KAVUMBANGU ASAINI MIAKA MIWILI AZAM FC


Kavumbangu akitia dole gomba Mkataba wa Azam leo

NAHODHA wa Burundi, Didier Kavumbangu amesaini Mkataba wa miaka miwili na mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Azam FC mchana wa leo, BIN ZUBEIRY imeipata hiyo.


Kavumbangu aliyemaliza Mkataba wake wa miaka miwili Yanga SC, ameamua kusaini Azam FC baada ya kuona klabu yake haina mawasiliano naye licha ya kumaliza Mkataba wake.


“Mimi ni mchezaji, kazi yangu ni mpira. Nimemaliza mkataba Yanga, lakini viongozi hawaniambii kitu, nimepata ofa nzuri Azam nikaamua kusaini,” amesema Kavumbangu akizungumza  baada ya kusaini Mkataba huo ambao unamfanya alipwe vizuri kuliko alivyokuwa analipwa Jangwani.



Pamoja na hayo, Kavumbangu ameishukuru Yanga SC na mashabiki kwa miaka miwili aliyoichezea timu hiyo na anasema itabakia kwenye kumbukumbu zake kwa ameshinda nayo mataji.


Mshambuliaji huyo mrefu mwenye nguvu amesema sasa akili yake anaipeleka kwa mwajiri wake mpya, Azam FC ambako pia amepania kwenda kushinda mataji na kuiwezesha timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika.
  
“Mimi sasa ni mchezaji wa Azam, nafurahi kujiunga na klabu hii kubwa. Kawaida yangu huwa nashabikia klabu nayochezea, sasa mimi ni mshabiki namba moja wa Azam,”amesema.   



Kavumbangu alitua Yanga mwaka 2013 akitokea Atletico ya Burundi na katika mechi misimu miwili ya kuichezea klabu hiyo, amefunga mabao 31 katika mechi 63 za mashindano yote, moja tu la penalti.

Na Mahmoud Zubeiry-Dar es Salaam

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments