Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Chama cha Madaktari wa Kikristo Tanzania (TCMA) kimesema hospitali na vituo vya afya vinavyomilikiwa na taasisi za dini vimekuwa na mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za afya nchini, huku vikitoa takribani asilimia 42 ya huduma hizo kwa miaka mingi ikiwa ni hatua ya kuunga mkono Serikali katika kuihudumia jamii.
Rais wa Chama cha Madaktari Wakristo Tanzania (TCMA),ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Upasuaji katika Hospitali ya Mwambani, Songwe,
Padre Gilbert Sanga, amesema mchango huo unaifanya taasisi za dini kuwa sehemu muhimu ya mfumo wa afya nchini, hususan katika maeneo ya vijijini.
Amesema kwa sasa kuna takribani vituo 900 vya afya na hospitali 100 vinavyomilikiwa na taasisi za dini na vinatoa huduma mbalimbali, ikiwemo za rufaa katika ngazi za mikoa na maeneo mengine.
Padre Sanga amesema hayo katika Mkutano Mkuu wa 89 wa TCMA unaoendelea jijini Dodoma, akieleza kuwa mkutano huo umejikita katika kujadili namna ya kuboresha huduma zinazotolewa katika vituo vya taasisi za dini, kuimarisha ushirikiano na Serikali pamoja na kuweka mikakati ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
Padre Sanga amesema TCMA imekuwa ikifanya mikutano kila mwaka tangu kuanzishwa kwake mwaka 1937, huku mkutano wa mwaka huu ukiwa wa 89 na umejikita katika kujadili namna ya kuboresha huduma za afya zinazotolewa katika vituo vinavyomilikiwa na taasisi za dini na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, watoa huduma na wadau wengine.
Amesema moja ya ajenda muhimu katika mkutano huo ni utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, ambapo hospitali na vituo vya afya vya taasisi za dini vimeingia katika mchakato wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma kupitia mfumo huo.
Kwa mujibu wa Padre Sanga, afya ya akili mahali pa kazi, pia imepewa kipaumbele katika mkutano huo kutokana na umuhimu wake katika ustawi wa watumishi na ubora wa huduma wanazozitoa kwa wananchi.
Padre Sanga amesema sehemu kubwa ya vituo hivyo ipo vijijini ambako wananchi wengi wanahitaji huduma za afya, hivyo uwepo wa hospitali hizo umesaidia kupunguza changamoto ya wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu.
Amesema ushirikiano kati ya Kanisa na Serikali katika sekta ya afya umeendelea kwa muda mrefu na umewezesha wananchi wengi, hususan waliopo maeneo ya vijijini, kupata huduma za afya.
Ameongeza kuwa TCMA itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma hizo na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zinazokidhi mahitaji yao.
Akizungumza katika mkutano huo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania na Makamu wa Pili wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Nelson Kisare, amewataka watoa huduma za afya kuacha mtazamo wa kumwona mgonjwa kama fursa ya kujipatia fedha, akisisitiza kuwa “ugonjwa si fursa.”
Amesema taaluma ya udaktari ni huduma inayohitaji uaminifu, weledi na kuheshimu utu wa binadamu, hivyo wagonjwa wanapaswa kuhudumiwa kwa haki, upendo na huruma bila kugeuzwa kuwa vitega uchumi vya watu binafsi.
Askofu Kisare pia amewataka watoa huduma kuwa waadilifu katika matumizi ya dawa, vifaa tiba na rasilimali nyingine za hospitali, akisema matumizi mabaya ya rasilimali hizo yanaweza kudhoofisha ubora wa huduma na kupunguza imani ya wananchi katika mfumo wa afya.
Amesema Serikali na wadau wa afya wanapaswa kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, hasa katika kuhakikisha wananchi kutoka kaya zenye uwezo mdogo wanatambuliwa na kupata huduma kwa urahisi. Amesema bado kuna changamoto ya uelewa kuhusu namna kaya maskini zinavyotambuliwa, mahali pa kujiandikisha na huduma zinazolipiwa kupitia mfumo huo.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TCMA na Katibu wa Afya wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Dkt. Paulina Arkard, amesema chama hicho kiko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora bila kujali maeneo wanayoishi au uwezo wao wa kifedha.
Amesema afya ya akili mahali pa kazi pia imepewa kipaumbele katika mkutano huo kutokana na umuhimu wake katika ustawi wa watumishi na ubora wa huduma wanazowapa wananchi.
Amesema Mkutano huo, uliofanyika kwa kuendelea na utaratibu wa mikutano ya kila mwaka tangu kuanzishwa kwa TCMA mwaka 1937, umejadili pia changamoto zinazokabili hospitali za taasisi za dini.
Naye Katibu wa Hospitali ya Kilutheri Machame, Kilimanjaro, Blessing Kisanga, amesema baadhi ya hospitali zilizoingia mikataba na Serikali zinakabiliwa na changamoto ya kupata watumishi mbadala baada ya watumishi wanaolipwa na Serikali kustaafu.
Amesema hali hiyo hupunguza idadi ya watumishi na kuathiri utoaji wa huduma, hivyo wamekuwa wakihitaji utaratibu wa kupata vibali vya kuajiri watumishi wapya.
Naye Afisa Utawala wa Hospitali ya Mtakatifu Martin, Kilwa Kivinje, Joseph Njenga, amesema changamoto kubwa katika vituo vya afya vya vijijini ni pamoja na uhaba wa watumishi, dawa, vifaa tiba na vifaa vya maabara. Amesema Serikali inapaswa kuendelea kuimarisha upatikanaji wa rasilimali hizo ili wananchi wa vijijini wasilazimike kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
Kwa ujumla, Mkutano Mkuu wa 89 wa TCMA umeendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini katika kuimarisha sekta ya afya, huku washiriki wakieleza kuwa uwekezaji katika rasilimali watu, dawa, vifaa tiba, afya ya akili na Bima ya Afya kwa Wote ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati






Social Plugin