MTATURU AWAVAA WATUMISHI WA UMMA




MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameiomba serikali kuwachukulia hatua wote waliotajwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG),ili kukisafisha Chama Cha Mapinduzi (CCM),na kumsafisha Rais Samia Suluhu Hassan ambaye halali usiku na mchana akitafuta fedha kwa ajili ya wananchi.

Mtaturu ametoa ombi hilo Novemba 3,2023,bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC),kamati ya hesabu za serikali za mitaa (LAAC),na kamati ya hesabu za serikali (PAC),kuhusu ripoti ya CAG.

"Ombi langu wote waliohusika wachukuliwe hatua ili kuisafisha CCM na Mh Rais ambaye halali usiku na mchana akitafuta fedha kwa ajili ya wananchi maskini ,serikali ichukue hatua na maazimio ya kamati pia yazingatiwe na wachukuliwe hatua kwa kuifanya Tanzania kuwa sehemu salama ya kuishi,".amesema.

Amesema kipimo cha serikali inayozingatia utawala bora vipo vingi lakini viwili ndio nguzo yake ambacho cha kwanza ni kufuata demokrasia ,kufuata sheria kwenye kuongoza watu kwa maana ya kutoa haki kwa wananchi wake ikiwemo huduma.

"Haya mambo makubwa matatu ndio yanakuwa yanaangaliwa katika vipimo,la pili ni kuzingatia matumizi bora ya fedha na rasilimali za umma,haya mambo mawili ndio yanabeba sura ya utawala bora,kwa hiyo kwenye hili tumpongeze sana Mh Rais kwa dhamira yake njema,".amesema Mtaturu.

Amesema kutokana vitendo hivyo maneno yake kwamba anatamani nchi iongozwe kwa utawala bora kwa maana ya kuwa na demokrasia na anataka watu waongozwe pamoja na kufuata sheria ili wananchi wapate haki zao.

"Tumekuwa tukimuona waziwazi kwenye hotuba zake mbalimbali,katika utawala duniani unaongozwa na aina mbili viongozi wa kisiasa na watumishi wa umma,kwa hiyo watu hawa wawili ndio wanasaidiana kwa pamoja kuongoza nchi au kuongoza eneo lolote,

"Kama ambavyo tunaona wote Mh Rais Samia anakemea,wabunge tunasimama hapa tunakemea lakini hata madiwani kwenye halmashauri zetu wanakemea kwa maana uongozi wa kisiasa wanayo dhamira njema ya kusaidia nchi hii kwa sababu tunaonekana kila mahali,".ameeleza Mtaturu.

Amesema kwenye taarifa ya PIC kupitia ripoti ya CAG,Bohari ya Dawa (MSD),imeonekana kuna upotevu au kuna madeni yanayokadiriwa kuwa Bil 375 kutokana na kutolipwa madeni.

" CAG jicho lake limeona,lakini kama haitoshi hii inaathiri mtiririko wa utoaji wa dawa, leo tunalalamika vituo vya utoaji wa dawa kwa maana utoaji wa huduma katika halmashauri zetu hakuna dawa hii ni kwa sababu ya mkwamo na halmashauri zetu zimekuwa zikiomba fedha zikiomba dawa au kupeleka maombi ya kununuliwa dawa bado haziletwi kwa sababu kuna deni kubwa lipo pale MSD wanadaiwa,

"Hii maana yake tunasababisha tatizo la huduma kwa wananchi wetu kwa sababu tu kuna baadhi ya watu hawajatimiza majukumu yao hili ni tatizo kubwa na CAG ametuonyesha kwamba kuna tatizo mahali,tujiulize kuna wananchi wangapi wanakufa bila ya dawa vijijini ni namna gani serikali inalaumiwa huko vijijini kwa sababu ya kikwazo hiki,"ameongeza.

Mtaturu amesema eneo la MSD kwa miaka mitatu mfululizo 2019/2020,2020/2021 na 2021/2022, kuna jumla ya dawa aina ya 2,540 zenye thamani ya Sh Bilioni 295 .76 zilipokelewa zikiwa zimebakiza miaka miwili kuisha muda wake lakini kama haitoshi katika hizo dawa zenye thamani ya Sh Bil 28.4 zilikutwa muda wake umeshaisha.

"Mh Mwenyekiti hapa unajiuliza hivi hakuna wataalam ambao wanaenda kutambua dawa hizo kabla hazijaletwa nchini,je wakati wanakagua walikuwa wamefunga macho,je wakati wanakagua vyeti vyao vilikuwa vimefungiwa kabatini kwamba sio wasomi,au watu hao walikuwa hawana roho ya Mungu,Mh Mwenyekiti hawa sio wazalendo wa nchi hii watu hawa ni wageni kutoka nje ya nchi ambao wanawaletea wananchi watanzania dawa zilizoisha muda wake ili wanywe wafe kwa kuwa dawa ikiisha muda wake inakuwa sumu,"ameeleza.

Amesema kuteketeza dawa hizo ni kuteketeza fedha za walipa kodi ambao baadhi wanashurutishwa hawalipi kwa kupenda wenyewe.

" Hawa watumishi wapo wanalipwa mshahara na marupurupu makubwa kabisa kwa kweli jambo hili haliwezi kuvumilika ,nchi yetu inaenda kuwa "Dumping Area", jambo hili haliwezi kupitia kwenye macho ya wabunge makini kama hawa wa CCM ambao wanaweza wakaacha jambo hili liendelee,hii ni hatari kwa afya lakini ni hatari kwa mazingira," amebainisha.

Mbali na MSD Mtaturu ameitaja Wakala wa Manunuzi ya Umma aliyepewa jukumu la kununua magari ya serikali lakini ripoti ya CAG inaonyesha kuna baadhi ya maeneo wamekuta magari hayajanunuliwa na wananchi waliingia taharuki kwamba kuna gari limelipiwa hazijaja nchini.

"Hali hiyo inawafanya wananchi waone tumepigwa kumbe taasisi hii inachelewesha kuleta magari nchini wakati fedha zimeshalipwa na halmashauri zetu,mfano gari za taasisi 14 zenye thamani ya Sh Bilioni 4.2 zilinunuliwa na zilishalipiwa lakini hazijaja nchini maana yake ni kwamba kuna urasimu mkubwa,

"Mkataba unasema utaleta magari ndani ya miezi minne au sita lakini tumeendelea kuletewa gari baada ya miaka miwili mbele,Mh Mwenyekiti jambo hili haliwezi kuvumiliwa kwa sababu wakala huyu amekuwa ana jambo baya,wakati ukinunua gari Japan unapewa ofa ya kufanyiwa service Km 70,000 ila ukinunua maeneo mengine kama wanavyofanya GPSA hiyo ofa hupati hivyo serikali unaipa hasara,".amebainisha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم