Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MZUMBE YATEKELEZA MIRADI YA SHILINGI BILIONI 15.6 KUBORESHA ELIMU YA JUU



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Uwekezaji katika miundombinu ya elimu ya juu nchini umeendelea kuwa chachu ya kuongeza ubora wa mafunzo, utafiti na ubunifu, huku Chuo Kikuu Mzumbe kikieleza kuwa kimekamilisha na kutekeleza miradi 27 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 15.6 katika mwaka wa fedha 2025/26.

Miradi hiyo imeelekezwa katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kuimarisha huduma kwa wanafunzi na watumishi pamoja na kuongeza uwezo wa chuo kutoa huduma za kitaaluma kwa jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya chuo hicho, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.William Mwegoha amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa chuo kuongeza uwezo wa kudahili wanafunzi na kukidhi mahitaji yanayobadilika katika sekta ya elimu ya juu.

Chuo Kikuu Mzumbe, ambacho ni taasisi ya umma chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 21 ya mwaka 2001, lakini historia yake inaanzia mwaka 1953 kilipoanzishwa kama Kituo cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa (Local Government Training Centre).

Amesema Mwaka 1972 kilibadilishwa na kuwa Taasisi ya Usimamizi wa Maendeleo (Institute of Development Management-IDM), kabla ya kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kinachotoa mafunzo katika ngazi mbalimbali ikiwemo astashahada, stashahada, shahada ya awali, shahada ya uzamili na uzamivu.

Kwa sasa chuo kina programu takribani 100 katika maeneo mbalimbali kama uongozi, utawala, sheria, fedha, uchumi, TEHAMA, maendeleo, elimu, takwimu, masoko na ununuzi.

WANAFUNZI WAFIKIA 17,955


Amesema Kwa mwaka wa masomo 2025/26, chuo kina jumla ya wanafunzi 17,955 katika kampasi zake tatu, idadi ambayo imeongezeka kutoka wanafunzi 13,074 waliodahiliwa mwaka 2021/22.

Chuo kinalenga kuongeza idadi hiyo hadi wanafunzi 22,000 katika mwaka wa masomo 2026/27.

Chuo kina kampasi tatu ambazo ni Kampasi Kuu Morogoro, Kampasi ya Mbeya na Kampasi ya Dar es Salaam yenye vituo vya Upanga na Tegeta. Pia kinaendelea na hatua za mwisho za uanzishaji wa kampasi mpya katika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga.

MIRADI 27 YENYE THAMANI YA SH BILIONI 15.6

Katika utekelezaji wa miradi ya mwaka 2025/26, Chuo Kikuu Mzumbe kimeeleza kuwa kimewekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo ujenzi na ukarabati wa majengo ya taaluma na utawala, viwanja vya michezo, studio ya kisasa ya kutengeneza maudhui ya kufundishia kwa njia ya mtandao pamoja na madarasa janja (smart classroom).

Miradi mingine ni pamoja na ukamilishaji wa jengo la upasuaji na maboresho ya vituo vya afya katika kampasi zake, ukarabati wa hosteli za wanafunzi, ujenzi wa barabara za ndani, uchimbaji wa visima vya maji, ufungaji wa kamera za ulinzi (CCTV), taa za barabarani zinazotumia nishati ya jua pamoja na maboresho ya miundombinu ya TEHAMA.

Chuo pia kimeongeza uwezo wa mtandao kutoka megabaiti 650 kwa sekunde (650 Mbps) hadi megabaiti 1,140 kwa sekunde (1140 Mbps) katika kampasi zake zote.

Mbali na miundombinu, chuo kimenunua vifaa mbalimbali vya TEHAMA, mashine za uchapishaji, magari matatu ya viongozi, basi kubwa la Yutong kwa ajili ya huduma za wafanyakazi pamoja na lori la tipper kwa ajili ya shughuli za ujenzi.

MRADI WA HEET WAONGEZA NGUVU

Kupitia mradi wa HEET, Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa madarasa na kumbi za mihadhara, kituo cha TEHAMA pamoja na miundombinu ya maji na majitaka katika Kampasi Kuu Morogoro.

Katika Kampasi mpya ya Tanga, mradi huo umehusisha ujenzi wa majengo ya madarasa, mihadhara, hosteli za wanafunzi, nyumba za watumishi, kituo cha afya na bwalo la chakula.

Uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa chuo kutoa huduma bora za elimu na kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kupata mazingira rafiki ya kujifunzia.

MWELEKEO WA MWAKA 2026/27

Kwa mwaka wa fedha 2026/27, Chuo Kikuu Mzumbe kimepanga kutekeleza miradi yenye thamani ya Sh bilioni 4.83 kupitia fedha za ndani.

Baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa awamu ya pili wa Kituo cha Afya Kampasi ya Mbeya kwa Sh milioni 420, ukarabati wa bweni la Abdel Nasser Mbeya kwa Sh milioni 444, ukarabati wa nyumba za watumishi Kampasi Kuu kwa Sh milioni 300 pamoja na kuendelea na ujenzi wa jengo la taaluma katika Kampasi ya Dar es Salaam Tegeta kwa Sh bilioni moja.

Pia chuo kinatarajia kununua ambulance na basi dogo la wafanyakazi kwa Kampasi ya Tanga, kuimarisha mtandao wa TEHAMA, kuendesha tafiti za kitaaluma ikiwemo matumizi ya akili mnemba (AI), pamoja na kutoa mafunzo kwa watumishi yenye thamani ya Sh bilioni 1.1.

TEHAMA YAIPA MZUMBE SIFA

Katika eneo la TEHAMA, Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kuwa miongoni mwa taasisi zinazofanya vizuri kwa matumizi ya mifumo ya kidijitali.

Chuo kimekuwa kikisaidia taasisi mbalimbali za umma na elimu katika matumizi ya mifumo kama National Data System, eOffice, GMS, PEPMIS, Investment Single Window, ARMS na mifumo mingine ya kidijitali.

Kutokana na uwezo huo, chuo kimefikia daraja la nne la ukomavu wa matumizi ya TEHAMA, huku kikiendelea na mikakati ya kufikia daraja la tano ambalo ndilo la juu zaidi.

KUONGEZA MAPATO KUPITIA UWEKEZAJI

Katika hatua nyingine, Chuo Kikuu Mzumbe kimeanza mikakati ya kuongeza mapato yake kwa kutumia fursa za uwekezaji katika maeneo ya ardhi yaliyopo mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Arusha na Mbeya.

Hatua hiyo inalenga kupunguza utegemezi mkubwa wa mapato ya ada za wanafunzi ambayo yanachangia zaidi ya asilimia 90 ya mapato ya chuo lakini hayatoshi kugharamia mahitaji yote ya maendeleo.

Chuo pia kimeeleza kuimarisha ushirikiano na vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi, sekta binafsi pamoja na wahitimu kupitia mfuko wa ufadhili wa wanafunzi (MUASF).

Kupitia mfuko huo, kuanzia mwaka 2026/27 wanafunzi wanne wenye changamoto za kifedha watanufaika na ufadhili wa masomo.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe amewashukuru wadau mbalimbali wakiwemo Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na waandishi wa habari kwa mchango wao katika kuhabarisha jamii kuhusu maendeleo ya chuo hicho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com