MABORESHO YA SERA NA MITAALA YA ELIMU KUZINGATIA MICHEZO,SANAA NA UBUNIFU NCHINI



Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema itahakikisha Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023 pamoja na Mitaala inayoboreshwa inaweka kipaumbele masuala ya Michezo, Sanaa na Ubunifu ili kukuza michezo nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga Juni 13, 2023 Mkoani Tabora wakati wa ufungaji wa mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Wanafunzi wa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) ambapo amesema Rasimu ya Sera ya Elimu una mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 ukurasa 39 imeweka bayana Utambuzi na uendelezaji wa vipaji na vipawa katika elimu na mafunzo.

Mhe. Kipanga ameongeza kuwa fani ya michezo, sanaa na ubunifu duniani inatiliwa mkazo kwa kuwa kitaalamu ndiyo inayojenga na kuimarisha ufahamu na afya ya mwanadamu pamoja na kwamba michezo inaburudisha, inakuza uwezo wa kufikiri kwa namna nyingi.

" Serikali inatambua faida nyingi zinazopatikana kutokana na michezo zikiwemo kuimarisha stadi za kujifunza, kujenga na kuimarisha afya, kujenga nidhamu ya raia, kujenga na kuimarisha mahusiano baina ya raia. Vijana katika nchi mbalimbali wamekuwa wakijipatia kipato kutokana na michezo na sanaa, jambo ambalo imechangia kukuza uchumi wa nchi" amesisitiza Kiongozi huyo.

Naibu Waziri Kipanga amesema kwa sasa wizara imetenga Vyuo vitano vya ualimu vinavyotoa mafunzo ya ualimu kwa fani ya michezo ambavyo ni Butimba, Tarime, Tabora, Ilonga na Mtwara Kawaida. Aidha Chuo cha ualimu Butimba kina fani za michezo, sana aza maonesho, muziki na sanaa ya ufundi.

Mhe. Kipanga ameongeza kuwa Serikali iko makini kuunga mkono juhudi zenye kuhakikisha michezo inalipeleka Taifa katika viwango vya juu kitaifa na kimataifa na kuwataka viongozi wa ngazi zote katika mashindano hayo kusimamia, kufuatilia, na kuhakikisha kuwa mashindano yanavuka mipaka ya nchi.

"Michezo hii itatuwezesha kupata wachezaji mahiri watakaotuwakilisha katika michezo ya wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari ya Afrika ya Mashariki itakayofanyika nchini Rwanda mwezi Agosti mwaka huu" amesema Naibu Waziri huyo.

Naye Mkurugenzi wa Elimu kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa TAMISEMI Vincent Kayombi amesema mashindano ya UMITASHUMTA kwa Mwaka 2023 yamehusisha wanamichezo wanafunzi 3,164 wasichana walikuwa 1531 na wavulana 1633 na walimu, waratibu na viongozi 729 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambao walipata fursa ya kuonyesha vipaji vyao katika michezo ya mpira wa miguu, mikono, wavu, kikapu, netiboli, riadha na mchezo wa goli na sanaa za jukwaani katika vipengele vya ngoma za asili, kwaya na mziki wa kizazi kipya.

Kayombo ameongeza kuwa ili kuwajengea stadi za maisha wanamichezo hao wameshindanishwa katika masuala ya usafi na nidhamu, na kwa kuwa michezo hiyo ni sehemu ya taaluma wa kati wa mashindano walimu na wanamichezo walipata mafunzo maalum ya uamuzi na ukocha ya michezo wanayoshiriki ili kuwajengea umahiri utakaowasaidia kuboresha uwezo wao katika michezo wanayoshiriki.

“Katika ufunguzi wa michezo hii Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango alizindua Mwongozo wa kudumu wa uendeshaji wa mashindaano ya michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA ambao umeanza kutumika katika mashindano ya mwaka huu ambapo umekuwa na manufaa ikiwemo kuwa na mashindani ya haki kwa kuzingatia umri stahiki”amesema…

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Dkt. John Mboya amesema mashindano hayo ambayo yanafanyika kwa mara ya pili mfulilizo yamekuwa na mafanikio makubwa nakushukuru kwa mashindano hayo kuendelea kufanyika kwa mara ya pili katika mkoa huo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم