Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWENGE WA UHURU WAZINDUA JENGO LA TIBA KWA WARAIBU WA DAWA ZA KULEVYA KAHAMA


Jengo la Kliniki ya Huduma za Tiba Saidizi kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya (Medically-Assisted Treatment – MAT) katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga limekamilika kwa asilimia 100 na kuzinduliwa rasmi, likiwa na thamani ya Shilingi milioni 438.

Jengo hilo limejengwa kwa fedha kutoka Serikalini kwa kushirikiana na wadau, likiwa na lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma za matibabu, malezi, ushauri na ufuatiliaji kwa watu wanaokabiliwa na utegemezi wa dawa za kulevya.

Ujenzi wa jengo hilo ulianza mwaka 2025 na limeanza kutoa huduma tangu mwezi Mei 2026, huku likitarajiwa kuwa sehemu muhimu ya juhudi za Manispaa ya Kahama katika kupambana na madhara yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya, hususan miongoni mwa vijana.
Akizindua jengo hilo Agosti 21,2026, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mang’onda, amepongeza Serikali na wadau kwa kuwezesha ujenzi wa kituo hicho, akisema kitasaidia kuwaokoa waraibu na kuwawezesha kurejea katika maisha ya kawaida.

Mang’onda amesema tatizo la matumizi ya dawa za kulevya limekuwa likiathiri vijana kwa kuwaondolea mwelekeo wa maisha na kuwanyima taifa nguvu kazi muhimu.

“Ninawaomba vijana waache kujihusisha na matumizi mabaya ya dawa za kulevya, kwa sababu yanawapotezea dira ya maisha na nguvu kazi ya taifa. Nawashauri vijana wafanye kazi halali zenye kuwaingizia kipato,” amesema Mang’onda.
Aidha, amewataka vijana kuwa na tabia njema, kujishughulisha na shughuli za uzalishaji na kutumia fursa zinazotolewa na Serikali ili kujikwamua kiuchumi.


“Vijana wenzangu, tukiwa na tabia njema na kujishughulisha, hata Rais wetu Samia Suluhu Hassan, ambaye ni mama yetu, ataendelea kufurahi na kutuwekea mikakati ya namna ya kutuinua kiuchumi. Tuchukulie mfano wa mama zetu nyumbani; tunapofanya mambo kinyume, huwa wanasikitika. Ndivyo ilivyo kwa Serikali. Hivyo, tuendelee kumfurahisha mama,” amesema.

WARAIBU WAIOMBA SERIKALI KUWADHIBITI WAFANYABIASHARA WA DAWA ZA KULEVYA

Wakati wa uzinduzi huo, baadhi ya waraibu wanaopatiwa matibabu katika kliniki hiyo wameiomba Serikali kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya wauzaji na wasambazaji wa dawa za kulevya ili kupunguza upatikanaji wa dawa hizo, hasa kwa vijana.
Wamesema pamoja na kuwapatia huduma za matibabu na ushauri, ni muhimu pia Serikali kuendelea kuwabaini na kuwachukulia hatua wale wanaohusika na biashara na usambazaji wa dawa za kulevya.

Miongoni mwa waraibu wanaopatiwa huduma katika kituo hicho ni Mutazi Maganga na Asia Wanga, ambao wameomba juhudi zaidi ziendelee kuwekwa katika kudhibiti dawa hizo ili kulinda kizazi cha vijana na kuzuia watu wengine kuingia katika matumizi.

Akizungumza kuhusu hali ya kituo hicho, Msimamizi wa Huduma kwa Waraibu Manispaa ya Kahama, Dkt. Grace Nzangamba, amesema hadi sasa kituo hicho kinahudumia waraibu 35 wanaopatiwa matibabu.

Dkt. Nzangamba ameitaka jamii kutowaficha au kuwanyanyapaa watu wenye changamoto ya matumizi ya dawa za kulevya, bali kuwasaidia kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya kupata matibabu na ushauri kwa wakati.

Amesema kupata huduma mapema ni muhimu kwa sababu humsaidia mhusika kuanza mchakato wa kurejea katika hali yake ya kawaida na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza endapo tatizo hilo litaachwa bila matibabu.

Akijibu ombi la waraibu kuhusu kupambana na wauzaji na wasambazaji wa dawa za kulevya, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mang’onda, amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) pamoja na Jeshi la Polisi itaendelea kuongeza juhudi za kukabiliana na tatizo hilo.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanafanyika kwa pande zote mbili, ikiwemo kuwasaidia waraibu kupata matibabu na kuchukua hatua dhidi ya wanaohusika na uzalishaji, uuzaji na usambazaji wa dawa hizo.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kahama, Baraka Msumi, amesema jengo hilo limekamilika kwa asilimia 100 baada ya ujenzi wake kuanza mwaka 2025.

Amesema uwepo wa jengo hilo umeongeza uwezo wa Manispaa ya Kahama kutoa huduma maalumu kwa waraibu wa dawa za kulevya katika mazingira bora na yenye kuzingatia mahitaji yao ya kiafya na kijamii.

Kukamilika kwa jengo hilo kunatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha huduma za afya kwa waraibu wa dawa za kulevya na kuongeza nafasi ya kuwasaidia waathirika kurejea katika maisha ya kawaida, familia zao na shughuli za uzalishaji.

Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 zinaongozwa na ujumbe usemao: “Tanzania Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo.”



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com