Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADINI YA UJENZI: UTAJIRI UNAOBADILISHA MAISHA YA WANANCHI WA HALI YA CHINI



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Kwa muda mrefu, neno madini limekuwa likiwapa picha Watanzania wengi kuwa ni migodi mikubwa na wawekezaji wenye mabilioni ya fedha.

Kwa wananchi wa hali ya chini, wakiwemo mama lishe wa Dodoma, fundi seremala wa Chunya, kijana wa boda boda wa Singida au mkulima wa Bariadi, sekta ya madini imeonekana kuwa jambo la mbali lisilowahusu.

Hiyo ndiyo dhana ambayo imewafanya maelfu ya Watanzania kubaki watazamaji wa utajiri unaochimbwa kwenye ardhi yao, huku wakiamini kwamba ili unufaike na madini lazima umiliki mgodi au uwe mchimbaji mkubwa.

Lakini ukweli ni kwamba mgodi ni mwanzo tu wa safari ya uchumi wa madini,fedha zinazozunguka sekta ya madini hazitokani na dhahabu au almasi pekee, bali pia madini mengine muhimu yaliyosahaulika, ikiwemo madini ya ujenzi.

Hayo yanawapa nafasi wananchi wa kawaida kunufaika na kubadilisha maisha yao.

Unapolitazama lori lililobeba kokoto likielekea eneo la ujenzi, huenda ukaona ni safari ya kawaida. Unapowaona vijana wakipakia mawe au mchanga machimboni, unaweza kudhani ni kazi ya kujikimu kwa siku moja tu.

Lakini nyuma ya shughuli hizo kuna sekta ya madini ya ujenzi yenye thamani inayochochea ujenzi wa nyumba, shule, hospitali, viwanda, reli na barabara kila siku.

Hata hivyo, pamoja na umuhimu wake katika maendeleo ya taifa, madini ya ujenzi bado hayajatambuliwa na Watanzania wengi kama fursa kubwa ya kiuchumi.

Wengi huyatazama kama mawe na mchanga wa kawaida, badala ya kuyaona kama rasilimali inayoweza kuanzisha biashara, kuzalisha ajira na kuinua maisha ya wananchi wa kipato cha chini.

Nelson Eliya ni mchimbaji wa madini ya ujenzi Dodoma,anasema kokoto, mawe, mchanga, changarawe na udongo wa matofali ndiyo msingi wa karibu kila mradi wa maendeleo unaotekelezwa nchini.

Anaeleza kuwa hakuna nyumba inayojengwa bila mchanga, hakuna daraja linalosimama bila kokoto na hakuna barabara inayokamilika bila mawe na changarawe.

Lakini anasema pamoja na mahitaji hayo makubwa, wananchi wengi wanaoishi karibu na machimbo wameendelea kuwa watazamaji wa uchumi unaozalishwa na rasilimali hizo.

Sababu kubwa si ukosefu wa fursa, bali ni ukosefu wa maarifa.

Anaeleza kuwa watu wengi bado wanaamini kuwa kushiriki kwenye sekta ya madini ya ujenzi kunahitaji mtaji mkubwa au umiliki wa machimbo.

“Ukweli ni kwamba mnyororo wa thamani ya madini haya unaanza kabla ya uchimbaji na unaendelea hadi bidhaa inapomfikia mteja,” anaeleza.

Ametaja fursa ndani ya mnyororo huo kuwa ni pamoja na dereva anayesafirisha mawe, fundi anayehudumia mitambo, mama lishe anayepika chakula kwa wafanyakazi, mkulima anayesambaza mazao, kijana anayefanya biashara ya vifaa vya usalama kazini, fundi wa magari, mchomeleaji, mhasibu, mtaalamu wa TEHAMA na vijana wanaotangaza bidhaa kupitia majukwaa ya kidijitali.

Kwa baadhi ya wanawake wa Dodoma, madini ya ujenzi ni chanzo cha kipato kinachowezesha familia kumudu mahitaji ya kila siku.

Rehema Juma, mkazi wa Mtumba Dodoma anayejishughulisha na biashara ya kokoto na mchanga, anasema shughuli hiyo imekuwa sehemu muhimu ya maisha yake baada ya kuingia kwenye biashara hiyo Kwa kuponda kokoto baada ya kuokota mawe bila kutumia gharama yoyote.
"Kwa siku nilikuwa naponda kokoto na kupata debe mbili ambazo niliuza Kwa bei ya Shilingi 10000 Kwa kila debe moja f dha iliyonisaidia mahitaji yangu ya familia,"anasema

Anasema awali alikuwa akifanya biashara ndogo ndogo zisizo na uhakika wa kipato, lakini baada ya kuona mahitaji makubwa ya vifaa vya ujenzi katika maeneo yanayokua ya Dodoma, aliamua kuanza kununua na kuuza mchanga na kokoto kwa wateja wanaojenga nyumba na wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi.

“Biashara hii imenisaidia sana,kipato ninachopata hapa kimenisaidia kugharamia mahitaji ya familia na kuendeleza biashara yangu,kadiri ujenzi unavyoongezeka, ndivyo na sisi tunavyopata soko,” anasema Rehema.

Kwa upande mwingine, Mariam Hassan, mama lishe anayehudumia wafanyakazi katika eneo lenye shughuli za uchimbaji wa madini ya ujenzi, Kijiji cha Msanga, Wilaya ya Chamwino, Dodoma, anasema uwepo wa machimbo umefungua soko ambalo awali hakulifikiria.

Anasema alianza kwa kuuza chakula kwa wafanyakazi wachache, lakini kadiri shughuli za uchimbaji na usafirishaji zilivyoongezeka, idadi ya wateja nayo ikaongezeka.

Kwa sasa, anasema biashara hiyo imemwezesha kupata kipato cha kila siku na kugharamia mahitaji ya familia.

“Nilianza kuuza sahani chache kama kumi kwa siku lakini sasa nauza mpaka sahani 200 kwa siku na kupata 400,000 kwa siku,hii ilikuwa ndoto kila kitu kinawezekana,” anasema.

Anasema kwa sasa ana uhakika wa maisha na kuwasomesha watoto wake shule nzuri bila wasiwasi.

Kwa mwanamke kama Rehema, kokoto na mchanga ni bidhaa inayoweza kuuzwa na kuleta kipato; kwa Mariam, shughuli hizo ni soko la chakula. Kwa wengine ni ajira ya udereva, ufundi wa magari, uchomeleaji, uuzaji wa vifaa au huduma nyingine.

Hapo ndipo maana ya mwananchi kunufaika na madini ya ujenzi inapojitokeza. Si lazima awe na leseni ya mgodi au lori lake mwenyewe; anaweza kuwa sehemu ya mnyororo huo kwa kutumia nafasi aliyonayo na kuigeuza kuwa chanzo cha kipato.

Zena Hamad ni mnunuzi wa madini ya ujenzi mkoani Dodoma,anaeleza kuwa mnyororo wa thamani wa madini ya ujenzi hauanzi wakati jiwe linapochimbwa na hauishii pale lori linapopakia mzigo.

“Unaanzia kwenye utambuzi wa eneo lenye malighafi, upatikanaji wa leseni, uchimbaji, uchakataji, upakiaji, usafirishaji, biashara na hatimaye matumizi ya bidhaa kwenye miradi ya ujenzi. Kila hatua ina nafasi ya kuzalisha ajira na kipato,” anafafanua.

Licha ya hayo, anatilia mkazo suala la uhifadhi mazingira, akisema kama madini ya ujenzi yanatakiwa kuwa chanzo cha utajiri wa muda mrefu, uchimbaji wake lazima uende sambamba na ulinzi wa mazingira na usalama wa watu.

Anasema machimbo yasiyosimamiwa vizuri yanaweza kuleta mashimo hatari, mmomonyoko wa ardhi, vumbi, kelele na athari nyingine kwa jamii.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Ramadhan Lwamo, madini ya ujenzi yapo katika kundi rasmi la madini yanayozalishwa nchini pamoja na madini ya metali, vito, viwandani na nishati.

Katika ripoti yake ya mwaka 2023/24, Katibu huyo Mtendaji ameeleza kuwa Tume ilisimamia biashara ya madini yenye thamani ya Sh9.741 trilioni, iliyozalisha mapato ya Serikali ya Sh625.09 bilioni kupitia mrabaha na ada za ukaguzi.

Anabainisha kuwa takwimu hiyo haimaanishi kuwa Sh9.741 trilioni zote ni za madini ya ujenzi pekee, bali inaonyesha ukubwa wa uchumi wa biashara ya madini kwa ujumla ambao ndani yake madini ya ujenzi yana nafasi yake.

Anaeleza kuwa changamoto ni kwamba elimu kuhusu mnyororo wa thamani wa madini ya ujenzi bado ni ndogo, ambapo wananchi wengi hawajui taratibu za kuingia kwenye biashara hizi, namna ya kupata leseni, masoko yaliyopo au jinsi ya kuongeza thamani ya huduma wanazotoa.

“Kutokana na hali hiyo, fursa nyingi huishia kwa watu wachache wenye taarifa, uzoefu na mtaji, huku wananchi wa kawaida wakiendelea kushuhudia malori yakibeba utajiri kutoka maeneo yao bila kushiriki kikamilifu katika uchumi huo,” anafafanua.

Tume ya Madini inaeleza kuwa kiwango cha mrabaha kwa makaa ya mawe, madini ya viwandani na madini ya ujenzi ni asilimia 3, huku ada ya clearance na inspection ikiwa asilimia 1 kwa madini yote isipokuwa chumvi na dhahabu inayouzwa katika vituo vya kusafishia.

Kile kinachoonekana kuwa jiwe la kawaida kinaweza kuwa sehemu ya uchumi rasmi wenye thamani na mchango katika mapato ya taifa.


Kadiri Dodoma inavyoendelea kujenga miji, viwanda na miundombinu, mahitaji ya madini ya ujenzi yatazidi kuongezeka. Hii ina maana kuwa sekta hii itaendelea kuwa chanzo cha ajira na biashara kwa miaka mingi ijayo.

Mtaalamu wa masuala ya jiolojia kutoka Tume ya Madini, Francis Mocho, anaeleza kuwa kinachohitajika sasa ni kuwekeza katika elimu ya biashara za madini ya ujenzi, kuwawezesha wananchi kupata mitaji nafuu, kurahisisha upatikanaji wa leseni na kuhakikisha taarifa za masoko zinawafikia watu wengi zaidi.

Anasema madini ya ujenzi yanaweza kuwa daraja la kutoka kwenye umaskini kwenda kwenye ustawi wa kiuchumi ikiwa wananchi wataelewa nafasi yao katika mnyororo wa thamani.

Ametolea mfano wa bei elekezi za Januari hadi Machi 2025, kokoto Dodoma kuwa iliwekewa bei ya Sh34,670 kwa tani.

“Kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2025, Tume iliainisha pia kifusi (morrum) Dodoma kwa Sh12,000 kwa tani na kifusi (gravel) kwa Sh16,670 kwa tani. Hizi si bei za mwisho ambazo kila mwananchi lazima auze au anunue kwa kiwango hicho, kwa sababu gharama za usafirishaji, ubora, eneo na mazingira ya biashara zinaweza kubadilisha bei,” anasema.

Anafafanua kuwa takwimu hizi zinaonyesha kuwa mchanga, kokoto na kifusi vina thamani inayoweza kupimika katika uchumi wa kawaida, kwa maana kwamba kila mwananchi anaguswa na biashara ya madini haya.

“Kwa hiyo, tunapozungumzia mwananchi wa kawaida kunufaika na madini, si lazima tumfikirie mchimbaji pekee. Unaweza kumfikiria dereva anayesafirisha tani kadhaa za kokoto, kijana anayefanya kazi kwenye mashine ya crusher, fundi anayerekebisha lori, mama anayesambaza chakula kwa wafanyakazi au mfanyabiashara anayenunua na kuuza bidhaa hizo,” anaeleza mtaalamu huyo wa jiolojia.

Mwisho wa yote, utajiri wa madini ya ujenzi haupo kwenye mawe pekee, upo kwenye fikra za Watanzania kuhusu namna ya kuyageuza mawe hayo kuwa biashara, ajira na maendeleo.

Pale ambapo fikra zitabadilika, hata jiwe la kawaida linaweza kuwa msingi wa maisha bora kwa maelfu ya familia za Kitanzania.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com