Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHILINGI 300 INAVYO WAGHARIMU WAFANYABIASHARA SOKO LA SABASABA




Na Dotto Kwilasa,Dodoma


Kila siku, maelfu ya wafanyabiashara hukusanyika katika Soko la Sabasaba jijini Dodoma kutafuta riziki,lakini nyuma ya pilikapilika za biashara kuna simulizi ambayo wengi hawaioni,gharama ya Sh300 kwa kila huduma ya choo.

Hali hii imewalazimu baadhi ya wafanyabiashara wenye kipato cha chini kukwepa kutumia vyoo na badala yake kujisaidia kwenye makopo, chupa au maeneo yasiyo rasmi, hali inayotishia afya ya umma, mazingira na utu wa binadamu.

Wengine hulazimika kuchagua kati ya kulinda afya zao au kuhifadhi fedha za kulisha familia zao.

Uchunguzi huu unaonyesha kuwa tatizo la vyoo katika Soko la Sabasaba si suala la usafi pekee, bali pia ni suala la uchumi, afya ya umma na heshima ya binadamu.

Kadri gharama ya huduma hiyo inavyoendelea kuwa juu kwa watu wenye kipato cha chini, ndivyo uwezekano wa kuendelea kwa matumizi ya makopo, chupa na maeneo yasiyo rasmi unavyoongezeka.

Wakati Soko hilo likiendelea kuwa kitovu kikuu cha biashara katika Jiji la Dodoma, changamoto ya miundombinu ya vyoo imeanza kujitokeza si tu kama suala la afya ya jamii, bali pia kama kikwazo kinachoongeza gharama za uendeshaji kwa wafanyabiashara wadogo.

Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara hulazimika kutumia makopo na chupa kujisitiri ili kuepuka gharama ya Sh300 kwa kila matumizi ya choo na wakati mwingine hujisaidia haja ndogo kwenye ndoo na kuchanganya na maji kisha kumwaga barabarani.

Kwa watu wenye kipato cha chini ya Sh2,000 kwa siku, kiasi hicho kinatajwa kuwa mzigo mkubwa unaopunguza mapato yao.

Soko la Sabasaba,ambalo lipo katikati ya Jiji la Dodoma, linahudumia zaidi ya watu 7,200 kila siku, wakiwemo wafanyabiashara wa moja kwa moja wanaokadiriwa kufikia 5,500.

Katika idadi hiyo, vyoo vinavyotumika ni Nane , ambavyo vinamilikiwa na wafabiashara binafsi.

Kutokuwepo kwa choo cha umma katika eneo hilo kunamaanisha kuwa huduma hiyo hupatikana kwa malipo ya juu ambayo ni Sh300 kwa kila matumizi.


Baadhi ya wanawake wanaofanya biashara sokoni hapo wanasema hali hiyo imekuwa chanzo cha athari za kimazingira, kwani wafanyabiashara wasiokuwa na fedha za kutosha hulazimika kujisaidia kwenye vichochoro na maeneo yasiyo rasmi.

Pili Juma, anayejishughulisha na kusambaza chakula kwa wafanyabiashara, anasema hutumia kati ya Sh600 hadi Sh900 kwa siku kwa ajili ya matumizi ya choo.

Kwa mujibu wake, malipo anayopata kwa siku ni takribani Sh2,000, hivyo sehemu kubwa ya kipato chake huishia kulipia huduma hiyo na kumwachia kiasi kidogo kisichozidi Sh1,100 kwa matumizi mengine.

“Ukitoa Sh900 ya choo, unabaki na Sh1,100 ambayo bado inatakiwa igawanywe kwa nauli na mahitaji mengine,bila kutumia ujanja mwingine, unajikuta hakuna kinachobaki kwa ajili ya familia,” anasema .

Anaongeza kuwa changamoto hiyo imekuwa kubwa zaidi kwa wanawake wanaotoa huduma sokoni humo, ambao mara nyingi hulazimika kujisaidia haja ndogo kwenye makopo na kumwaga Hali inayopelekea harufu mbaya na kutishia usalama wa afya.

Hali hii inaonesha namna ambavyo changamoto ndogo ya miundombinu inaweza kuwa na athari kubwa kwa maisha ya kila siku ya wafanyabiashara na mazingira ya biashara katika moja ya masoko makubwa jijini Dodoma.

Malunde Blog imebaini kuwa wasaidizi wengi wa mama lishe na wafanyakazi wa shughuli ndogo ndogo hulipwa wastani wa Sh2,000 kwa siku. Kutokana na mazingira ya kazi, wengi hulazimika kutumia choo mara mbili hadi tatu kwa siku, jambo linalowagharimu kutumia kati ya Sh600 na Sh900.

Kwa kipato hicho, zaidi ya asilimia 40 ya fedha wanazopata huenda kwenye matumizi ya choo pekee.

Matokeo yake, baadhi yao wamekiri kutumia njia mbadala zisizo salama ili kupunguza gharama hizo.

Salma Jafar, anayejishughulisha na Ususi anasema gharama ya choo imekuwa mzigo unaopunguza uwezo wake wa kuhudumia familia.

“Nafanya kazi Saluni ,kwa siku nalipwa 5000,nikienda chooni mara tatu natumia Sh900,nikitoa fedha hiyo nabaki na Sh4100 kumbuka hapo bado nauli ya kunirudisha nyumbani inatokea humo na matumizi mengine,mwisho wa siku hakuna kinachobaki,” anasema.

Anasema hali hiyo imewafanya baadhi ya wafanyakazi kutafuta mbinu mbadala za kujisitiri badala ya kutumia vyoo kila wanapohitaji.

"Kuna wakati nikiwaza hii 5000 Ina matumizi mengi naamua kujisaidia kwenye kopo kisha nachanganya mkojo kwenye maji machafu namwaga nje wapitanjia wanadhani namwaga maji kumbe nimechanganya na mkojo mwisho wa siku maisha yanaendelea,"anasisitiza na kuongeza;

Hii tabia tumewarithisha hata baadhi ya wateja wetu ,wamezoea pia kutumia makopo ,japo kuwa tumeizoea hii tabia na kuiona ya kawaida hatufanyi kwa kupenda tunatamani mabadiliko,"anasema

Naye Monica Gabriel mfanyabiashara wa Matunda anasema wanawake ndiyo waathirika wakubwa wa hali hiyo kutokana na mahitaji yao ya kiafya.

“Mtu akiwa hana fedha ya choo anaanza kutafuta njia nyingine,Wapo wanaotumia makopo ya taka au maeneo yasiyo rasmi kwa sababu hawawezi kumudu gharama ya kila haja ya kwenda chooni,” anasema.

Anasema gharama ya Sh300 inaweza kuonekana ndogo kwa watu wenye kipato kikubwa, lakini kwa mfanyakazi anayepata Sh2,000 kwa siku inapunguza sehemu kubwa ya mapato yake.

Anasisitiza kuwa mbali na athari za kiuchumi, hali hiyo imeanza kuleta changamoto za kiafya na usafi wa mazingira kwa baadhi ya watu na maeneo yanayozunguka soko.

Wamiliki wa vyoo binafsi katika Soko la hilo wanasema ongezeko la gharama za uendeshaji, ikiwemo maji, sabuni na matengenezo, limewalazimu kuendelea kutoza tozo ya Shilingi 300 ili kuendana na gharama za uendeshaji.

Mmoja wa wamiliki hao Lubago Julius anasisitiza kuwa kwa kukosekana kwa vyoo vya umma vinavyosimamiwa na mamlaka husika, wao hulazimika kuendesha huduma hiyo kwa misingi ya biashara huku wakizingatia usafi na uendelevu wa shughuli zao.

"Hali hii imetupa uhuru wa kupanga bei kutokana na kutokuwepo kwa mfumo mbadala wa ushindani, mapato yanayotokana na huduma hutusaidia kugharamia uendeshaji na matengenezo ya kila siku, idadi ya watumiaji hubadilika kulingana na msimu na tabia za baadhi ya wananchi kutafuta njia mbadala za kujisaidia,"amefafanua

Pamoja na kuiona changamoto hiyo kama fursa ya kiuchumi, Lubago anasisitiza kuwa suluhisho la muda mrefu linapaswa kujumuisha uwekezaji wa vyoo vya umma vya kutosha na vinavyopatikana kwa gharama nafuu ili kupunguza mzigo kwa wafanyabiashara na kuboresha afya ya jamii kwa ujumla.

Kutokana na hayo Mtaalamu wa afya ya mazingira kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI)Judith Harrison anasema kuwa masoko makubwa yanapaswa kuwa na mfumo maalum wa “Public Sanitation Subsidy”, ambapo Serikali hushirikiana na sekta binafsi kugharamia sehemu ya uendeshaji wa vyoo ili kupunguza mzigo kwa wananchi.

Anaeleza kuwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki zimefanikiwa kudhibiti changamoto kama hizi kwa kuweka vyoo vya umma vinavyofadhiliwa kwa sehemu na mapato ya ushuru wa soko, hivyo mfanyabiashara halipii kila anapoingia bali hulipia kwa mfumo wa pamoja au punguzo maalum la siku.

Anasisitiza kuwa uwepo wa vyoo vya bei nafuu si suala la hiari bali ni nguzo la afya ya umma, kwani kila hatua ya kukwepa kutumia choo rasmi huongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa ya mlipuko katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.

"Katika muktadha huo, napendekeza uwekezaji wa “vyoo vya kisasa vya jamii” ndani ya masoko, vyenye usimamizi wa moja kwa moja wa halmashauri, ili kuhakikisha huduma inakuwa endelevu, salama na yenye bei nafuu kwa wote,"anasisitiza.

Anasema Wakati Serikali na Uongozi wa soko wakiendelea kutafuta suluhisho, hatua za haraka zinahitajika ili kupunguza gharama hizo na kuzuia kuendelea kwa matumizi ya makopo na maeneo yasiyo rasmi, hali ambayo inaweza kuhatarisha afya ya umma na taswira ya moja ya masoko makubwa zaidi jijini Dodoma.

Naye Afisa Afya Usafishaji kutoka Idara ya Usafi na Udhibiti wa Taka ya Jiji la Dodoma, John Lugendo, anasema matumizi ya maeneo yasiyo rasmi kujisaidia yanaweza kuongeza hatari ya uchafuzi wa mazingira na kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Anasema magonjwa kama kipindupindu, homa ya matumbo na magonjwa ya ngozi yanaweza kuongezeka pale ambapo usafi wa mazingira hautazingatiwa.

“Tabia ya kukwepa kutumia vyoo si salama,inahatarisha afya za watu wanaofanya biashara na hata wateja wanaofika sokoni,elimu ya matumizi sahihi ya vyoo ni muhimu, lakini pia huduma yenyewe inapaswa kupatikana kwa urahisi,” anasema.

Lugendo anaongeza kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la pamoja kati ya Serikali na wananchi, hivyo kila upande unapaswa kuhakikisha mazingira yanabaki salama.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Soko la Sabasaba, Adam Kombo, anakiri kuwepo kwa malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu gharama ya choo.

Anasema uongozi wa soko umeanza kufanya mazungumzo na wamiliki wa vyoo ili kuona uwezekano wa kupunguza gharama hiyo hadi Sh200.

“Tunaendelea kujadiliana nao lakini changamoto wanayoieleza wamiliki ni gharama za uendeshaji ikiwemo maji na vifaa vya usafi.tunaamini tutafikia mwafaka utakaowanufaisha wafanyabiashara na watoa huduma,” anasema.

Kombo anaongeza kuwa pia kuna mpango wa kutafuta suluhisho la muda mrefu litakalowezesha upatikanaji wa huduma za vyoo kwa gharama nafuu zaidi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Usafi wa Mazingira na Udhibiti wa Taka Ngumu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro, anasema mamlaka hiyo inaendelea kushirikiana na uongozi wa soko kutafuta njia bora za kuboresha huduma za usafi.

Anasema lengo ni kuhakikisha wafanyabiashara wanapata huduma bora bila kuathiri afya zao wala mazingira ya biashara.

“Tunataka kuona huduma za vyoo zinakuwa salama, nafuu na zinazokidhi mahitaji ya watumiaji ili kuondoa mazingira yanayoweza kusababisha uchafuzi na magonjwa,” anasema.

Anakiri kuwa mfanyabiashara anayepata Sh2,000 kwa siku, kutumia hadi Sh900 kwa ajili ya choo ni mzigo mkubwa unaoweza kumlazimu kuchagua kati ya kuhifadhi afya yake au kuhifadhi fedha za matumizi ya familia.

Anasema mjadala ukiendelea kuhusu gharama ya huduma ya vyoo suluhisho halipaswi kuishia kwenye kupunguza bei pekee, bali pia kuangalia uwekezaji wa miundombinu ya vyoo vya umma vinavyodhibitiwa na halmashauri.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com