Na Sheila Ahmadi, Ruangwa
Tanzania imejipanga kuongeza thamani ya madini ya marble yanayozalishwa nchini kupitia ujenzi wa kiwanda cha kuchakata madini hayo katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam.
Uwekezaji huo unalenga kuwezesha uchakataji wa marble kufanyika hapa nchini, hatua inayotarajiwa kuongeza thamani ya rasilimali hiyo, kukuza fursa za biashara na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi.
Akizungumza katika Maonyesho ya Madini yaliyofanyika Ruangwa, mkoani Lindi, Hussein Abdalah. kutoka Kampuni ya Team One Marble amesema ujenzi wa kiwanda hicho utasaidia kupunguza utegemezi wa kusafirisha madini ghafi nje ya nchi na badala yake kuwezesha uzalishaji wa bidhaa zenye thamani zaidi ndani ya Tanzania.
Amesema kiwanda hicho kinatarajiwa kutumia malighafi zinazopatikana nchini na kuzalisha bidhaa mbalimbali za marble kwa matumizi ya ndani pamoja na masoko ya nje, hatua ambayo inaweza kufungua fursa zaidi kwa wawekezaji na wafanyabiashara katika sekta hiyo.
uwepo wa kiwanda hicho pia utachochea ukuaji wa shughuli zinazohusiana na uchimbaji, usafirishaji na uchakataji wa marble, huku ukitoa fursa za ajira na kuwawezesha Watanzania kushiriki katika hatua mbalimbali za mnyororo wa thamani wa madini.
Aidha uwekezaji katika viwanda vya kuchakata madini nchini ni sehemu muhimu ya kuongeza manufaa yatokanayo na rasilimali za madini, kwa kuhakikisha madini hayauzwi yakiwa ghafi pekee, bali yanaongezewa thamani kabla ya kufikia soko.
Vilevile hatua hiyo inaakisi fursa iliyopo katika sekta ya madini ya kutumia rasilimali zinazopatikana nchini kukuza uzalishaji wa bidhaa, uwekezaji na shughuli nyingine za kiuchumi zinazoweza kuongeza mapato na ajira kwa Watanzania.


Social Plugin