Taarifa Kamili!! MWANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI AMUUA MWENZAKE WAKIGOMBANIA DAFTARI LA NOTES DARASANI HUKO SHINYANGA VIJIJINI

Mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Ilola iliyopo katika wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga Veronica Venance(12) amefariki dunia kwa kupigwa na mwanafunzi mwenzake wakati wakigombania daftari darasani  kwa ajili ya kuandika dondoo (notes).

Tukio hilo limetokea Februari 24 ,mwaka huu saa 7 na nusu mchana katika darasa la tano shule ya msingi Ilola iliyopo katika kata ya Ilola tarafa ya Itwangi wilaya ya Shinyanga.

Walioshuhudia tukio hilo walisema mwanafunzi huyo aliyekuwa anasoma darasa la tano alifariki dunia baada ya kupigwa makofi na ngumi sehemu za kichwani na mwanafunzi mwenzake aitwaye Sophia Mathew(12) ambaye pia ni mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo kutokana na ugomvi uliotokana na  kugombania daftari.

Akizungumza na Malunde1 blog, afisa mtendaji wa kata ya Ilola Mahona Joseph alisema tukio hilo lilitokea wakati wanafunzi hao wakigombania daftari ambapo marehemu alikuwa ameng’ang’ania daftari aliloazima kwa mwanafunzi mwenzake Sophia Mathew kwa ajili ya kuandika dondoo za daftari hilo.

Alisema kitendo cha kung’ang’ania daftari hilo wakati siyo mali yake kilimkera mwanafunzi mwenzake na kuzua ugomvi kati ya wanafunzi hao na kubababisha kifo cha mwanafunzi huyo.

Naye mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ilola Magere Jonas aliiambia malunde1 blog kuwa tukio hilo lilitokea wakati wanafunzi hao wakigombana darasani na kwamba huenda mwanafunzi huyo aliumia kisogoni baada ya kuanguka wakati wa ugomvi huo.

“Ilikuwa muda wa saa saba mchana wakati wanafunzi wengi wameenda kula wengine wakiwa bado wako shuleni,walimu walikuwa majumbani lakini mimi na mwalimu mkuu msaidizi tulikuwa chini ya mti tunapunga upepo,mara akaja mwanafunzi mmoja akasema kuna wanafunzi wanagombana darasani, ndipo tukaenda na kumkuta amelala chali darasani” alisimulia mwalimu mkuu.

“Kufuatia hali hiyo tukachukua jukumu la kumpeleka kwenye zahanati ya Ilola ambapo nesi akatushauri kwenda kituo cha afya cha Bugisi kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo mwanafunzi huyo lakini tulipofika Bugisi tukaambiwa tayari ameshafariki dunia,tunahisi pengine aliumia kisogoni”,alieleza mwalimu Jonas.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Longinus Tibishubwamu alisema wanamshikilia mtuhumiwa Sophia Mathew anayedaiwa kumpiga Veronica Venance sehemu za kichwani kwa kutumia mikono yake.
Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم