TBS YASAINI MKATABA WA USHIRIKIANO NA WAKURUGENZI WATENDAJI WA HALMASHAURI YA MKOA WA MWANZA


Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Ziwa limesaini mkataba wa ushirikiano na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa Mwanza, unaolenga kukaimisha majukumu ya TBS kwa Halmashauri hizo.

Mkataba huo umesainiwa Ijumaa Juni 09, 2023 ukishuhudiwa na Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkataba wa awali baina ya TBS na Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini (OR- TAMISEMI).

Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Happy Kanyeka amesema hatua ya mamlaka hiyo kukaimisha baadhi ya majukumu yake kwa Halmashauri ikiwemo ukaguzi wa ubora na usalama wa bidhaa mbalimbali itasaidia wananchi kupata huduma bora za ukaguzi.

Kanyeka amesema kupitia makubaliano hayo, maafisa wakaguzi wa halmashauri watasaidia ukaguzi wa bidhaa mbalimbali zinazoingia sokoni ikiwemo vyakula na vipodozi na kuchukua hatua mapema kwa bidhaa ambazo hazipaswi kuwa sokoni zikiwemo bidhaa bandia na zenye kemikali zilizopigwa marufuku na hivyo kuondoa madhara yanayoweza kuwapata watumiaji.

“Tunaamini kwa sasa wananchi watapata huduma bora, kwa haraka na karibu zaidi tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo huduma ya kaguzi mbalimbali ilikuwa ikifanywa na maafisa wa TBS pekee” amesema Kanyeka.

Naye Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya amewataka Watendaji wa Halmashauri waliokasimishwa mamlaka ua ukaguzi na TBS kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kama ilivyokusudiwa na kuwaepusha kutumia bidhaa zisizopaswa kuwa sokoni.

Baada ya zoezi la kusaini mkataba huo, TBS pia imekabidhi vishikwambi kwa halmashauri zote nane za Mkoa Mwanza ambavyo vitasaidia ukusanyaji wa taarifa za kaguzi mbalimbali ili kuhakikisha bidhaa za vyakula na vipodozi zinazozalishwa ndani na nje ya nchi zinakidhi viwango kabla ya kuingizwa sokoni.

"Makubaliano haya yatasaidia ukaguzi wa bidhaa kufanyika katika maeneo mengi zaidi ambayo yalikuwa hayafikiwi kwa wakati kutokana na changamoto za kimazingira na umbali, lakini kupitia maafisa wa Halmashauri itakuwa rahisi kuyafikia maeneo yote" amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Emmanuel Shelembi.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم