Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAWATAKA WAKULIMA KUTUMIA TEKNOLOJIA KUONGEZA THAMANI YA MAZAO



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

SERIKALI imewataka wakulima, wafugaji na wavuvi kuachana na utegemezi wa mbinu za jadi pekee na kutumia maarifa, taarifa sahihi pamoja na teknolojia za kisasa ili kuongeza tija, ubora na thamani ya mazao yanayozalishwa nchini.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi hayaishii kuuzwa katika hali ghafi, bali yanachakatwa na kuongezewa thamani kupitia viwanda, hatua itakayoongeza kipato cha wazalishaji, ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Akizungumza Nanenane Dodoma Agosti 7,2026  katika mkutano ulioandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na wadau mbalimbali, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Denis Londo amesema matumizi ya maarifa na taarifa sahihi ni msingi muhimu wa kuongeza tija katika uzalishaji na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema Serikali imejipanga kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinaongezewa thamani kupitia viwanda kabla ya kufikishwa kwa walaji na masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, Serikali pia itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wazalishaji kwa kuboresha miundombinu ya barabara kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na kuendelea kutoa ruzuku kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji.
TEKNOLOJIA KUTAMBUA SUMUKUVU KWA HARAKA

Katika mkutano huo, umuhimu wa matumizi ya sayansi na teknolojia umepewa uzito, huku wadau wakieleza kuwa ubora wa mazao ni miongoni mwa vigezo muhimu vinavyoamua uwezo wa Tanzania kushindana katika masoko ya kimataifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo kwa Utaratibu wa Koroba nchini, Geoffrey Kilenga, amesema Tanzania ina fursa kubwa ya masoko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), pamoja na masoko ya Ulaya, Asia na Marekani.

Hata hivyo, amesema fursa hizo haziwezi kutumika kikamilifu bila kuhakikisha mazao yanayozalishwa nchini yana ubora unaokidhi viwango vinavyotakiwa katika masoko hayo.

Amesema mkutano huo umeonesha namna sayansi na teknolojia zinavyoweza kusaidia kuthibitisha ubora wa mazao kwa ufanisi zaidi, akitolea mfano kifaa kipya cha AflaBox, kinachoweza kusaidia kubaini kwa haraka uwepo wa sumukuvu (aflatoxin) katika nafaka bila kulazimika kupeleka sampuli maabara.

Kwa mujibu wa Kilenga, matumizi ya teknolojia hiyo yanaweza kuwasaidia wakulima, wasindikaji na wanunuzi kupata taarifa ya ubora wa mazao mapema kabla hayajapelekwa sokoni.

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda afya za walaji, kupunguza hatari ya bidhaa zisizo salama kuingia sokoni na kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya kimataifa.
WITO KWA WANANCHI

Kilenga amewataka wananchi kuwa makini katika ununuzi wa mazao kwa kuchagua bidhaa zinazotoka katika maeneo na kwa wazalishaji wanaozingatia viwango vya ubora na usalama wa chakula.

Aidha, amewataka wakulima na wadau wengine wa sekta ya kilimo kuendelea kutumia ushauri wa wataalamu ili kuboresha uzalishaji, usindikaji na uhifadhi wa mazao.

Amesema matumizi sahihi ya maarifa na teknolojia, yakichanganywa na uzalishaji unaozingatia viwango, yanaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuhakikisha Tanzania haitoi tu mazao mengi, bali inazalisha bidhaa zenye ubora, thamani na ushindani mkubwa katika masoko ya ndani na kimataifa.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com