News Alert_MUSWADA WA HABARI WAONDOLEWA BUNGENI


 

Serikali imeuondoa muswada wa sheria ya haki ya kupata habari uliokuwa uwasilisilishwe na kujadiliwa katika mkutano unaondelea wa bunge mjini Dodoma.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (asiye na wizara maalum) Prof Mark Mwandosya ameliambia bunge leo asubuhi kuwa serikali imefikia uamuzi huo kutokana na maoni ya kamati ya kudumu ya bunge ya maendeleo ya jamiii iliyotaka musawada huo uondolewe ili kutoa muda wa kujadiliwa na wadau.

Katika taarifa yake hiyo kwa Bunge Mh. Mwandosya amewataka wadau wa habari waendelee kutoa ushauri juu ya muswada huo pamoja na kuchangia maoni zaidi ili kupata muswada ulio bora zaidi.

Prof Mwandosya amesema muswada huo utawasilishwa na kujadiliwa katika mkutano ujao wa bunge ambao utakuwa ni wa bunge la kumi na moja chini ya serikali ya awamu ya tano.

Uamuzi huo wa serikali umekuja kutokana na muswada huo kuzusha mgogoro na wadau wa tasnia ya habari baada ya kuonekana kutowashirikisha wadau wa habari moja kwa moja lakini pia kuonekana inaminya uhuru wa wananchi kupata habari.

Wadau mbalimbali wa habari wakiwemo chama cha wamiliki wa vyombo vya habari MOAT wamekuwa wakilalamikia maudhui ya muswada huo kwa madai ya kuminya uhuru wa vyombo vya habari pamoja na haki ya kupata taarifa kwa wananchi.

Katika mahojiano na mwanachama wa MOAT ambaye ni mwanzilishi mwenza wa mtandao wa Jamii Forums jana Maxence Melo, alisema kuwa endapo muswada huo ungepitishwa na kuwa sheria, basi tasnia nzima ya habari ingekufa kwa kuwa umeweka njia ngumu ambazo hazitekelezeki katika upatikana wa taarifa pamoja na mlolongo wa adhabu kali kwa wadau na waandishi watakaokiuka sheria hiyo.

Naye mwanasheria na mtafiti wa uchumi na biashara kutoka katika kituo cha sheria na haki za binadamu Masud George alisema kuwa muswada huo ni hatari kwa uchumi wa nchi kwani shughuli nyingi za kiuchumi zinategemea upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati.

Aliongeza pia kuwa, vyombo binafsi vya habari kama sehemu ya wawekezaji katika sekta binafsi na chanzo muhimu cha ajira wanachangia kiasi kikubwa cha uchumi wa nchi hivyo kuwadhoofisha ni kudhoofisha uchumi wa nchi kiujumla.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527