Na, Elizabeth Cosmas,Shinyanga
Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wametakiwa kuacha kutumia miwani na dawa za macho bila kufanyiwa vipimo na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya ya macho, ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na matumizi yasiyo sahihi.
Ushauri huo umetolewa leo 01 sept,2026 na Mratibu wa Huduma za Tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Alistidi Ngalawa, wakati wa ufunguzi wa kambi ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya macho inayofanyika katika hospitali hiyo.
Dkt. Ngalawa amesema baadhi ya wananchi wamekuwa na tabia ya kutumia miwani au dawa za macho bila kupata uchunguzi wa kitaalamu, hali inayoweza kuwafanya kutumia huduma zisizoendana na mahitaji yao.
“Tumekuwa tukipokea wagonjwa wa macho wa aina tofauti lakini asilimia kubwa ni kundi la watu wa makamo kuanzia umri wa miaka 40 na kuendelea ambalo kundi hili changamoto yake kubwa ni uonaji hafifu kutokana na kuongeza kwa umri lakini kutokana na geografia ya mikoa mingi ya kanda Ziwa kuwepo kwa hali ya hewa ya kiangazi ,na maeneo yenye vumbi kwa sana na hivyo kupelekea wagonjwa wengi kupata changamoto ya macho kwa asilimia kubwa.
Aidha Dkt,Ngalawa ameongezea kuwa kumekuwa na wimbi kubwa la watu wengi kutumia vifaa vya kujikinga na changamoto ya macho na njia za asili ili kupona kwa haraka na hivyo kutoa rai kwa wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga kuacha kujichukulia maamuzi ya kutumia njia zozote za kujikinga na kuwaona matabibu kwa ushauli wa kitabibu zaidi.
"Nitoe wito kwa wananchi wote kuacha kuamini imani za nje bila kwenda kuwaona wataalamu wanahusika na changamoto zote za macho wananchi wanapaswa kuhakikisha wanapata vipimo na ushauri wa kitaalamu kabla ya kutumia miwani au dawa za macho”
Dkt ,Paul kabuche akitoa wito kwa wananchi kuja kufanya vipimo katika hospitali hiyo.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Macho kutoka Hospitali ya Mkoa wa Simiyu, Dkt. Paul Kabuche, ambaye anaongoza huduma katika kambi hiyo, amesema kuna sababu mbalimbali zinazoweza kuchangia kuongezeka kwa changamoto za afya ya macho, hususani katika maeneo ya Kanda ya Ziwa.
Dkt. Kabuche amesisitiza umuhimu wa wananchi kufanya uchunguzi wa macho mapema ili kubaini matatizo yote yanayosababisha magonjwa ya macho kabla hayajaendelea na kusababisha madhara makubwa.
“Kuna sababu mbalimbali ambazo zinasababisha kuwepo kwa changamoto ya afya ya macho na mpaka sasa katika kambi yetu tumepokea makundi tofauti tofauti ambayo yameathilika na tatizo hili hasa kundi la wazee ambao changamoto yao kubwa ikiwa ni uonaji hafifu kutokana na kuongezeka kwa umri na hivyo kupelekea kuona kwa shida lakini sababu nyingine ikiwa ni pumu ya macho , presha n.k na kutambua changamoto hizo na moja ya njia ya kutambua changamoto hizo ni kuja kufanya uchunguzi wa kitabibu na niseme tu kuwa wananchi wote Ni muhimu kufanya uchunguzi wa macho ili kubaini tatizo na kupata huduma ya matibabu yanayostahili.”
Mwananchi akitoa wito kwa wakazi wote wa Mkoa wa Shinyanga kuja kupata matibabu ya kitaalamu.
Aidha, baadhi ya wananchi waliojitokeza katika kambi hiyo kwa ajili ya uchunguzi na kupata matibabu ya macho wameeleza kufurahishwa na huduma walizopata, huku wakitoa wito kwa wananchi wengine kujitokeza na kutumia fursa hiyo Bertha Yohana ni mkazi wa Shinyanga ni mmoja ya wanufaika wa kuwepo kwa kambi hiyo amesema kuwa kuletwa kwa daktari bingwa kumewapa nafasi kuja kufanya kubwa ya kuja kufanya uchunguzi wa kina ambapo huduma hiyo imesogezwa ndani Mkoa wao
“Tunawashukuru wataalamu kwa kuona umuhimu wa kuleta huduma hii katika hospitali yetu ya hapa Mwawaza ili kila wananchi mwenye changamoto ya macho apate nafasi ya kupata matibabu ya kitaalamu zaidi lakini tunashukuru kwa huduma wanazotupatia. Tunawaomba wananchi wengine wajitokeze kwa wingi ili nao waweze kupata huduma hii na kufahamu hali za afya zao"

Kambi hiyo ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya macho inaendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, ambapo wananchi wanapata fursa ya kufanyiwa uchunguzi na kupata huduma za kitaalamu kuhusu afya ya macho.
Lengo ni kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwahamasisha kuchukua hatua mapema pale wanapobaini changamoto za uoni au dalili za magonjwa ya macho.













Social Plugin