Na Sheila Ahmadi, Dar es salaam
Serikali imeahidi kuharakisha mchakato wa kuanzisha Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Uchukuzi nchini, ambapo ni hatua inayolenga kuimarisha taaluma hiyo, kuongeza ubora wa huduma na kuboresha ufanisi wa sekta ya uchukuzi nchini.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es salaam na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Mwigulu nchemba Mara baada ya kufungua Kongamano la Wataalamu wa Usafirishaji na Lojistiki lililofanyika katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ambapo amesema kuwa Serikali imezipokea hoja zilizowasilishwa na wataalamu wa sekta hiyo na kwamba zinaendana na azma ya kuboresha utoaji wa huduma katika taasisi za umma.
Aidha, Waziri Mkuu alisema Serikali itafanyia kazi pendekezo la kuanzisha vitengo maalumu vya usimamizi wa usafirishaji katika wizara, taasisi za umma na halmashauri, hatua itakayosaidia kuboresha matumizi ya rasilimali za Serikali, hususan magari na mifumo ya usafiri.
Sanjari na hayo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya reli, bandari, viwanja vya ndege na usafiri wa majini, jambo ambalo limeongeza mchango wa sekta ya uchukuzi katika ukuaji wa uchumi na kuongeza mapato ya fedha za kigeni.
"utekelezaji wa Reli ya Kisasa (SGR), maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine pamoja na upanuzi wa viwanja vya ndege kuwa miongoni mwa miradi mikubwa inayoiwezesha Tanzania kuimarisha ushindani wake kama kitovu cha biashara katika ukanda."Amesema Waziri Nchemba."
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dkt. Prosper Mgaya, alisema uwekezaji wa Serikali umeifanya ndoto ya kutoa mafunzo ya urubani nchini kuwa halisi na ufanisi katika utendaji kazi
"chuo chetu kimeandikisha wanafunzi 22 katika programu ya urubani, ambapo wanafunzi wanne wamehitimu huku wanane wakifikia hatua ya kuruka ndege peke yao (solo flight), ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kuhitimu rasmi.
Dkt. Mgaya alisema mafunzo hayo yatasaidia kuziba pengo la marubani wazawa, hususan katika Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ambalo limeendelea kuongeza idadi ya ndege na hivyo kuhitaji wataalamu wengi zaidi." Dkt Mgaya
Naye Rais wa Chama cha Wataalamu wa Lojistiki na Usafirishaji Tanzania (TANTA), Alphonce Mwingira, alisema sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kutokuwepo kwa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Uchukuzi, ukosefu wa vitengo maalumu vya usimamizi wa usafirishaji katika taasisi za umma pamoja na kutokuzingatiwa kwa taaluma husika wakati wa matangazo ya ajira.
Alisema matumizi sahihi ya wataalamu wa uchukuzi yanaweza kupunguza gharama za shughuli za usafirishaji kwa kati ya asilimia 15 na 25, sambamba na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.






Social Plugin