanaosomesha watoto wao katika shule hiyo kilichofanyika Julai 13,2016 ,diwani wa kata ya Ndembezi David Nkulila , alisema kubomoka kwa vyoo hivyo kumesababishwa na uzembe uliofanywa na wataalam wa halmashauri akiwemo injinia kwa kushindwa kusimamia vizuri na kutaka kusababisha madhara kwa watumiaji wa vyoo hivyo.

“Inatuuma sana hii ni michango ya wananchi inateketea bure kwa uzembe wa mainjinia wa manispaa yetu, mkurugenzi na watu wao mtajua njia mtakayotumia kujenga choo hiki maana uzembe ni wa watumishi wako na hatutakubali watoto wetu wasome katika mazingira hatarishi lazima shule ifungwe watabaki darasa la saba na la nne”,alisema Nkulila.


Alisema tatizo lililopo ni wataalamu wa halmashauri kutozingatia ushauri wanaopewa kwa kuona kuwa wao ni wasomi wanajua kila kitu na kuwapuuza wengine ambao hawana elimu , matokeo yake tatizo linapotokea wanaanza kubadilisha maneno kwa kuweka utalaamu wao mbele na kusingizia siasa.

Mtendaji wa kata ya Ndembezi Felister Msemelwa alisema kuwa utaratibu ulifuatwa wa kuandika barua ili mhandisi wa manispaa aje kuwatolea ramani ( BOQ) na kuthaminisha kiasi cha fedha kinachohitajika wazazi walikubali kuchangia ila barua ya majibu kutoka manispaa ndiyo ilichelewa na kuyapata wakati wanafunzi wamekwisha fungua shule.


Naye mwenyekiti wa mtaa wa Mbuyuni ilipo shule hiyo Chifu Abdalah Sube alisema vyoo hivyo viko katika hali mbaya kwani vilijengwa chini ya kiwango hali iliyosababisha kutitia na sehemu nyingine kubomoka jambo ambalo ni hatari kwa watoto na kwamba kufungwa kwa muda shule hiyo ni hatua nzuri.

Afisa elimu wa manispaa hiyo Yesse Kanyuma aliyefika kwenye kikao cha wazazi  kwa niaba ya mkurugenzi wa manispaa alisema hajafurahishwa na hatua iliyochukuliwa na jinsi kikao kilivyoendeshwa ,ambapo awali nusura mkutano huo uvunjike baada ya afisa elimu kudai mkutano huo ni wananchi na siyo wazazi wa watoto.

Kanyuma alisema serikali imeshatenga milioni 5 za kuanzia ujenzi wa vyoo hivyo, lakini wananchi wanapaswa kuchimba shimo ndiyo ujenzi uanze, kauli ambayo ilipingwa vikali na wazazi na kusababisha kikao hicho kitake kuvunjika.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Eustadius Nkulu alisema hatua ya kufungwa kwa muda shule hiyo imewaathiri wanafunzi kutokana na kukosa masomo kwani haijajulikana ni lini mapungufu yaliyopo yatafanyiwa kazi ili wanafunzi waendelee na masomo na kwa kuzingatia kuwa darasa la nne la saba wanajiandaa kufanya mitihani miezi michache ijayo.

Nkulu alimueleza mkuu wa wilaya kuwa tatizo lililojitokeza na kushindwa kufanyika utekelezaji ni viongozi na wazazi kulihusisha suala la maendeleo na siasa kwani baadhi ya wazazi wakikubali kutekeleza kitu fulani hujitokeza kundi lingine kupinga na kujikuta wanakata tamaa.

Nao wazazi wanaosomesha watoto wao kwenye shule hiyo walikubaliana na uamuzi huo wa kufungwa kwa shule, huku wakiitupia lawama halmashauri kwa uzembe walioufanya wa kusimamia choo hicho kujengwa chini ya kiwango bila ya kuwekwa nondo chini yake na kusababisha kutitia na kuhatarisha maisha ya watoto wao.

Aidha wazazi hao waliitaka halmashauri ijenge vyoo hivyo haraka na wao hawawezi kuchangia chochote juu ya ujenzi huo, ikiwa hapo awali mwaka (2004 ) walichanga fedha na hatimaye choo kujengwa chini ya kiwango kwa usimamizi wa halmashauri, hivyo wao ndio wenye jukumu la kujenga vyoo hivyo.
 
Barua ya kufungwa kwa shule ya Bugoyi B

Julai 13,2016 Asubuhi-Mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi Bugoyi 'B akichungulia kwenye choo cha shule hiyo alipotaka kujisaidia na kuogopa kutumbukia na hivyo kuamua kujisaidia nyuma ya uzio wa shule ili kunusuru maisha yake mara baada ya bampa la choo kutumbukia ambapo choo hicho chenye matundu manane kilijengwa bila nondo kwa usimamizi wa wahandisi wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga.

Wanafunzi wa shule ya msingi Bugoyi B wakiwa eneo la vyoo vya shule hiyo pamoja na baadhi ya wazazi wao kama unavyoona wakitahamaki jinsi walivyokuwa wanahatarisha usalama wa maisha yao .

Wanafunzi wakizagaa ovyo shuleni baada ya kukosa mahali pa kujisaidia huku muda mwingine wakichangia choo kimoja na walimu wao ambacho kipo salama ,nacho kikiwa hakikidhi mahitaji ya wanafunzi 909 huku walimu wakiwa 25 na hivyo kuwepo hatari ya kufumaniana chooni.

Wazazi nao wakishuhudia matundu hayo ya vyoo vya shule jinsi vinavyo hatarisha maisha ya watoto wao na hivyo kuridhia agizo la idara ya afya ya kata kuifunga shule hiyo hadi pale ujenzi wa matundu mapya ya vyoo vitakapokamilika kujengwa.

Wazazi wakiendelea na ukaguzi wa vyoo vya shule ambavyo vilishatitia na muda wowote vinaweza kusababisha vifo vya wanafunzi
Mwenyekiti wa mtaa wa Mbuyuni kata ya Ndembezi Chifu Abdalah Sube akifungua kikao cha wazazi ili kujadili mstakabali wa vyoo hivyo na kunusuru maisha ya watoto wao.

Afisa elimu wa shule za msingi manispaa ya Shinyanga Yesse Kanyuma akiomba radhi wazazi mara baada ya kuharibu hali ya hewa kwa kutoa kauli tata kwao na kuwalazimisha wachimbe kwanza shimo la choo ndipo halmashauri itoe pesa ya ujenzi lasivyo hakuna kitakachoendelea.


Kauli hiyo ilipingwa vikali na wazazi na kudai kuwa choo hicho kilicho anguka walichanga pesa zao na kusimamiwa na halmashauri lakini wahandisi wakachakachua pesa zao na kujenga chini ya kiwango.

Wazazi walidai kuwa kutokana uzembe huo kufanywa na halmashauri hivyo wananchi hawatachangia bali halmashauri ndio ihusike na ujenzi huo ili ifidishie pesa walizochakachua kwa wananchi.

Diwani wa kata ya Ndembezi David Nkulila akituliza hasira za wazazi wawe wapole ili kujadili hatma ya choo hicho.

Kikao kiliendelea huku wazazi wakigeuka mbogo na kutokubali kutoa pesa zingine za ujenzi wa choo hicho kutokana na hapo awali pesa zao kuchezewa na kujengwa choo chini ya kiwango.

Wazazi wakisikiliza maneno kutoka kwa viongozi wao na hivyo kuridhia shule hiyo ifungwe mpala pale ujenzi wa choo utakapo kamilika ili kunusuru maisha ya watoto wao
Julai 13,2016 mchana-Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro (kulia) akielekea kwenye vyoo vya wanafunzi katika shule ya msingi Bugoyi B katika manispaa ya Shinyanga

Vyoo vya wanafunzi vikiwa vimefungwa kwa miiba kutokana na kuwa vimeharibika kwa sababu ya kujengwa chini ya kiwango

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiingia kwenye choo kilichotitia

Choo kikiwa kimetitia kutokana na kutokuwa na nondo

Pamoja na kwamba choo kimeharibika lakini wanafunzi walikuwa wanajisaidia katika choo hicho
Mwenyekiti wa kamati ya shule ya msingi Bugoyi B Omari Gindu akimuonesha mkuu wa wilaya jinsi choo cha wanafunzi kilivyotitia

Nyuma ya choo cha wanafunzi,nyufa zikionekana

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bugoyi B Eustadius Nkulu akitoa maelezo kwa mkuu wa wilaya kuhusu tatizo la choo katika shule yake,kulia ni
afisa afya wa kata ya Ndembezi Costancia Michael alitoa amri ya kufungwa kwa shule ya msingi Bugoyi B
Afisa elimu wa manispaa ya Shinyanga Yesse Kanyuma akijieleza kwa mkuu wa wilaya kuhusu vyoo kutitia kwa sababu ya uzembe.Kulia ni mratibu elimu kata ya Ndembezi bwana Johansen Muntu
Waandishi wa habari wakiwa eneo la tukio

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza katika vyoo vya wanafunzi ambapo alisema mambo ya siasa na uzembe wa uongozi wa kata na manispaa umechangia kuwepo kwa tatizo hilo

Mwenyekiti wa mtaa wa Mbuyuni ilipo shule hiyo Chifu Abdalah Sube akieleza matatizo yaliyopo katika shule hiyo ambapo alisema kamati ya shule hiyo inaongozwa na mtu mmoja ambaye ni Omari Gindu na kwamba hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa matatizo katika shule hiyo

Mkuu wa wilaya akiwa katika eneo ambapo choo kitajengwa

Julai 14,2016 asubuhi-Greda likichimba shimo la choo katika shule ya msingi Bugoyi B baada ya mkuu wa wilaya kuagiza choo kijengwe haraka

Shimo la choo likiendelea kuchimbwa

Kushoto ni Mwalimu mkuu msaidizi wa shule ya msingi Bugoyi B,Gaudensia Mathias (katikati) na Mtendaji wa kata ya Ndembezi Felister Msemelwa na mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Omari Gindu wakiangalia shimo la choo
Mwenyekiti wa kamati ya shule ya Bugoyi B Omari Gindu akionesha shimo hilo.
Picha zote na Kadama Malunde wa Malunde1 blog na Marco Maduhu wa Msukuma Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com