Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YASISITIZA MNYORORO WA THAMANI KUWA UFUNGUO WA MAFANIKIO YA SEKTA YA KILIMO




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Serikali imezitaka taasisi zote zinazohusika na sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, fedha, viwanda na biashara kuimarisha ushirikiano ili kujenga mnyororo kamili wa thamani utakaoongeza tija, ubora wa bidhaa na ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Rai hiyo ilitolewa Agosti 2, 2026 na Waziri wa Fedha, Khamis Musa Omary, alipotembelea mabanda ya taasisi mbalimbali katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma, ambapo alijionea teknolojia, bidhaa na huduma zinazotolewa na taasisi za Serikali pamoja na sekta binafsi.

Waziri Omary alisema kuongeza uzalishaji wa mazao pekee hakutoshi ikiwa bidhaa hizo hazitachakatwa, hazitazingatia viwango vya ubora na kushindwa kufikia masoko yenye uhakika.

Alieleza kuwa mafanikio ya sekta za uzalishaji yanategemea ushirikiano wa wadau wote katika kila hatua ya mnyororo wa thamani, kuanzia uzalishaji, usindikaji, upatikanaji wa mitaji, uthibitishaji wa ubora hadi bidhaa kufika kwa mlaji.

"Wadau wote wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha mnyororo mzima wa uzalishaji unaimarika, kuanzia uzalishaji wenyewe, usindikaji, upatikanaji wa mitaji, viwango vya ubora hadi bidhaa kufika sokoni," amesema.

Amesema ushirikiano huo utasaidia kuondoa vikwazo vinavyopunguza tija, kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta za uzalishaji.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika tafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia ili kupata suluhisho la changamoto zinazowakabili wakulima, wafugaji na wavuvi, akibainisha kuwa hatua hiyo itaongeza uzalishaji wenye tija na thamani zaidi.

Katika ziara hiyo, Waziri huyo pia alionesha kuvutiwa na maendeleo ya sekta ya ufugaji wa samaki, akisema ni eneo lenye fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji wa chakula chenye virutubisho, kuinua kipato cha wananchi na kupanua fursa za biashara.

Alibainisha kuwa kutokana na changamoto zinazoikabili sekta ya uvuvi wa asili katika bahari na maziwa, kuna umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika ufugaji wa samaki ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya soko.

Vilevile, amewataka wadau wa viwango kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa nchini zinakidhi matakwa ya masoko ya kikanda na kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa kutangaza zaidi bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wa ndani ili kuongeza uelewa wa wananchi na kupanua fursa za biashara.

Akihitimisha ziara yake, Waziri Omary amesema mafanikio ya sekta za kilimo, mifugo na uvuvi hayatategemea uzalishaji pekee, bali uwezo wa kujenga mnyororo imara wa thamani unaounganisha uzalishaji, usindikaji, ubora na masoko kwa manufaa ya uchumi wa Taifa.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com