Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TADB YATAJWA KUWA NGUZO KATIKA MAPINDUZI YA KUCHOCHEA UZALISHAJI WA MAFUTA YA KULA




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Wakati Serikali ikiendelea na juhudi za kupunguza utegemezi wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendelea kujidhihirisha kuwa mhimili muhimu wa mageuzi ya sekta ya kilimo kupitia uwekezaji unaowezesha kuanzishwa na kupanuliwa kwa viwanda vya uchakataji wa mazao nchini.

Mafanikio hayo yamebainishwa katika Maonesho ya 33 ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, alitembelea banda la TADB na kupata maelezo kuhusu mchango wa benki hiyo katika kuongeza uzalishaji wa kilimo na kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao.

Akiwa ameambatana na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, Makamu wa Rais alielezwa na Mkurugenzi wa Mipango, Ushauri na Mahusiano ya Taasisi wa TADB, Mkani Waziri, kuwa benki hiyo imeendelea kutoa mikopo na huduma za kifedha kwa wakulima, wafugaji, wavuvi pamoja na wawekezaji katika sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji, tija na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.

Alisema uwekezaji huo umewezesha biashara nyingi za kilimo kukua kutoka uzalishaji wa kawaida hadi viwanda vya kisasa vinavyoongeza thamani ya mazao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Ushuhuda wa mafanikio hayo ulitolewa na Mkurugenzi wa Kiwanda cha Mafuta ya Kula cha Trolle Meesle, Daniel Amulike, aliyesema ufadhili wa TADB umeiwezesha kampuni hiyo kujenga kiwanda cha kisasa na kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula kutoka tani 30 hadi tani 624 kwa mwezi.

Alisema ongezeko hilo limeongeza uwezo wa kampuni kununua mazao kutoka kwa wakulima, kuzalisha mafuta mengi zaidi ya kula na kuchangia juhudi za Serikali za kupunguza uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.

"Baada ya kufadhiliwa na TADB tumetoka kuzalisha tani 30 kwa mwezi hadi kufikia tani 624 za mafuta safi ya kula kwa mwezi kupitia kiwanda cha kisasa," alisema Amulike.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, alisema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta pamoja na kuimarisha uwekezaji katika viwanda vya uchakataji ili kuongeza kiwango cha kujitosheleza kwa mafuta ya kula nchini.

Alisema ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za kifedha kama TADB ni msingi muhimu wa kufanikisha mageuzi ya sekta ya kilimo, kuongeza thamani ya mazao, kufungua masoko kwa wakulima na kukuza uchumi wa viwanda unaolenga kuinua kipato cha wananchi na uchumi wa Taifa.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com